Mitume wa Quran: Utangulizi (sehemu ya 2 kati ya 2)
Maelezo: Kuwaamini manabii wa Mungu ni sehemu muhimi ya imani ya Kiislamu. Sehemu ya 2 itataja manabii wote waliokuja kabla ya Mtume Muhammad, amani iwe juu yake, waliotajwa katika maandiko ya Kiislamu kuanzia Lutu hadi Yesu.
- Na Imam Mufti (© 2013 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 10 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,882 (wastani wa kila siku: 5)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 1
9. Luti au Loot ametajwa mara 17 katika Qurani. Yeye ni mpwa wa Ibrahimu, mwana wa nduguye Ibrahimu. Luti aliishi kwa ncha ya kusini ya Bahari ya Chumvi. Watu wake walikuwa wa Sodoma na Gomora. Luti alimwamini Ibrahimu na baada ya kurudi kutoka Misri, wakaishi kwa maeneo tofauti. Watu wa Sodoma walikuwa wa kwanza kufanya ushoga. Ndiyo sababu mashoga wakati mwingine huitwa wasodoma. Mke wake hakuwa Muumini. Yeye hakufanya dhambi hiyo, lakini aliikubali. Mawe yalinyesha kama mvua juu ya watu wa Sodoma na Gomora na yaliwaangamiza.
10. Yaqub au Yakobo, mwana wa Isaka na mjukuu wa Ibrahimu anatajwa mara 16 katika Qurani. Jina jingine la Yakobo lilikuwa Israeli. “Bani Israel,” Wana wa Israeli, au Waisraeli walipewa jina hilo kwa sababu yake. Manabii wote wa Kiebrania walitoka kwake, na wa mwisho kati yao alikuwa Eesa au Yesu. Yakobo ni baba wa makabila kumi na mawili yaliyojulikana kama Al-Asbaat (7:160) katika Qurani. Inasemekana alisafiri kuenda kaskazini mwa Iraki, akarudi Palestina na kisha kukaa Misri na kufa hapo. Alizikwa Hebroni, Palestina, pamoja na baba yake kulingana na usia wake wa mwisho. Biblia inataja kuwa Isaka alimwoa Rebeka na mwanawe Yakobo alimwoa Raheli (Rahil kwa Kiarabu).
11. Yusuf au Yosefu, mwana wa Yakobo au Israeli anatajwa mara 17 kwa Qurani. Aliachwa katika kisima huko Yerusalemu na ndugu zake, halafu akapelekwa Misri ambapo alipata cheo cha juu kwa serikali. Baadaye, baba yake, Yakobo, na ndugu zake walikaa Misri.
12. Shuaib au Yethro, aliyetajwa mara 11 katika Qurani, alitumwa kwa watu wa Madyan, na alikuwa mmoja kati ya wana wa Ibrahimu. Shuaib aliishi kati ya wakati wa Lutu na Musa na alikuwa nabii Mwarabu. Watu wake waliabudu mti uitwao Al-Ayka (15:78, 26:176, 38:13, 50:14). Walikuwa wakiwapora watu barabarani, na kuwalaghai katika shughuli za biashara. Basi zikawashukia adhabu kadhaa: Kilio cha kutisha kilichokuwa na tetemeko la ardhi kiliwaangamiza.
13. Ayyub au Ayubu ametajwa mara 4 katika Qurani. Inasemekana aliishi karibu na Bahari ya Chumvi au Dameski. Alikuwa nabii mwenye utajiri aliyetahiniwa na Mungu kwa ufukara na ugonjwa, lakini alikuwa na subira na alisaidiwa na mke wake mwaminifu ambaye alikaa naye kwa kila shida. Hatimaye, Mwenyezi Mungu anawalipa vizuri kwa uvumilivu wao.
14. Yunus au Yona, pia anajulikana kama “Dhun-Noon,” anatajwa mara 4 katika Qurani. Aliishi Ninawi, karibu na Mosul, nchini Iraki. Aliwaacha watu wake kabla Mungu hajampa ruhusa, akaeleka nchi ambayo kwa sasa inajulikana kama Tunisia, lakini aliishia Yafa. Alimezwa na nyangumi, kisha akamtubia Mungu na kurudi kwa watu wake huko Iraki ambapo wote, wakiwa na idadi ya 100,000 walitubu na kumwamini.
15. Dhul-Kifl ametajwa mara mbili katika Qur'ani. Baadhi ya wasomi wanasema alikuwa mwana wa Ayubu, wengine wanasema yeye ndiye Ezekieli wa Biblia.
16. Muusa au Musa ndiye nabii aliyetajwa mara nyingi katika Qurani, akitajwa mara 136. Kabla ya Musa, Yosefu alikuwa ameanza kueneza ujumbe wa umoja wa Mungu (tawhid: ibada ya Mungu Mmoja, Mungu wa kweli) miongoni mwa watu wa Misri. Ujumbe wake uliimarishwa wakati baba yake, Yakobo, na ndugu zake pia walikuja kukaa Misri, wakiwabadilisha polepole watu wa Misri nzima. Baada ya Yusuf, Wamisri waligeuka tena kwa ushirikina (shirk) na watoto wa Yakobo, Waisraeli, wakaongezeka na kupata umaarufu kwa jamii. Musa alikuwa nabii wa kwanza aliyetumwa kwa Waisraeli wakati Farao wa Misri alikuwa akiwafanya watumwa wake. Musa alikimbilia Madyan ili kuepukana na mateso. Mungu alimfanya nabii huko Mlima Toor, ulio katika Sinai na alipewa miujiza tisa kubwa.
17. Haroon au Haruni ni ndugu wa Musa na anatajwa mara 20 katika Qurani.
18,19. Ilyas au Eliya na Yas'a wanatajwa wote mara mbili katika Qurani. Wote wawili waliishi Baalbek.
20,21. Dawud au Daudi anatajwa katika Qurani mara 16. Aliwaongoza Waisraeli kwenye vita na kushinda, na alikuwa na miujiza mingi. Mwanawe, Suleiman au Sulemani anatajwa mara 17 na pia alikuwa mfalme mwenye miujiza mikubwa. Wote wamezikwa Yerusalemu.
22. Zakariyyah au Zekaria anatajwa mara 7. Alikuwa seremala. Alimlea Maria, mama yake Yesu.
23. Yahya au Yohana ni mwana wa Zekaria na anatajwa mara 5. Aliuawa Yerusalemu, na kichwa chake kikapelekwa Dameski.
24. Jina la Eesa au Yesu limetajwa mara 25, Masihi mara 11, na 'mwana wa Maryamu' mara 23. Alizaliwa Bethlehemu, Palestina. Inasemekana alitembelea Misri akiwa na mama yake. Yeye ndiye nabii wa mwisho miongoni mwa Wana wa Israeli.
Manabii watano walikuwa Waarabu: Hud, Salih, Shuaib, Ismail, na Muhammad, amani iwe juu yao. Wanne kati yao walitumwa kwa Waarabu, na Muhammad alitumwa kwa wanadamu wote.
Kwa kumalizia, manabii, wa biblia na wasio wa Biblia, ni watu wenye umuhimu mkubwa katika maandiko ya Kiislamu. Waislamu wanajiona kama warithi wa kweli wa utume wa manabii waliotumwa na Mungu kwa ubinadamu: ibada ya Mungu Mmoja wa Kweli na utiifu Kwake.
Marejeleo yaliyochaguliwa:
1.Ibn Kathir. Qasas ul-Ambiya. Cairo: Dar at-Taba’a wa-Nashr al-Islamiyya, 1997.
2.Ibn Hajr al-Asqalani. Tuhfa ul-Nubala’ min Qasas il-Ambiya lil Imam al-Hafid Ibn Kathir. Jedda: Maktaba as-Sahaba, 1998.
3.Mahmud al-Masri. Qasas ul-Ambiya lil-Atfaal. Cairo: Maktaba as-Safa, 2009.
4.Dr. Shawqi Abu Khalil. Atlas al-Quran. Damascus: Dar-ul-Fikr, 2003.