Yesu, mwana wa Maryamu (sehemu ya 3 kati ya 5): Wanafunzi wake
Maelezo: Muujiza mwingine wa Yesu unaelezwa. Umuhimu halisi wa muujiza wa meza, kuenea kwa vyakula.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,660 (wastani wa kila siku: 5)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Sura ya 5 ya Kurani inaitwa Al Maidah (au Meza Iliyoandaliwa Chakula). Ni moja ya sura tatu katika Kurani zinazozungumzia kwa mapana maisha ya Yesu na mama yake Maryamu. Sura nyingine ni sura ya 3 Al Imran (familia ya Imran) na sura ya 19, Maryam (Maryamu). Waislamu wanampenda Yesu, na wanamheshimu Mama yake, lakini hawawaabudu. Kurani, ambayo Waislamu wanaamini kuwa ni maneno ya moja kwa moja ya Mwenyezi Mungu, inawaheshimu sana Yesu na Mama yake Maryamu, na kwa hakika familia yao yote - familia ya Imran.
Tunajua kwamba Yesu aliishi miongoni mwa watu wake Waisraeli kwa miaka mingi, akiwaita warudi kwenye ibada ya Mungu Mmoja wa Kweli, pamoja na kufanya miujiza kwa idhini ya Mungu. Wengi wa wale waliokuwa karibu naye walikataa wito wake na kushindwa kutii ujumbe wake. Hata hivyo, Yesu alikusanya karibu naye kundi la masahaba walioitwa Al Hawariyeen (wanafunzi wa Isa) kwa Kiarabu.
Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani:
“Na nilipowafunulia Al-Hawariyeen (Wanafunzi) kwamba waniamini Mimi na Mtume wangu, wakasema: ‘Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.’” (Kurani 5:111)
Wanafunzi walijiita Waislamu; hii ingewezekanaje wakati dini ya Uislamu isingefunuliwa kwa miaka 600 mingine? Mungu lazima anarejelea maana ya jumla ya “Muislamu”. Muislamu ni mtu yeyote anayejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu Mmoja na utiifu Wake, na yeyote ambaye utiifu wake na uaminifu wake ni kwa Mwenyezi Mungu na Waumini kuliko kitu kingine chochote. Maneno Muislamu na Uislamu yanatokana na mzizi mmoja wa Kiarabu - sa la ma - na hiyo ni kwa sababu amani na usalama (Salam) asili yake ni kunyenyekea kwa Mungu. Kwa hivyo inaweza kueleweka kwamba Mitume wote wa Mungu na wafuasi wao walikuwa Waislamu.
Meza Iliyoandaliwa Chakula
Wanafunzi wa Yesu wakamwambia:
“Ewe Isa mwana wa Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni?” (Kurani 5:112)
Je, walikuwa wakimwomba Yesu afanye muujiza? Je, wanafunzi wa Yesu waliojiita Waislamu walihisi kutokuwa na hakika kuhusu uwezo wa Mungu wa kufanya miujiza apendavyo? Haiwezekani, kwani hiki kitakuwa ni kitendo cha kutoamini. Wanafunzi wa Yesu hawakuwa wakiuliza kama ingewezekana, bali iwapo Yesu angemwomba Mungu wakati huo mahususi awape chakula. Hata hivyo, huenda Yesu alifikiri tofauti, kwa kuwa alijibu:
“...Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.” (Kurani 5:112)
Walipoona jinsi Yesu alivyoitikia, wanafunzi wake walijaribu kueleza maneno yao. Hapo awali walisema: "Tunataka kukila chakula hicho kutoka kwenye (hiyo meza)."
Huenda walikuwa na njaa sana na walitaka Mungu atimize mahitaji yao. Kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie riziki kunakubalika, kwani Mwenyezi Mungu ndiye mpaji, Ambaye riziki zote hutoka kwake. Wanafunzi wakaendelea kusema, “na nyoyo zetu zitue (ziridhike).”
Walimaanisha kwamba imani yao ingeimarika zaidi iwapo wangeona muujiza kwa macho yao wenyewe, na hilo linathibitishwa na kauli yao ya mwisho. "Na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia (ni mashahidi wa kuteremshwa hiyo meza iliyojaa vyakula)."
Ijapokuwa ilitajwa mwisho, kuwa shahidi wa kweli ilivyo na kuona miujiza ambayo ni uthibitisho muhimu zaidi wa ombi lao. Wanafunzi walikuwa wakimuomba Mtume Yesu afanye muujiza huo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ili wawe mashahidi mbele ya wanadamu wote. Wanafunzi hao walitaka kueneza ujumbe wa Yesu kwa kutangaza miujiza waliyoshuhudia kwa macho yao wenyewe.
“Wakasema: ‘Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia.’ Akasema Isa mwana wa Maryamu: ‘Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mlezi! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanaoruzuku.’” (Kurani 5:113-114)
Yesu aliomba muujiza huo. Alisali kwa Mungu, akiomba kwamba meza iliyokuwa na vyakula iteremshwe. Yesu pia aliomba kwamba hii iwe kwa ajili yao wote na kwamba iwe sikukuu. Neno la Kiarabu linalotumiwa na Kurani ni Idi, likimaanisha sherehe inayotokea au kurudi tena. Yesu alitaka wanafunzi wake na wale waliokuja baada yao wakumbuke baraka za Mungu na kushukuru.
Tuna mengi ya kujifunza kutokana na dua zilizoombwa na Mitume na waumini wengine wema. Dua ya Yesu haikuwa tu kwa ajili ya meza iliyotandazwa vyakula, bali kwa Mungu kuwapa riziki. Ameifanya dua hiyo kuwa jumuifu kwa sababu chakula ni sehemu ndogo tu ya riziki inayotolewa na Mbora wa Wanaoruzuku. Riziki kutoka kwa Mungu inajumuisha mahitaji yote muhimu kwa maisha yakiwemo, lakini sio tu, chakula, makao, na ujuzi. Mungu akajibu:
“...Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakayekana baadaye, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu.” (Kurani 5:115)
Ujuzi ni Sawa na Uwajibikaji
Sababu kwa nini jibu la Mungu lilikuwa limetoa uamuzi wa mwisho ni kwamba ikiwa mtu atakufuru baada ya kuonyeshwa ishara au muujiza kutoka kwa Mungu, ni mbaya zaidi kuliko kukufuru bila kuona muujiza. Unaweza kujiuliza ni kwa nini. Ni kwa sababu pindi mtu anapoona muujiza, anakuwa na ujuzi na ufahamu wa kuwa Mungu ni muweza wa yote. Kadiri mtu anavyokuwa na ujuzi mwingi, ndivyo anavyokuwa na uwajibikaji zaidi mbele ya Mungu. Unapoziona ishara, wajibu wa kuamini na kueneza ujumbe wa Mungu unakuwa mkubwa zaidi. Mungu aliwaamuru wanafunzi wa Yesu watakapoikea meza hiyo iliyotandazwa vyakula waweze kutambua wajibu mkubwa ambao walikuwa wamejitwika wenyewe.
Siku ya meza ikawa siku ya karamu na sherehe kwa wanafunzi na wafuasi wa Yesu, lakini, kadiri muda ulivyopita, maana halisi na kiini cha muujiza huo ilipotea. Hatimaye Yesu alikuja kuabudiwa kama mungu. Siku ya Ufufuo, wakati wanadamu wote watasimama mbele ya Mungu, wanafunzi wale watabeba daraka kubwa la kujua ujumbe wa kweli wa Yesu. Mungu atazungumza na Yesu moja kwa moja akisema:
“...Ewe Isa mwana wa Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu?’ (Na Isa) atasema: ‘Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyofichikana. Sikuwaambia lolote ila uliyoniamrisha, nayo ni: Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi...’” (Kurani 5:116-117)
Sisi ambao tumebarikiwa na ujumbe huu wa kweli wa Yesu, ujumbe uleule ulioenezwa na Mitume wote akiwemo mtume wa mwisho, Muhammad, pia tutabeba jukumu kubwa Siku ya Kiyama.
Ongeza maoni