Yesu, mwana wa Maryamu (sehemu ya 1 kati ya 5): Waislamu wanampenda Yesu pia!
Maelezo: Yesu na muujiza wake wa kwanza, na muhtasari wa wanachoamini Waislamu kumhusu.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 19 Dec 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,999 (wastani wa kila siku: 5)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Wakristo mara nyingi huzungumza juu ya kukuza uhusiano na Kristo na kumkubali katika maisha yao. Wanadai kwamba Yesu ni zaidi ya mtu na alikufa msalabani ili kuwakomboa wanadamu kutoka kwa dhambi ya asili. Wakristo wanazungumza juu ya Yesu kwa upendo na heshima na ni wazi ana nafasi maalumu katika maisha yao namioyoni mwao. Lakini vipi kuhusu Waislamu; wanafikiria nini juu ya Yesu Kristo na anashikilia nafasi gani katika Uislamu?
Mtu asiyejua Uislamu anaweza kushangaa kujifunza kwamba Waislamu wanampenda Yesu pia. Muislamu hatazungumza jina la Yesu bila kuongeza kwa heshima maneno "amani iwe juu yake". Katika Uislamu, Yesu ni mtu anayependwa na kuthaminiwa, ni Mtume na Mjumbe anayelingania watu wake katika ibada ya Mungu Mmoja wa Kweli.
Waislamu na Wakristo wanashirikiana katika imani kadhaa zinazofanana juu ya Yesu. Wote wanaamini kuwa Yesu alizaliwa na Bikira Maria na wote wanaamini kwamba Yesu ndiye Masihi aliyetumwa kwa watu wa Israeli. Wote pia wanaamini kuwa Yesu atarudi duniani katika siku za mwisho. Walakini kwa jambo moja kuu wanatofautiana sana kama mbingu na ardhi. Waislamu wanaamini kwa yakini kwamba Yesu sio Mungu, yeye sio mwana wa Mungu na yeye sio sehemu ya Utatu wa Mungu.
Katika Kurani, Mungu anazungumzia moja kwa moja na Wakristo akisema:
“Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lililo kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake. Wala msiseme: ‘Utatu.’ Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu Mmoja tu. ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote vilivyomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha.” (Kurani 4:171)
Kama vile Uislamu unavyokanusha kimsingi kwamba Yesu alikuwa Mungu, pia inakataa dhana kwamba mwanadamu huzaliwa akiwa ametiwa ila ya aina yoyote ya dhambi ya asili. Kurani inatuambia kuwa haiwezekani kwa mtu mmoja kubeba madhambi ya mwingine na kwamba sisi sote tunawajibika, mbele ya Mungu, kwa matendo yetu wenyewe. "Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine." (Kurani 35:18) Hata hivyo, Mungu, kwa Rehema Yake isiyo na mipaka na Hekima hajawatelekeza wanadamu wajifanyie mambo wanavyotaka. Ametuma mwongozo na sheria ambazo zinaonyesha jinsi ya kuabudu na kuishi kulingana na maamrisho Yake. Waislamu wanahitajika kuwaamini, na kuwapenda Mitume wote; kwani kumkataa mmoja ni kuikataa imani ya Uislamu. Yesu alikuwa mmoja tu miongoni mwa mfuatano mrefu ya Mitume na Wajumbe, akiwaita watu wake kumwabudu Mungu Mmoja. Alikuja hasa kwa Watu wa Israeli, ambao wakati huo walikuwa wamepotea kwa kutofuata njia iliyo wazi ya Mungu. Yesu alisema:
“Na ninasadikisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlioharimishiwa, na nimekujieni na ishara kutokana na Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini mimi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.” (Kurani 3:50-51)
Waislamu wanapenda na kumstahi Yesu. Hata hivyo, tunamuelewa yeye na jukumu lake katika maisha yetu kulingana na Kurani na masimulizi na maneno ya Mtume Muhammad. Sura tatu za Kurani zinaonyesha maisha ya Yesu, mama yake Maryamu na familia zao; kila sura ikitoa maelezo yasiyopatikana katika Biblia.
Mtume Muhammad alizungumzia kuhusu Yesu mara nyingi, na wakati mmoja akimsifu kama kaka yake.
“Mimi ndiye niliye karibu sana na mwana wa Maryamu kuliko watu wote, na mitume wote ni ndugu wa baba, na hakuna mtume alikuja baina yangu na yeye (yaani Isa).” (Saheeh Al-Bukhari)
Hebu tufuatilie kisa cha Yesu kupitia vyanzo vya Kiisilamu ili tuelewe ni vipi na kwa nini nafasi yake katika Uislamu ni muhimu.
Muujiza wa Kwanza
Kurani inatuarifu kwamba Maryamu, binti ya Imran, alikuwa msichana ambaye hajaolewa, safi na mcha Mungu aliyejitolea kumwabudu Mungu. Siku moja alipokuwa amejitenga, Malaika Jibril alifika kwa Maryamu na kumjulisha kwamba atakuwa mama wa Yesu. Jibu lake lilikuwa la woga, mshtuko, na kufadhaika. Mungu alisema:
“...Na ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu, na Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lililokwisha hukumiwa.” (Kurani 19:21)
Maryamu alibeba mimba ya Yesu, na wakati ulipofika wa kuzaliwa kwake, alijiondoa kutoka kwa familia yake na kusafiri kuelekea Bethlehemu. Chini ya mtende, Maryamu alimzaa mtoto wake ambaye ni Yesu.[1]
Maryamu alipokuwa anapumzika na kupona kutokana na maumivu na woga uliohusika na kujifungua peke yake, ilimjia fahamu kuwa lazima arudi kwa familia yake. Maryamu aliogopa na kuwa na wasiwasi alipomfunika mtoto huyo na kumkumbatia mikononi mwake. Angewezaje kuelezea kuzaliwa kwake kwa watu wake? Alisikiliza maneno ya Mungu na akarudi Jerusalemu.
“...Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: ‘Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu.’ Akaenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba...” (Kurani 19:26-27)
Mungu alijua kwamba Maryamu angejaribu kutoa maelezo, watu wake hawangemwamini. Kwa hivyo, kwa hekima Yake, alimwambia asiongee. Kuanzia muda Maryamu aliwakaribia watu wake, walianza kumtuhumu, lakini alifuata maagizo ya Mungu kwa busara na kukataa kujibu. Mwanamke huyu mwenye haya, asiyezini, alimwashiria mtoto mikononi mwake.
Wanaume kwa wanawake waliomzunguka Maryamu walimtazama bila kuamini na walidai kujua wangeweza vipi kuzungumza na mtoto mchanga aliyebebwa mikononi. Basi, kwa idhini ya Mungu, Yesu, mwana wa Maryamu, bado angali mtoto mchanga, alifanya muujiza wake wa kwanza. Aliongea:
“...Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu na amenifanya Mtume; na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia sala na zaka maadamu niko hai, Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai.” (Kurani 19:30-34)
Waislamu wanaamini Yesu alikuwa mtumwa wa Mungu na Mjumbe aliyetumwa kwa Waisraeli wa wakati wake. Alifanya miujiza kwa matakwa na ruhusa ya Mungu. Maneno yafuatayo ya Mtume Muhammad yanaelezea wazi umuhimu wa Yesu katika Uislamu:
“Mwenye kushuhudia ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hana mshirika wala msaidizi, na kwamba Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake, na kwamba Isa ni mja Wake na Mtume Wake, ambaye ni neno ambalo Mwenyezi Mungu alimpa Maryamu na ni roho iliyoumbwa Naye. na kwamba Pepo ni kweli, na Jehanamu ni kweli, basi Mwenyezi Mungu atamuingiza katika milango minane ya Mbinguni anayotaka.” (Saheeh Bukhari and Saheeh Muslim)
Rejeleo la maelezo:
[1] Kwa maelezo ya muujiza wa kupata mimba na kuzaliwa kwake, tafadhali rejelea makala ya Maryamu
Ongeza maoni