Nabii Saleh
Maelezo: Mungu aliwatuma Manabii kwa mataifa yote duniani.
- Na Aisha Stacey (© 2009 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 10 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,657 (wastani wa kila siku: 4)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Mwenyezi Mungu alisema katika Qur'ani kwamba Manabii na Mitume wametumwa kwa kila taifa duniani, na kwamba wote walitangaza ujumbe huo huo: kumuabudu Mungu Mmoja peke yake, Asiyekuwa na washirika wala wana wala mabinti. Manabii wengi waliotajwa katika Qurani na mila za Mtume Muhammad, amani iwe juu yake, wanatambulika, na kuchukuliwa kama manabii katika dini za Kiyahudi na za Kikristo. Hata hivyo, Mtume Saleh ni mmoja kati ya manabii wanne Waarabu na hadithi yake haijulikani sana kote ulimwenguni.
“Na bila ya shaka tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia khabari zao, na wengine hatukukusimulia. Na haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.” (Kurani 40:78)
Ad na Thamud zilikuwa vizazi viwili vikubwa vilivyoangamizwa na Mungu kutokana na uovu wao uliopita kiasi. Baada ya kuangamizwa kwa Ad, Thamud ndio ilikuja baada yao na kurithi nguvu na anasa zao. Watu waliishi maisha ya kitajiri sana, wakajenga majengo makubwa kwenye maeneo tambarare na pia kuyachonga ndani ya milima. Kwa bahati mbaya, maisha yao ya raha yalikuja na ibada ya sanamu na uovu. Alitumwa Nabii Saleh kuwaonya watu wa Thamud, kwamba Mwenyezi Mungu hakupendezwa na matendo yao, na angewanyeshea maangamizi juu yao, ikiwa hawatabadilisha njia zao mbaya.
Saleh alikuwa mcha Mungu aliyeshikilia nafasi ya uongozi katika jamii, lakini wito wake wa kumwabudu Mungu peke yake uliwakasirisha watu wengi. Baadhi walielewa hekima ya maneno yake, lakini wengi wa watu walikataa na kumdhuru Saleh kwa maneno na matendo.
"Wakasema: Ewe Saleh! Hakika kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa kheri kwetu. Je, unatukataza tusiwaabudu waliyo kuwa wakiwaabudu baba zetu? Na hakika sisi tuna shaka na wasiwasi kwa hayo unayo tuitia.” (Kurani 11:62)
Watu wa Thamud wakakusanyika mahali pao pa mikutano, chini ya kivuli cha mlima mkubwa. Walidai kwamba Saleh athibitishe kuwa Mungu Mmoja anayemzungumzia ni mwenye nguvu na uwezo. Walimwambia afanye muujiza - asababishe ngamia wa kipekee na asiye na mfano kujitokeza kutoka milima iliyo karibu. Saleh aliwauliza watu wake, iwapo ngamia angetokea wangeamini ujumbe wake. Wote walijibu ndiyo, na watu waliomba pamoja na Saleh ili muujiza utokee.
Kwa uwezo wa Mungu, ngamia mkubwa, mjamzito wa miezi kumi aliibuka kutoka kwenye miamba chini ya mlima. Baadhi ya watu walielewa ukubwa wa muujiza huo, lakini wengi waliendelea kukufuru. Waliona alama kubwa na yenye kushangaza mbele yao lakini bado walibaki na kiburi na ukaidi.
“Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. ” (Kurani 17:59)
Mchambuzi wa Qurani na mwanazuoni wa Kiislamu Ibn Kathir anatujulisha kwamba kuna hadithi kadhaa za ngamia jike na asili yake ya kimiujiza. Inasemekana kwamba ngamia yule alionekana akitoka kwenye mwamba uliogawanyika wazi, na baadhi ya watu walisimulia kuwa ngamia alikuwa mkubwa sana hadi alikuwa na uwezo wa kunywa maji yote katika visima vya mji kwa siku moja. Watu wengine walisema ngamia yule aliweza kila siku kutoa maziwa ya kutosha wakazi wote. Ngamia aliishi miongoni mwa watu wa Thamud, na kwa bahati mbaya, makafiri waliomdhulumu Saleh wakageuza hasira yao na chuki kuelekea kwa huyo ngamia.
Ingawa watu wengi walimwamini Mungu, wakamsikiliza Mtume Saleh, na kuelewa muujiza wangamia jike, wengine wengi walikataa kusikiliza. Watu walianza kulalamika kwamba ngamia alikunywa maji mengi, au kwamba aliogofya mifugo wao. Nabii Saleh alianza kuogopa kuhusu usalama wa ngamia. Akawaonya watu wake kuhusu adhabu kubwa itakayowapata ikiwa watamdhuru ngamia huyo.
“Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ni Ishara kwenu. Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya, isije ikakuangamizeni adhabu iliyo karibu.” (Kurani 11:64)
Kundi la wanaume liliwahimiza wake zao, wakapanga njama ya kumwua huyo ngamia jike na kuchukua nafasi ya kwanza kumpiga na mshale na kumchoma kwa upanga. Ndipo ngamia akaanguka chini na kufa. Wauaji wakashangilia na wakapongezana. Na makafiri wakamcheka na kumdhihaki Saleh. Nabii Saleh aliwaonya watu kuwa adhabu kubwa ingewapata kwa ndani ya siku tatu, lakini aliendelea kuwa na matumaini kwamba wangetambua kosa lao na kumwomba Mungu msamaha. Nabii Saleh alisema: "Enyi watu wangu! Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi hamwapendi wenye nasaha.” (Kurani 7:79) Hata hivyo, watu wa Thamud walimdhihaki Saleh na walipanga kumwangamiza yeye na familia yake kama walivyomuua ngamia jike wake.
“Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha.Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia usiku yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamizo ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli..’” (Kurani 27: 48 & 49)
Mwenyezi Mungu alimwokoa Nabii Saleh na wafuasi wake wote; walikusanya virago vyao vidogo, na kwa nyoyo nzito, wakaelekea mahali pengine. Baada ya siku tatu, onyo la Mtume Saleh likatokea. Anga ilijaa umeme na radi na ardhi ikatetemeka kwa ukali. Mwenyezi Mungu aliuangamiza mji wa Thamud, na watu wake wakafa kwa adhabu ya khofu na kufuru.
Ibn Kathir alisema kuwa watu wa Saleh walianguka wafu, wote kwa wakati mmoja. Kiburi na ukafiri wao haukuweza kuwaokoa, wala sanamu zao kuwasaidia. Majengo yao makubwa na ya kuvutia hayakuwapa ulinzi wowote. Na Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaletea watu uwongofu ulio wazi, lakini makafiri wanajivuna na kukataa. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kurehemu, Mwenye kusamehe: Anapenda kusamehe. Hata hivyo, maonyo ya Mungu hayapaswi kupuuzwa. Adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama walivyoipata watu wa Thamud, inaweza kuwa wa haraka sana na wenye ukali.
Ongeza maoni