Yesu, mwana wa Maryamu (sehemu ya 2 kati ya 5): Ujumbe wa Yesu
Maelezo: Hali halisi ya Yesu na ujumbe wake katika Kurani, na umuhimu wa Bibilia leo kuhusiana na imani za Waislamu.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,601 (wastani wa kila siku: 4)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Tumeshathibitisha ya kwamba Yesu mwana wa Maryamu, au kama anavyoitwa na Waislamu, Isa ibn Maryam, alifanya muujiza wake wa kwanza akiwa amebebwa mikononi mwa Maryamu. Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu alisema, na maneno yake ya kwanza yalikuwa “Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu,” (Kurani 19:30). Hakusema “Mimi ni Mungu” au hata “Mimi ni mwana wa Mungu”. Maneno yake ya kwanza yaliweka msingi wa ujumbe wake, na utume wake ulikuwa: kuwaita watu warudi, kwenye ibada halisi ya Mungu Mmoja.
Wakati wa Yesu, dhana ya Mungu Mmoja haikuwa jipya kwa Wana wa Israeli. Taurati ilikuwa imetangaza “Sikia, Ee Israeli, Bwana Mungu wako ndiye Mmoja,” (Kumbukumbu la Torati 6:4). Hata hivyo, mafunuo ya Mungu ilitafsiriwa vibaya na kutumiwa vibaya, na nyoyo zikawa ngumu. Yesu alikuja kuwakana hadharani viongozi wa Wana wa Israili, ambao walijiingiza katika maisha ya kupenda mali na anasa, na kuitetea sheria ya Musa iliyopatikana ndani ya Taurati ambayo hata wao waliibadilisha.
Utume wa Yesu ulikuwa ni kuithibitisha Taurati, kuhalalisha mambo ambayo hapo awali yalikuwa haramu na kutangaza na kuthibitisha tena imani katika Muumba Mmoja. Mtume Muhammad amesema:
“Kila Mtume alitumwa kwa umma wake peke yake, lakini mimi nilitumwa kwa watu wote,” (Saheeh Bukhari).
Kwa hivyo, Yesu alitumwa kwa Waisraeli.
Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani kwamba atamfundisha Yesu Taurati, Injili na Hekima.
“Na atamfunza kuandika na Hekima na Taurati na Injili.” (Kurani 3:48)
Ili kueneza ujumbe wake kwa ufanisi, Yesu aliielewa Taurati, na alipewa ufunuo wake mwenyewe kutoka kwa Mwenyezi Mungu - nayo ni Injili. Pia, Mungu alijaalia Yesu uwezo wa kuwaongoza na kuwashawishi watu wake kupitia ishara na miujiza.
Mwenyezi Mungu huwapa nguvu Mitume Wake wote kupitia miujiza inayoonekana na yenye maana kwa watu ambao Mtume huyo alitumwa kuwaongoza. Wakati wa Yesu, Waisraeli walikuwa na ujuzi mwingi katika uwanja wa tiba. Kwa hiyo, miujiza aliyoifanya Yesu (kwa idhini ya Mungu) ilikuwa ya namna hii na ilijumuisha kurudisha kuona kwa vipofu, kuponya wenye ukoma na kufufua wafu. Mungu anasema:
“...na ulipowaponyesha vipofu na wakoma kwa idhini Yangu; na ulipowafufua wafu kwa idhini Yangu...” (Kurani 5:110)
Mtoto Yesu
Si Kurani wala Biblia inayorejelea ujana wa Isa. Tunaweza kukisia, hata hivyo, kwamba kama mtoto wa kiume katika familia ya Imran, yeye alikuwa mtoto mcha Mungu aliyejitolea kujifunza na mwenye shauku ya kuwashawishi watoto na watu wazima waliomzunguka. Baada ya kumtaja Yesu akizungumza angali mtoto mchanga wa kubebwa, Kurani mara moja inasimulia kisa cha Yesu akifinyanga umbo la ndege kutoka kwenye udongo. Akapuliza ndani yake na kwa idhini ya Mungu ukawa ndege.
“...nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu...” (Kurani 3:49)
Injili ya Utotoni ya Thomas, mojawapo ya seti ya maandishi yaliyoandikwa na Wakristo wa mwanzo lakini haikukubaliwa kuingizwa katika kanuni au mafundisho ya Agano la Kale, pia inarejelea hadithi hii. Inasimulia kwa undani hadithi ya Yesu angali mdogo akitengeneza ndege kutoka kwa udongo na kupuliza uhai ndani yao. Ingawa inavutia, Waislamu wanaamini ujumbe wa Yesu iwapo tu unasimuliwa katika Kurani na simulizi za Mtume Muhammad.
Waislamu wanatakiwa kuamini vitabu vyote vilivyoteremshwa na Mungu kwa wanadamu. Walakini, Biblia, kama ilivyo leo, sio Injili ambayo ilifunuliwa kwa Mtume Yesu. Maneno na hekima ya Mungu aliyopewa Yesu yamepotea, yamefichwa, yamebadilishwa na kupotoshwa. Hatima ya maandishi ya Apokrifa (Yasiyothibitishwa au Yaliyobuniwa) ambayo Injili ya Utotoni ya Thomas ni ushuhuda wa hili. Mnamo 325BK, Mfalme Konstantino alijaribu kuunganisha Kanisa la Kikristo lililovunjika kwa kuitisha mkutano wa Maaskofu kutoka kote ulimwenguni kunapojulikana. Mkutano huu ulijulikana kama Baraza la Naisia, na waliwakifia fundisho la imani ya Utatu, ambalo hapo awali halikuwepo, na kuchangia kupotea kati ya injili 270 na 4000. Baraza hilo liliamuru kuchomwa moto injili zote ambazo hazikustahiki kuingizwa katika Biblia mpya, na Injili ya Utotoni ya Thomas ilikuwa ni mojawapo yazo.[1] Hata hivyo, nakala za Injili nyingi zilisalimika, na, ingawa hazimo katika Biblia, zinathaminiwa kwa umuhimu wao wa kihistoria.
Kurani Inatukomboa
Waislamu wanaamini kwamba Yesu kwa hakika alipokea ufunuo kutoka kwa Mungu, lakini hakuandika neno hata moja, wala hakuwaagiza wanafunzi wake kuliandika.[2] Hakuna haja ya Muislamu kujaribu kuthibitisha au kukanusha vitabu vya Wakristo. Kurani hutuondolea haja ya kujua kama Biblia tuliyo nayo leo ina neno la Mungu, au maneno ya Yesu. Mungu anasema:
“Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili.” (Kurani 3:3)
Na pia:
“Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu...” (Kurani 5:48)
Chochote chenye manufaa kwa Waislamu kukijua kutoka katika Taurati au Injili kimeelezwa kwa uwazi ndani ya Kurani. Jema lolote ambalo linaweza kupatikana katika vitabu vilivyotangulia linapatikana sasa ndani ya Kurani.[3] Ikiwa maneno ya Agano Jipya ya leo yanakubaliana na maneno ya Kurani, basi maneno haya huenda yanaunda sehemu ya ujumbe wa Yesu ambao haukupotoshwa au kupotea kwa kupita muda. Ujumbe wa Yesu ulikuwa ni ujumbe uleule ambao Mitume wote wa Mungu walifundisha watu wao. Mola wenu Mlezi, Mungu wenu, ni Mmoja, basi muabuduni Yeye peke yake. Na Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani kuhusu kisa cha Yesu:
“Hakika haya ndiyo maelezo ya kweli. Na hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu tu, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hekima.” (Kurani 3:62)
Ongeza maoni