Hadithi ya Adam (sehemu ya 3 kati ya 5): Kuteremka
Maelezo: Udanganyifu wa Shetani kwa Adamu na Hawa huko Mbinguni na baadhi ya mafundisho tunayoweza kujifunza kwayo.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 22 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 5
- Imetazamwa: 8,565 (wastani wa kila siku: 8)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Uislamu unakataa dhana ya Kikristo ya dhambi ya asili na wazo la kuwa wanadamu wote wamezaliwa wakiwa wenye madhambi hususan kutokana na matendo ya Adam. Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani:
“Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine.” (Kurani 35:18)
Kila mwanadamu anawajibika kwa matendo yake na amezaliwa bila ya doa na asiye na dhambi. Adam na Hawa walifanya kosa, walitubu kwa dhati na Mwenyezi Mungu kwa hekima Yake isiyo kifani akawasamehe.
“Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake Mlezi, na akapotea njia. Kisha Mola wake Mlezi akamteuwa, naye akamkubalia toba yake, naye akamwongoa.” (Kurani 20:121-122)
Wanadamu wana historia ndefu ya kufanya makosa na kusahau. Hata hivyo, iliwezekanaje kwa Adam kufanya kosa kama hilo? Ukweli ni kwamba Adam hakuwa na uzoefu wowote wa minong'ono na hila za Shetani. Adam alikuwa ameona kiburi cha Shetani pindi alipokataa kufuata amri za Mwenyezi Mungu; alijua kwamba Shetani alikuwa adui yake lakini hakujua jinsi ya kustahamili hila na mbinu za Shetani. Mtume Muhammad alituambia:
“Kujua kitu sio sawa na kukiona.” (Saheeh Muslim)
Mwenyezi Mungu alisema:
“na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa dhaahiri?.” (Kurani 7:22)
Mwenyezi Mungu alimpa mtihani Adam kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu. Kwa njia hii Mwenyezi Mungu alimuandaa Adam kwa wajibu wake hapa duniani kama mlinzi na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kutokana na uzoefu huu, Adam alijifunza somo la maana kwamba Shetani ni mjanja, na asiye na shukrani na vile vile ni adui dhahiri wa wanadamu. Adam, ikiwa ni pamoja na Hawa na kizazi chao walijifunza kwamba Shetani ndiye aliyesababisha kufukuzwa kwao kutoka mbinguni. Utiifu kwa Mwenyezi Mungu na uadui dhidi ya Shetani ndiyo njia pekee ya kurudi Mbinguni.
Mungu akamwambia Adam:
“Akasema: Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukikufikieni uwongofu kutoka kwangu basi atakaye ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika, Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki.” (Kurani 20:123)
Kurani inatuambia kwamba baada ya hapo, Adam alipokea maneno kutoka kwa Mola wake; maombi ya toba, ambayo aliomba msamaha wa Mwenyezi Mungu. Dua hili ni nzuri sana na inaweza kutumika wakati wa kuomba msamaha wa dhambi zako kwa Mwenyezi Mungu.
“Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.” (Kurani 7:23)
Wanadamu wanaendelea kufanya makosa na kutenda mabaya. Kadhalika, tunajiumiza wenyewe tu. Kamwe, Madhambi na makosa yetu hayakumdhuru, wala hayawezi kumdhuru Mwenyezi Mungu. Iwapo Mwenyezi Mungu hatotusamehe na kuturehemu, bila shaka basi sisi tutakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara. Tunamuhitaji Mwenyezi Mungu!
“‘Na kwenye ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda.Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo mtatolewa.’” (Kurani 7:24–25)
Adam na Hawa waliondoka mbinguni na kushuka duniani. Kuteremka kwao hakukuwa njia ya udhalilishaji; bali ilikuwa ni heshima. Katika lugha ya Kiingereza tunafahamu vitu kuwa ima katika hali ya umoja au wingi; hali ni tofauti katika lugha ya Kiarabu. Kwenye lugha ya Kiarabu kuna hali ya umoja, kisha kategoria ya nambari ya ziada ya kisarufi inayoashiria mbili. Wingi hutumiwa kwa vitu vitatu na zaidi.
Wakati Mwenyezi Mungu alisema: “Shukeni ninyi nyote” Alitumia neno hilo kwa wingi kuashiria kwamba hakuwa akizungumza na Adam na Hawa pekee bali alikuwa akimaanisha Adam, mkewe na kizazi chake—wanadamu. Sisi, nasaba ya Adam, si wenyeji wa ardhi hii; ila tuko hapa kwa muda, kama inavyojitokeza kwenye maneno: “kwa muda.” Mwisho wetu ni akhera na tumekusudiwa kwenda Peponi au Motoni.
Uhuru wa Kuchagua
Uzoefu huu ulikuwa somo la kimsingi na ulionyesha uhuru wa kuchagua. Iwapo Adam na Hawa wangaliishi duniani, basi wangalihitajika kufahamu hila na mbinu za Shetani, walihitaji pia kuzingatia matokeo mabaya ya dhambi, na Rehema na Msamaha wa Mungu usio na kifani. Mungu alijua kuwa Adam na Hawa wangekula matunda kutoka kwenye mti huo. Alijua kwamba Shetani angewaondolea hatia.
Ni muhimu kuelewa kuwa, ingawa Mwenyezi Mungu anajua matokeo ya matukio kabla hayajatokea na kuyaruhusu, yeye halazimishi mambo kutendeka. Adam alikuwa na hiari ya kuchagua na alivumilia matokeo ya matendo yake. Mwanadamu ana hiari na hivyo yuko huru kutomtii Mungu; lakini kuna matokeo. Mwenyezi Mungu anawasifu wale wanaotii amri zake na anawaahidi malipo makubwa, na anawashutumu wale wanaomuasi na anawaonya dhidi ya kufanya hivyo.[1]
Pale Walipoteremkia Adam na Hawa
Kuna ripoti mbali mbali kuhusu mada ya pale walipoteremkia Adamu na Hawa duniani, ingawaje hakuna maelezo kama hayo yanayotoka kwenye Kurani au Sunnah. Kwa hivyo, tunaelewa kwamba eneo la kuteremshwa kwao ni suala lisilo na umuhimu mkubwa na wala hakuna manufaa kwa uelewa huo, hata kama tungekuwa nao.
Hata hivyo, tunafahamu kwamba Adam na Hawa waliteremshwa duniani katika siku ya Ijumaa. Katika kaida na taratibu iliyosimuliwa kwetu kwa lengo la kutufahamisha kuhusu umuhimu wa siku za Ijumaa, Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie yeye, alisema:
“Siku bora kwa kuchomoza kwa jua ni siku ya ijumaa. Siku moja Adam aliumbwa, na siku hii pia aliteremshwa duniani.” (Saheeh Al-Bukhari)
Ongeza maoni