Wageni ni kina nani?
Maelezo: Sisi si Waislamu wa kwanza au wa pekee kutafakari kuhusu ugeni wetu.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 10 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 2,865 (wastani wa kila siku: 3)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Nabii Muhammad alisema: “Uislamu ulianza kama kitu kigeni, na utarejea kuwa kitu kigeni, basi wabashirieni wageni.“[1] Akaulizwa: Wageni ni kina nani, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: “Wale wanaowarekebisha watu watakapo kuwa wafisadi. “[2] Masimulizi mengine yanasema, “Wale wanaorekebisha mafundisho yangu yaliyoharibiwa na watu waliokuja baada yangu.” Katika masimulizi mengine alisema kuhusu swali lile, “Wao ni kundi ndogo la watu kati ya idadi kubwa ya watu wabaya. Na wanaowapinga ni zaidi ya wale wanaowafuata.“[3]
Wageni ni kina nani haswa? Je! Ni mimi au nyinyi au jirani; Ni watu wa Msikiti huu au Msikiti mwingine? Ni sisi sote au hakuna hata mmoja wetu? Ni wale walioingia katika Uislamu? Au ni Muislamu aliyezaliwa kwa Uislamu ambaye ghafla anaanza kuwacha ndevu, au anavaa hijab kwa mara ya kwanza? Nadhani wengi wenu wangekubaliana kuwa mtu kuwa Muislamu katika karne ya 21 inamfanya ajue vizuri ugeni ni nini. Huenda hata ikawa ni mfano wa bahati, yaani umechaguliwa kibahati.
Hata hivyo, Waislamu wengi wapya watakuambia kuhusu hisia ya kuhisi kana kwamba walikuwa wageni, kabla ya kupata Uislamu. Watazungumzia vile walihisi kwamba walikuwa ni wa sehemu nyingine, kwamba maisha yao yalikuwa yakienda kombo kwa kiasi fulani. Mara nyingi huzungumzia kuhusu hisia isiyoeleweka ya kujua kuwa hawakuwa kama watu wengine waliowazunguka, wakihisi kama mgeni katika nchi ya kigeni. Kusilimu kunaleta hisia ya kurudi nyumbani, ya kuwa mtu wa kawaida sasa, ingawa wakati mwingine bado upo ugenini.
Haitachukua muda mrefu hata hivyo kabla ya Waislamu wengi wapya kuanza kujisikia kuwa bado ni wageni na wanaanza kujiuliza kama hisia hii ya kutotulia kamwe, au kuhisi upo nyumbani, itaisha. Wengine hujiambia kuwa hawatahisi hivyo mpaka watakapokuwa katika nyumba yao ya kweli, Al Jenna, Peponi. Hisia hii si kwa Waislamu wapya tu; mara nyingi wale waliozaliwa katika dini ya Uislamu wanahisi hisia ya kutokuwa nyumbani, ya kuwa mgeni, ya kutokufaa, ya kuwa mtu wa nje.
Sisi si Waislamu wa kwanza au wa pekee kutafakari kuhusu ugeni wetu. Waislamu wa kwanza huko Makka lazima waliwatazama dada zao, baba zao na shangazi zao na kujiuliza kwa nini hawakuweza kuona ukweli. Kwa nini hawakuona kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu? Kupata na kukubali ukweli ni mafanikio ya kipekee lakini mara nyingi hisia ya ugeni hubaki. Na hilo si jambo baya.
Mwanazuoni maarufu wa Kiislamu Ibnul Qayyim alisema, Waislamu ni wageni miongoni mwa wanadamu; waumini wa kweli ni wageni miongoni mwa Waislamu; na wasomi ni wageni miongoni mwa waumini wa kweli. Na wafuasi wa Sunnah, wale wanaoacha aina zote za uvumbuzi, pia ni wageni.
Ugeni tunaohisi ni hisia iliyobebwa na manabii na mitume kabla ya Mtume Muhammad, rehma ziwe juu yao. Nabii Nuhu alihubiri neno la Mungu kwa watu wake kwa miaka 950 lakini alikataliwa na kufanyiwa dhihaka. Nabii Lutu, Nabii Ibrahim na Nabii Yona, waliteswa na kudhalilishwa. Nabii Musa hakukataliwa na Farao tu bali pia na watu wake walipokataa wito wake na kuabudu ndama ya dhahabu badala ya Mungu Mmoja. Nabii Yesu na wanafunzi wake walikejeliwa walipochagua kumwabudu Mungu peke yake na hakika wamehisi ugeni ambao tunahisi leo.
Imam Ibnul Qayyim alipendekeza kuwa kuna na viwango vitatu vya ugeni.[4] Cha kwanza alikiita 'Ugeni wa kusifiwa ', ambacho ni matokeo ya kushikamana na imani katika Mungu Mmoja. Ni ugeni wa wanaosema Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu, na Muhammad ni Mtume wake. Huu ni ugeni unaoridhisha, unaotokana na kujua kwamba hakuna msaada ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anasema kwamba watu wengi hawatafuata Haki. Hakika wanaomuabudu Mwenyezi Mungu kwa yakini na kwa usahihi, hao ndio wageni miongoni mwa wanaadamu.
Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Mwenyezi Mungu. (Quran 6: 116)
Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi. (Quran 12: 103)
Na hakika wengi wa watu ni wapotofu. (Quran 5: 49)
lakini watu wengi hawashukuru. (Quran 12: 38)
Kwa upande wa aina ya pili ya ugeni, 'ugeni wa kulaumiwa ', Ibnul Qayyim alisema zaidi ya miaka 600 iliyopita, maneno ambayo yanafaa hata leo. “Ugeni wao ni kutokana na kukataa kwao kufuata Njia ya Mwenyezi Mungu iliyo sawa na Iliyo Nyooka. Ugeni huu ni ugeni wa kutokubaliana na dini ya Uislamu na, kwa hivyo, utabaki ugeni hata kama wafuasi wake ni wengi, nguvu zake ni imara na kuwepo kwake kunaenea. Hao ndio wageni kwa Mwenyezi Mungu. Mungu atuzuie tusiwe mmoja wao.”
Aina ya tatu ni ugeni ambao msafiri anahisi. Haustahili kusifiwa wala hauna lawama. Hata hivyo unaweza kuwa na uwezo wa kustahili kusifiwa. Wakati mtu anapoishi mahali kwa muda mfupi, akijua kwamba anahitaji kuhama anahisi ugeni, kana kwamba yeye si wa pahali popote.
Sisi sote ni wageni katika dunia. Na sisi sote tutaingia katika makao yetu ya kudumu katika Akhera. Kuelewa hii ina maana kwamba tunaelewa na kufuata kile Ibnul Qayyim alichokiita ugeni wa kusifiwa.
Nabii Muhammad alisema, “ Ishi katika dunia kama mgeni au msafiri.“ Hisia ya Ugeni unaosikika na Waislamu wengi kwa kawaida ni jambo jema. Inaweza kuwa ugeni unaostahili sifa ambao unathibitisha upendo wetu kwa Mungu na Mtume wake. Inatukumbusha tuishi maisha yetu kana kwamba sisi ni wasafiri katika njia inayoisha, tukimngoja Mungu atuite nyumbani kwa makao yetu ya milele.
Ongeza maoni