Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 1 kati ya 8): Utangulizi
Maelezo: Utangulizi wa dhana ya kuwepo maisha baada ya kifo katika Uislamu, na jinsi inavyofanya maisha yetu kuwa na maana; kwa kusudi.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 12 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 13 Mar 2023
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 6,726
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Utangulizi
Muhammad, Mtume wa Uislamu aliyefariki mwaka 632, alisimulia:
"Jibril alikuja kwangu na kuniambia, ‘Ewe Muhammad, ishi upendavyo, kwani mwishowe utakufa. Mpende unayemtaka, kwani hatimaye utaondoka. Fanya upendavyo, kwani utalipwa. Jua kuwa sala ya usiku[1]ni heshima ya Muumini, na fahari yake ni kuwa huru bila kuwategemea wengine.’" (Silsilah al-Saheehah)
Kuna jambo moja tu la uhakika kuhusu maisha, nalo ni kuwa yana mwisho. Kauli hii ya ukweli huzua swali la kiada ambalo huwashughulisha watu wengi angalau mara moja katika umri wao: Kuna nini kinaendelea baada ya kifo?
Katika kiwango cha fiziolojia (sayansi ya mwili wa viumbe unavyofanya kazi), safari ambayo marehemu hupitia hushuhudia waziwazi na wote. Sehemu za mwili kitabia zikiachwa zijiendeshe peke yake,[2] moyo utaacha kupiga, mapafu yataacha kupumua, na seli za mwili zitakuwa na njaa ya damu na oksijeni. Kukomesha mtiririko wa damu kupitia seli hizo na kusambaa mwili mzima hivi karibuni huzifanya kupauka rangi. Oksijeni ikiwa imekatwa, seli zitapumua kama anerobi (viumbe vyenye kuishi bila oksijeni) kwa muda, na kutoa asidi ya maziwa yaliyochachuka inayosababisha ukakamaaji wa misuli - kukausha misuli ya maiti. Kisha, seli zinapoanza kuoza, ukakamavu hupungua, ulimi hujitokeza nje, halijoto huteremka, ngozi hubadilika rangi, nyama huoza, na vimelea huwa na karamu yao - mpaka kinachobaki ni jino na mifupa iliyokauka.
Kuhusu safari ya roho baada ya kufa, basi hili si jambo linaloweza kushuhudiwa, wala haliwezi kupimwa kwa uchunguzi wa kisayansi. Hata katika mwili ulio hai, fahamu, au roho, ya mtu haiwezi kufanyiwa majaribio ya kiuchunguzi. Ni nje ya udhibiti wa binadamu. Kuhusu hili, dhana ya Akhera - maisha baada ya kifo, ufufuo, na Siku ya Hesabu; bila kusahau kutaja uwepo wa Mwenyezi Mungu, Muumba Muweza wa yote, malaika Wake, majaaliwa, na kadhalika - huwekwa chini ya mada ya imani ya mambo ya ghaibu. Njia pekee ambayo mwanadamu anaweza kujua lolote la ulimwengu usioonekana ni kupitia wahyi wa kiungu.
"Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha." (Kurani 6:59)
Ingawa yale yaliyotufikia kutoka Taurati, Zaburi, Injili - maandiko yaliyoteremshwa kwa mitume wa mwanzo - yote yanazungumzia Akhera, ni kupitia Wahyi wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu, Kurani Tukufu, kama ilivyoteremshwa kwa Mtume Wake wa Mwisho, Muhammad, kwamba tunajifunza mambo zaidi kuhusu maisha ya baada ya kifo. Na kama vile Kurani ilivyo, na itabakia daima, imehifadhiwa na bila kuvurugwa na mikono ya wanadamu, ubainifu unaotupa katika ulimwengu wa ghaibu, kwa Muumini, ni ukweli, halisi na uhakika kama vile kitu chochote kinachoweza kufunzwa kupitia jitihada yoyote ya kisayansi (na bila athari yoyote katika matokeo!).
"…Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha kwa Mola wao Mlezi watakusanywa." (Kurani 6:38)
Sambamba na swali la kile kinachotokea baada ya kufa, ni swali jingine: Kwa nini tuko hapa? Kwani ikiwa kwa hakika hakuna kusudi kubwa zaidi la kuishi (yaani, kubwa zaidi ya kuishi maisha yenyewe), swali la kile kinachotokea baada ya kifo huwa la kitaaluma, ama lisiwe na maana yoyote. Ni kama tu mtu akikubali kwanza kuwa usanifu wetu wa akili, uumbaji wetu, unahitaji yule mwenye akili na ruwaza zaidi nyuma yake, na ni Muumba ambaye atatuhukumu kwa yale tunayofanya katika uhai huu wa duniani, ndipo maisha huwa na maana muhimu.
"Je, mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa Arshi Tukufu." (Kurani 23:115-116)
Ikiwa sivyo, mtu mwenye utambuzi atalazimika kukata kauli kwamba maisha duniani yamejaa ukosefu wa haki, ukatili na uonevu; kwamba sheria ya msituni, kuishi kwa walio na nguvu zaidi, ndio muhimu zaidi; kwamba ikiwa mtu hawezi kupata furaha katika maisha haya, iwe ni kutokana na kutokuwepo vitu vya kupumbaza, mapenzi ya kimwili, au kufurahia starehe nyingine, basi maisha hayo mtu hafai kuyaishi. Kwa hakika, mtu hukata tamaa na maisha ya hapa duniani akiwa na imani ndogo, au hana imani kabisa, au ana imani isiyo kamilifu kuhusu maisha ya baada ya kifo, ndipo anaweza kujiua. Baada ya yote, ni nini kingine kinachofanya wasio na furaha, wasiopendwa na wasiohitajika; waliovunjika moyo (waliokata tamaa), wenye kuhuzunika na waliokosa matumaini, kupoteza wakikosa budi?![3]
"Akasema: Na nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale waliopotea?" (Kurani 15:56)
Kwa hivyo, je, twaweza kukubali ya kwamba kifo chetu kinategemea kusitishwa tu kifiziolojia, au kuwa uhai ni tokeo tu la nadharia ya mageuko ya upofu na ya kibinafsi? Hakika, kuna mambo zaidi tusiyoyajua kuhusu kifo, na vivyo hivyo uhai, kuliko hili.
Rejeleo la maelezo:
[1] Hii ni sala (salati)ambayo ni ya hiari na inasaliwa usiku baada ya sala ya mwisho (isha) na kabla ya kwanza (fajr), ambazo ni miongoni mwa sala tano rasmi za kila siku. Wakati mzuri wa kusali sala ya tahajjud ni katika theluthi ya mwisho ya usiku.
[2]Ingawa moyo unaweza kudumishwa kuendelea kupiga kupitia mashine, na damu kusukumwa kwa msaada wa mashine, iwapo ubongo umekufa, ndivyo kiumbe kwa ujumla.
[3]Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa inayoadhimisha 'Siku ya Kuzuia Kujiua Ulimwenguni', "Watu wengi hujiua kila mwaka kuliko wanaokufa kutokana na vita na mauaji kwa pamoja ... Kati ya milioni 20 hadi 60 hujaribu kujiua kila mwaka, lakini karibu milioni moja tu ya watu wanaojiua. hufanikiwa." (Reuters, Septemba 8, 2006)
Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 2 kati ya 8): Muumini ndani ya Kaburi
Maelezo: Maelezo ya maisha ndani ya kaburi kuanzia kifo hadi Siku ya Hukumu kwa waumini waaminifu.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 12 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,905
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Ulimwengu wa Kaburini
Sasa tutaangalia kwa ufupi safari ya roho baada ya kifo. Kwa kweli hii ni hadithi ya kushangaza, hususan kwa sababu ni ya kweli na ambayo sote lazima tutaipitia. Elimu tuliyonayo kuhusu safari hii, usahihi wake na undani wake, ni dalili ya wazi kwamba Muhammad alikuwa kweli Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Wahyi alioupokea kisha akatufikishia kutoka kwa Mola Wake Mlezi hauna utata katika maelezo yake ya maisha ya Akhera kwa sababu ni pana. Unapoitazama elimu hii kijuujuu utaanza na ugunduzi mfupi wa safari ya roho ya muumini kutoka muda wa kifo hadi mahali pake pa kupumzika Peponi.
Muumini anapokaribia kuondoka duniani, malaika wenye nyuso nyeupe hushuka kutoka mbinguni na kusema:
"Ewe nafsi iliyotulia, toka mwilini upate msamaha wa Mwenyezi Mungu na radhi zake." (Hakim na wengine)
Muumini atatarajia kukutana na Muumba wake, kama alivyoeleza Mtume, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu zimshukie:
"…wakati wa kifo cha Muumini unapokaribia, anapokea habari njema ya radhi za Mungu pamoja na baraka Zake juu yake, na hivyo wakati huo hakuna kitu chenye thamani zaidi kwake kuliko kile kilicho mbele yake. Kwa hivyo anapenda kukutana na Mungu, na Mungu anapenda kukutana naye." (Saheeh Al-Bukhari)
Roho hutoka mwilini kwa amani kama tone la maji litokalo kwenye kiriba, na malaika huishikilia:
Malaika huitoa kwa upole, wakiwaambia:
"…Msiogope wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinachotamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyovitaka. Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." (Kurani 41:30-32)
Mara baada ya kutolewa kutoka kwenye mwili, malaika huifunika roho katika sanda yenye harufu ya miski na kupaa nayo juu mbinguni. Malango ya Mbinguni yanapofunguka kwa ajili ya roho hiyo, malaika huisalimu:
"Roho njema imekuja kutoka duniani, Mungu akubariki na mwili uliokuwa ukiishi ndani yake."
…itatambulishwa kwa majina bora ambayo iliitwa nayo katika maisha haya ya duniani. Mungu anaamuru "kitabu" chake kirekodiwe, na roho inarudishwa tena duniani.
Roho itabakia kuzimuni ndani ya kaburi lake, iitwayo Barzakhi, ikingojea Siku ya Hukumu. Malaika wawili wa kutisha, wanaoitwa Munkar na Nakir huitembelea roho ili kuiuliza kuhusu dini yake, Mungu, na mtume. Roho ya muumini hukaa wima katika kaburi lake huku Mwenyezi Mungu akiipa nguvu ya kuwajibu malaika hao kwa imani kamili na yakini.[1]
Munkar na Nakir: "Dini yako ni ipi?"
Roho ya Muumini: "Uislamu."
Munkar na Nakir: "Nani Mola wako?"
Roho ya Muumini: "Allah."
Munkar na Nakir: "Nani Mtume wako?" (au "Unasemaje kuhusu mwanamume huyu?")
Roho ya Muumini: "Muhammad."
Munkar na Nakir: "Ulijuaje mambo haya?"
Roho ya Muumini: "Nilisoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu (yaani Kurani) na nikaamini."
Na roho ikishapita mtihani, sauti kutoka mbinguni itaita:
"Mja wangu amesema kweli, mpeni vyombo vya Peponi, mvisheni mavazi ya Peponi, na mfungulieni lango moja la Peponi."
Kaburi la muumini hupanuliwa nafasi na kufanywa pana na kujazwa nuru. Huonyeshwa yale yangekuwa makazi yake katika Jehanamu – lau angekuwa mwovu mtenda dhambi – hayo yatatendeka kabla ya mlango kufunguliwa kwa ajili yake kila asubuhi na jioni ukimuonyesha makazi yake halisi Peponi. Kwa msisimko na matarajio ya furaha, muumini ataendelea kuuliza: ‘Saa (ya Ufufuo) itakuja lini?! Lini Saa itafika?!’ mpaka aambiwe atulie.[2]
Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 3 kati ya 8): Muumini wakati wa Siku ya Hukumu
Maelezo: Jinsi waumini watakuwa Siku ya Hesabu, na baadhi ya sifa za waumini zitakazowarahisishia kupita kwenye milango ya Peponi.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 12 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,126
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Siku ya Hukumu
"Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, na mamaye na babaye, na mkewe na wanawe. Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha." (Kurani 80:34-37)
Saa ya Ufufuo itakuwa tukio la kutisha na kubwa. Hata hivyo, pamoja na dhiki zake, Muumini atakuwa na furaha, kama Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alivyosimuliwa kutoka kwa Mola wake Mlezi:
Mwenyezi Mungu anasema, "Kwa Ezi Yangu na Jalali Yangu (Utukufu Wangu), Sitampa mja Wangu dhamana mbili na vitisho viwili. Akijihisi salama kutoka Kwangu akiwa duniani[1], nitamtia hofu Siku nitakapowakusanya waja Wangu; na akiniogopa akiwa duniani, nitamweka salama Siku nitakapowakusanya waja Wangu."[2]
"Jueni kuwa vipenzi vya Mwenyezi Mungu hawatakuwa na khofu wala hawatahuzunika. Hao ni ambao wameamini na wakawa wanamcha Mungu. Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa." (Kurani 10:62-64)
Wakati wanadamu wote waliowahi kuumbwa watakusanywa kusimama uchi na bila kutahiriwa kwenye tambarare pana chini ya joto kali linalochoma la Jua, kundi la wanaume na wanawake wachaji Mungu litawekwa chini ya kivuli cha Kiti cha Enzi cha Mungu. Mtume Muhammad alibashiri nafsi hizo zilizobahatika kuwa ni za akina nani, Siku ambayo hakutakuwa na kivuli kingine:[3]
·mtawala mwadilifu ambaye hakutumia vibaya mamlaka yake, bali alipitisha haki iliyofunuliwa na Mungu miongoni mwa watu
·kijana ambaye alikua akimuabudu Mola wake Mlezi na akadhibiti matamanio yake ili aendelee kuwa safi
·wale ambao nyoyo zao zilishikamana na Misikiti, wakitamani kurejea humo kila walipotoka
·wale waliopendana kwa ajili ya Mungu
·wale waliojaribiwa na wanawake warembo wenye kuvutia, lakini hofu yao ya Mungu iliwazuia wasitende dhambi
·yule aliyetoa sadaka kwa moyo halisi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kuzificha sadaka zao
·yule ambaye alilia kwa hofu ya Mungu akiwa peke yake
Matendo mahususi ya ibada pia yatawaweka watu salama siku hiyo, yaani:
·jitihada za ulimwengu huu za kuwaondolea taabu wanaotaabika, kuwasaidia maskini, na kupuuza makosa ya wengine, zitawaondolea watu dhiki katika Siku ya Hukumu[4]
·huruma iliyoonyeshwa kwa wadaiwa (kwa kuwasamehe na kufuta madeni yao)[5]
·waadilifu ambao wanawatendea haki familia zao na kufanya uadilifu katika mambo waliyopewa kama amana wasimamie[6]
·kudhibiti hasira[7]
·mwenye hutoa wito kwa sala[8]
·kuzeeka mtu akiwa katika hali au ndani ya Uislamu[9]
·kutia udhu wa kiibada (kutawadha) mara kwa mara na ipasavyo[10]
·wale wanaopigana pamoja na Isa bin Maryam dhidi ya Dajjali na jeshi lake[11]
·kifo cha kishahidi
Mwenyezi Mungu atamleta muumini karibu naye, atamhifadhi, atamfunika (atamsitiri), na atamuuliza kuhusu madhambi yake. Baada ya kuyakubali madhambi yake, ataamini kuwa ameangamia, lakini Mwenyezi Mungu atasema:
"Nilikufichia duniani, na nakusamehe Siku hii ya leo."
Atakemewa kwa mapungufu yake,[12] lakini atakabidhiwa kitabu chake cha matendo mema kwa mkono wake wa kulia.[13]
"Ama atakayepewa daftari lake kwa mkono wa kulia! Basi huyo atahesabiwa hesabu nyepesi!" (Kurani 84:7-8)
Kwa furaha akitazama rekodi yake, atatangaza furaha yake:
"Basi ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: ‘Haya someni kitabu changu! Hakika nilijua ya kuwa nitapokea hesabu yangu.’ Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza – katika Bustani ya juu, matunda yake yakaribu. [Waambiwe]: ‘Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyotanguliza katika siku zilizopita.’" (Kurani 69:19-24)
Kisha rekodi ya matendo mema itapimwa, kihalisi, ili kubainisha kama inapita rekodi ya matendo mabaya ya mtu, na ili thawabu au adhabu itolewe ipasavyo.
"Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hesabu." (Kurani 21:47)
"Basi anayetenda chembe ya wema, atauona!" (Kurani 99:7)
"Jambo zito zaidi litakalowekwa katika Mizani ya mtu Siku ya Kiyama [baada ya ushahidi wa Imani] ni tabia njema, na Mwenyezi Mungu anamchukia mtu mpujufu (mchafu kutokana na mdomo wake au maneno) na mtu fasiki au asiye mwadilifu (mchafu kutokana na vitendo vyake)." (Al-Tirmidhi)
Waumini hao watakata kiu yao kutoka kwenye hifadhi maalumu (Raudhwa) iliyowekwa kwa ajili ya Mtume Muhammad. Yeyote atakayekunywa humo hataona kiu tena. Uzuri wake, ukubwa wake, na ladha tamu nzuri, imeelezwa kwa kina na Mtume.
Waumini wa Uislamu - wakosefu miongoni mwao na wachaji Mungu - pamoja na wanafiki wataachwa katika bonde kubwa baada ya makafiri kufukuzwa na kukimbizwa Motoni. Daraja refu linalopita juu Motoni na kugubikwa na giza litawatenganisha na Pepo.[14]Waamini watapata nguvu na faraja katika kuvuka kwao kwa haraka juu ya moto unaonguruma wa Jehanamu na kupitia ‘nuru’ ambayo Mungu ataiweka mbele yao, ikiwaongoza kwenye makao yao ya milele:
"Siku utakapowaona Waumini wanaume na Waumini wanawake, nuru yao iko mbele yao, na kuliani kwao: ‘Furaha yenu leo - Bustani zipitazo mito kati [chini] yake, mtakaa humo milele.’ Huko ndiko kufuzu kukubwa." (Kurani 57:12)
Hatimaye, baada ya kuvuka daraja, waumini watatakaswa kabla ya kuingia Peponi. Vifundo vyote kati ya waumini vitasuluhishwa ili kwamba hakuna mwanamume anayeweka kinyongo dhidi ya mwingine.[15]
Rejeleo la maelezo:
[1] Kwa maana kwamba haogopi adhabu ya Mungu na hivyo kufanya dhambi.
[2]Silsila Al-Saheehah.
[3]Saheeh Al-Bukhari.
[4]Saheeh Al-Bukhari.
[5]Mishkat.
[6]Saheeh Muslim.
[7]Musnad.
[8]Saheeh Muslim.
[9]Jami al-Sagheer.
[10]Saheeh Al-Bukhari.
[11]Ibn Majah.
[12]Mishkat.
[13]Saheeh Al-Bukhari. Ishara ya kuwa wao ni katika watu wa Peponi, kinyume na wale watakaopewa daftari lao la matendo yao kwa mikono yao ya kushoto au nyuma ya migongo yao.
[14] Saheeh Muslim.
[15]Saheeh Al-Bukhari
Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 4 kati ya 8): Muumini na Pepo
Maelezo: Jinsi wanavyopokelewa humo wenye kufaulu kufika Peponi kwa ajili ya imani.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,341
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Peponi
Waumini wataongozwa kuelekea kwenye milango minane mikuu ya Peponi. Huko, watapata mapokezi ya furaha ya kimalaika na kupongezwa kwa sababu ya kuwasili kwao salama na kuokoka na Jahannamu.
"Na waliomcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea Peponi kwa makundi, mpaka watakapofikilia, nayo milango yake imekwishafunguliwa. Walinzi wake watawaambia: ‘Salaam Alaikum, [Amani iwe juu yenu]! Mmetwahirika. Basi ingieni humu mkae milele.’" (Kurani 39:73)
(Watu wema wataambiwa): "Ewe nafsi iliyotua! Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha. Basi ingia miongoni mwa waja wangu. Na ingia katika Pepo yangu." (Kurani 89:27-30)
Waliobora miongoni mwa Waislamu wataingia Peponi kwanza. Waliowema zaidi nao watapandishwa daraja za juu.[1]
"Na atakayemjia [Mwenyezi Mungu] naye ni muumini aliyetenda mema, basi hao ndio wenye vyeo vya juu." (Kurani 20:75)
"Na wa mbele [katika imani] watakuwa mbele [Akhera]. Hao ndio watakaokaribishwa [mbele kwa Mungu], katika Bustani zenye neema..." (Kurani 56:10-12)
Maelezo ya Kurani ya Pepo yanatupatia maono ya jinsi palivyo pahali pazuri sana. Nyumba ya milele ambayo itatimiza matamanio yetu yote mazuri, ishawishi hisia zetu zote, itupe kila kitu tunachoweza kutaka na mengine mengi zaidi. Mungu anaielezea Pepo Yake kuwa kama ardhi iliotengenezwa kwapoda au unga laini wa miski,[2] udongo wa zafarani,[3] matofali ya dhahabu na fedha, na changarawe za lulu na yakuti/ rubi/ marijani. Chini ya bustani za Peponi inapita mito ya maji inayong'aa, ya maziwa matamu, ya asali safi, na ya mvinyo usio na kilevi. Hema zilizo kwenye kingo zao ni mfano wa makuba ya lulu yaliyo wazi.[4] Nafasi nzima imejazwa mwangaza unaometameta, mimea yenye kutoa harufu nzuri na manukato ambayo yanaweza kunusika kutoka mbali.[5] Kuna makasri ya kifahari, majumba makubwa, mizabibu, mitende, mikomamanga,[6] myungiyungi na mikangazi ambayo mashina yake yametengenezwa kwa dhahabu.[7] Matunda yaliyoiva, mengi ya kila aina: jamii ya beri au vitole, jamii ya machungwa, aprikoti, zabibu, tikiti, mbwembwe; kila aina ya matunda, ya kitropiki na ya kigeni; chochote ambacho waumini wangeweza kutamani!
"…na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia..." (Kurani 43:71)
Kila Muumini atakuwa na mke mrembo sana, mchaji Mungu na msafi, aliyevaa mavazi maridadi; nakutakuwa na mengi zaidi katika ulimwengu mpya wa furaha ya milele, ng'aavu.
"Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho - ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda." (Kurani 32:17)
Pamoja na furaha za kimwili, Pepo pia itawapa wakazi wake hali ya furaha ya kihisia na kisaikolojia, kama Mtume alivyosema:
"Mwenye kuingia Peponi amebarikiwa maisha ya furaha; hatahisi huzuni kamwe, nguo zake hazitachakaa, na ujana wake hautafifia. Watu watasikia mwito wa kimungu: ‘Ninawapa hiba ya kwamba mtakuwa na afya njema na kamwe hamtaugua, mtaishi na kamwe hamtakufa, mtakuwa vijana na kamwe hamzeeka, mtakuwa na furaha na kamwe hamtahisi huzuni.’" (Saheeh Muslim)
Hatimaye, jambo litakalopendeza zaidi macho litakuwa kuona Uso wa Mwenyezi Mungu Mwenyewe. Kwa muumini wa kweli, kuuona utukufu wa Mungu ni kuwa ameshinda tuzo kuu.
"Zipo nyuso siku hiyo zitakazong'ara, zinamwangallia Mola wao Mlezi." (Kurani 75:22-23)
Hii ndiyo Pepo, makazi ya milele na mwisho wa safari ya muumini mwema. Tunamuomba Mwenyezi Mungu, Aliye Juu Zaidi, atufanye tustahiki kupata Pepo.
Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 5 kati ya 8): Kafiri ndani ya Kaburi
Maelezo: Ufafanuzi wa maisha ndani ya kaburi kuanzia kifo hadi Siku ya Hukumu kwa kafiri aliyekanusha.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 1
- Imetazamwa: 5,034
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Mauti yanapomkaribia kafiri muovu, anafanywa kuhisi kitu cha joto la Moto wa Jehanamu. Mwonjo huu wa kile kitakachokuja humfanya aombe kupewa nafasi ya pili duniani kufanya yale mema ambayo alijua angepaswa kuyafanya. Ole wake! Ombi lake litakuwa bure.
"Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: ‘Mola wangu Mlezi! Nirudishe (duniani). Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha.’ Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi (maisha ya Barzakhi) mpaka siku watakapofufuliwa." (Kurani 23:99-100)
Ghadhabu za Mungu na adhabu huwasilishwa kwa roho mbaya na malaika wabaya sana, weusi ambao hukaa mbali nayo:
"Pokea habari za kusikitisha za maji yanayochemka, usaha kutoka kwa jeraha, na mateso mengi kama hayo." (Ibn Majah, Ibn Katheer)
Roho iliyokufuru haitarajii kukutana na Mola wake Mlezi, kama Mtume alivyoeleza:
"Inapokaribia wakati wa kifo cha kafiri, hupokea habari mbaya za adhabu ya Mwenyezi Mungu na malipo yake, ambapo hakuna kinachochukiza zaidi kwake kuliko yale yaliyo kabla yake. Kwa hiyo, anachukia kukutana na Mungu, na Mungu pia anachukia kukutana naye." (Saheeh Al-Bukhari)
Mtume pia alisema:
"Yeyote anayependa kukutana na Mungu, Mungu hupenda kukutana naye, na yeyote anayechukia kukutana na Mungu, Mungu huchukia kukutana naye." (Saheeh Al-Bukhari)
Malaika wa mauti anakaa kichwani mwa kafiri katika kaburi lake na kusema: "Nafsi mbaya, toka mwilini kwa hasira ya Mwenyezi Mungu" huku akiinyakua roho nje ya mwili.
"...Na lau ungeliwaona madhalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti, na malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia: ‘Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyo ya haki, na mlivyokuwa mkizifanyia kiburi ishara zake.’" (Kurani 6:93)
"Na laiti ungeliona malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao, na kuwaambia: ‘Ionjeni adhabu ya Moto!’" (Kurani 8:50)
Nafsi mbaya huacha mwili kwa shida sana, inayotolewa na malaika kama vibaniko huvutwa kupitia pamba yenye unyevu.[1] Kisha Malaika wa Mauti huikamata roho na kuiweka kwenye gunia lililofumwa kwa nywele ambalo linatoa uvundo uliooza, kama uchafu wa kukirihisha wa mfu uliooza wenye harufu mbaya zaidi inayopatikana duniani. Kisha malaika huichukua roho juu akipita kundi jingine la malaika wanaomuuliza: "Nani huyu roho mbaya?" na atawajibu: "Fulani wa fulani, mwana wa fulani na fulani." - akitumia majina mabaya sana ambayo aliwahi kuitwa wakati alipokuwa duniani. Kisha, anapoletwa kwenye mbingu ya chini kabisa, ombi linatumwa kwamba lango lake lifunguliwe, lakini ombi hilo linakataliwa. Mtume alipokuwa akielezea matukio haya, na alipofikia hapa, alisoma:
"...hawafunguliwi milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia katika tundu la sindano..." (Kurani 7:40)
Mungu atasema: "Rekodi kitabu chake katika Sijjin katika ardhi ya chini kabisa."
…na roho yake itatupwa chini. Katika hatua hii, Mtume, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisoma:
"...Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali." (Kurani 22:31)
Kisha nafsi ovu itarejeshwa kwenye mwili wake na wale malaika wawili wa kutisha, Munkar na Nakir, watakuja humo kwa ajili ya kumhoji. Baada ya kumfanya aketi, watauliza:
Munkar na Nakir: "Nani Mola wako?"
Roho ya Asiyeamini: "Aah, aah, sijui."
Munkar na Nakir: "Nini dini yako?"
Roho ya Asiyeamini: "Aah, aah, sijui."
Munkar na Nakir: "Unasemaje kuhusu huyu mwanamume (Muhammad) aliyetumwa kwenu?"
Roho ya Asiyeamini: "Aah, aah, sijui."
Akiwa ameshindwa mtihani wake, kichwa cha kafiri kitapigwa kwa nyundo ya chuma kwa nguvu nyingi ya kishindo hivi kwamba ingebomoa mlima. Kilio kitasikika kutoka mbinguni: "Amesema uongo, basi mkunjulieni mazulia ya Jehanamu, na mfungulie mlango wa kuingia Motoni."[2] Sakafu ya kaburi lake litawashwa moto kidogo mkali wa Jehanamu, na kaburi lake litafanywa kuwa jembamba na kubanwa, kiasi cha mbavu zake kuunganika mwili wake unapopondwa.[3] Kisha kiumbe chenye sura mbaya, kilichovaa nguo mbaya na kutoa harufu mbaya ya kukirihisha kitaijia nafsi iliyokufuru na kusema: "Uwe na huzuni kwa yale yanayokuchukiza, kwani hii ndiyo siku yako uliyoahidiwa." Kafiri atauliza: "Wewe ni nani, mwenye uso mbaya na kuleta maovu?"Kile kiumbe kibaya kitajibu:"Mimi ni matendo yako maovu!"Kisha kafiri ataonjeshwa majuto ya uchungu huku akionyeshwa yale yangekuwa makazi yake Peponi - lau angeishi maisha mema ya uadilifu - hayo yatatendeka kabla ya kufunguliwa mlango kwa ajili yake kila asubuhi na jioni ukimuonyesha makazi yake halisi ya Motoni.[4]Mwenyezi Mungu anataja katika Kitabu Chake jinsi watu waovu wa Firauni wanavyoteseka wakati huu kwa kufichuliwa Jehanamu kutoka ndani ya makaburi yao:
"Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itakapofika Saa ya Kiyama patasemwa: ‘Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa!’" (Kurani 40:46)
Akiwa ameingiwa na hofu na chuki, wasiwasi na kukata tamaa, kafiri ndani ya kaburi lake ataendelea kuuliza: "Mola wangu Mlezi, usilete saa ya mwisho. Usilete saa ya mwisho."
Sahaba, Zaid b. Thabit, alisimulia jinsi, wakati Mtume Muhammad na Maswahaba zake walipokuwa wakipita kando ya baadhi ya makaburi ya washirikina, farasi wa Mtume alikurupuka na karibu kumwangusha. Kisha Mtume, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu zimshukie, akasema:
"Watu hawa wanateswa makaburini mwao, na lau si kwamba nyinyi mngeacha kuwazika wafu wenu, ningemuomba Mwenyezi Mungu awape masikizi ya kusikia adhabu ya kaburini ambayo mimi (na farasi huyu) huisikia." (Saheeh Muslim)
Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 6 kati ya 8): Asiyeamini wakati wa Siku ya Hukumu
Maelezo: Baadhi ya mashtaka atakayokutana nayo kafiri Siku ya Kiyama.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,694
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Utisho mkubwa utawapata watakaofufuliwa Siku kubwa ya Kiyama.
"…Hakika Yeye anawaahirisha tu mpaka siku yatakapokodoka macho yao." (Kurani 14:42)
Kafiri atafufuliwa kutoka kwenye ‘kaburi’ lake kama ilivyoelezwa na Mungu:
"Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo. Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyokuwa wakiahidiwa." (Kurani 70:43-44)
Moyo utakuwa ukitetemeka, utachanganyikiwa kuhusu adhabu gani mbaya inawangojea:
"Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi. Giza totoro litazifunika. Hao ndio makafiri watenda maovu." (Kurani 80:40-42)
"Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayoyafanya madhalimu. Hakika Yeye anawaahirisha tu mpaka siku yatakapokodoka macho yao. Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na nyoyo zao tupu." (Kurani 14:42-43)
Watakusanywa makafiri - kama walivyozaliwa wakiwa uchi na hawajatahiriwa - kwenye uwanja mkubwa, wakikimbizwa hali ya kuwa nyuso zimeinamishwa, hawaoni, hawasikii na hawasemi:
"...Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makazi yao ni Jehanamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu." (Kurani 17:97)
"Na atakayejiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu." (Kurani 20:124)
Mara tatu "watakutana" na Mungu. Mara ya kwanza watajaribu kujitetea kwa hoja zisizo na maana dhidi ya Mwenyezi Mungu, wakisema mambo kama vile: "Mitume hawakutujia!" Ingawa Mwenyezi Mungu ameteremsha katika Kitabu Chake:
"…Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume." (Kurani 17:15)
"…msije mkasema: ‘Hakufika kwetu mbashiri wala mwonyaji….’" (Kurani 5:19)
Mara ya pili, watawasilisha visingizio vyao huku wakikiri hatia yao. Hata mashetani watajaribu kujitoa lawama kutokana na makosa yao ya kuwapoteza watu:
"Mwenzake aseme: ‘Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali.’" (Kurani 50:27)
Lakini Mungu, Aliye Juu Zaidi na Mwadilifu, hatadanganyika. Atasema:
"...Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu. Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu." (Kurani 50:28-29)
Mara ya tatu, nafsi mbaya itakutana na Muumba wake ili kupokea Kitabu chake cha Matendo[1], yenye rekodi isiyosaza chochote.
"Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyoogopa kwa yale yaliyomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyoyatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote." (Kurani 18:49)
Baada ya kupokea kumbukumbu zao, waovu watakemewa mbele ya wanadamu wote.
"Na wakahudhurishwa mbele ya Mola wako Mlezi kwa safu (wakaambiwa): Mmetujia kama tulivyokuumbeni mara ya kwanza! Bali mlidai kwamba hatutakuwekeeni miadi!" (Kurani 18:48)
Mtume Muhammad amesema: "Hawa ni wale ambao hawakumwamini Mungu!"[2] Na ni hawa ambao Mungu atawauliza kuhusiana na neema walizozipuuza. Kila mmoja ataulizwa: ‘Ulifikiri Tungekutana?’ Na kila mmoja atajibu: ‘Hapana!’ Mungu atamwambia: ‘Nitakusahau kama ulivyonisahau Mimi!’[3] Kisha kafiri atakapojaribu kudanganya, akijitoa, Mwenyezi Mungu atauziba mdomo wake, na viungo vyake vya mwili badala yake vitamshuhudilia dhidi yake.
"Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyokuwa wakiyachuma." (Kurani 36:65)
Zaidi ya madhambi yake, kafiri pia atabeba madhambi ya wale aliowapoteza.
"Na wanapoambiwa: ‘Kateremsha nini Mola wenu Mlezi?’ Husema: ‘Hadithi za kubuni za watu wa kale!’ Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu Siku ya Kiyama, na sehemu ya mizigo ya wale wanaowapoteza bila ya kujua. Angalia, ni maovu mno hayo wanayoyabeba!" (Kurani 16:24-25)
Maumivu ya kisaikolojia ya kunyimwa, upweke na kuachwa, yote yatasababisha mateso ya kimwili.
"…wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu chungu." (Kurani 3:77)
Wakati Mtume Muhammad atawaombea kwa niaba ya waumini wote kwa njia ya shufaa, kafiri hatapata mwombezi; kwani yeye aliabudu miungu ya uongo badala ya Mungu Mmoja, wa Kweli.[4]
"…Na wenye kudhulumu hawana mlinzi wala msaidizi." (Kurani 42:8)
Watakatifu wao na washauri wao wa kiroho watajitenga nao, na kafiri angetamani angerudi kwenye maisha haya ya duniani na kuwafanyia vivyo hivyo wale ambao sasa wanawakana wao.
"Na watasema wale waliofuata: ‘Laiti tungeweza kurudi tukawakataa wao kama wanavyotukataa sisi!’ Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyowaonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni." (Kurani 2:167)
Huzuni ya nafsi iliyojaa dhambi itakuwa kubwa sana hivi kwamba ataomba: ‘Ewe Mola nirehemu na uniingize Motoni.’[5] Ataulizwa ‘Je, ungependa kuwa na dhahabu iliyojaa dunia nzima ili uweze kuilipa ili ujikomboe au uwe huru?’ Ambapo atajibu: ‘Ndiyo.’ Ambapo ataambiwa: ‘Uliulizwa kitu rahisi zaidi kuliko hicho - mwabudu Mungu peke yake.’[6]
"Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu…" (Kurani 98:5)
"Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo, naye amlipe hesabu yake sawasawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu." (Kurani 24:39)
"Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyotawanyika." (Kurani 25:23)
Kisha nafsi iliyokufuru itakabidhiwa kwa mkono wake wa kushoto na kutoka nyuma ya mgongo wake, kumbukumbu yake iliyoandikwa na kutunzwa na malaika ambao walibainisha kila kitendo chake katika maisha yake ya duniani.
"Na ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: ‘Laiti nisingelipewa kitabu changu! Wala nisingelijua nini hesabu yangu.’" (Kurani 69:25-26)
"Na ama atakayepewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake, basi huyo ataomba kuteketea." (Kurani 84:10-11)
Hatimaye ataingizwa Motoni:
"Na waliokufuru wataongozwa kuendea Jehanamu kwa makundi. Mpaka watakapoifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: ‘Kwani hawakukujilieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi na kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii?’ Watasema: ‘Kwani! Lakini limekwisha thibiti neno la adhabu juu ya makafiri.’" (Kurani 39:71)
Wa kwanza kuingia Motoni watakuwa wapagani (asiyeamini Mungu wala kufuata dini yoyote), wakifuatiwa na wale Mayahudi na Wakristo walioiharibu dini ya kweli ya mitume wao.[7] Wengine watakokotwa Motoni, wengine wataanguka humo, wakinyakuliwa kwa kulabu.[8] Wakati huo, kafiri atatamani lau angeligeuzwa kuwa udongo, badala ya kuvuna matunda machungu ya matendo yake maovu.
"Hakika tumekuhadharisheni adhabu iliyo karibu kufika; Siku ambayo mtu atakapoona yaliyotangulizwa na mikono yake; na kafiri atasema: ‘Laiti ningelikuwa udongo!’" (Kurani 78:40)
Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 7 kati ya 8): Kafiri na Moto
Maelezo: Jinsi Moto wa Jehanamu utawapokea makafiri.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,170
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Jehanamu itawapokea makafiri kwa ghadhabu yake na kishindo chake.
"…na Sisi tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa. Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yake na mngurumo wake." (Kurani 25:11-12)
Watakapoikaribia, watatazamia kufungwa pingu na hatima yao ni kufanywa kuni.
"Hakika Sisi tumewaandalia makafiri minyororo na pingu na Moto mkali." (Kurani 76:4)
"Hakika Sisi tunazo pingu nzito na Moto unaowaka kwa ukali kabisa!" (Kurani 73:12)
Malaika watakimbia kutii amri ya Mwenyezi Mungu ya kumkamata na kumfunga pingu:
"(Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu!" (Kurani 69:30)
"…na Tutaweka makongwa shingoni mwao waliokufuru..." (Kurani 34:33)
Atafungwa kwa minyororo...
"…mnyororo wenye [kipimo cha] urefu wa dhiraa sabini!" (Kurani 69:32)
...ataburutwa:
"Zitakapokuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa." (Kurani 40:71)
Wakiwa wamefungwa chini, kwa minyororo, na kuburutwa ili watumbukizwe Motoni, watasikia hasira ya Moto.
"Na kwa waliomkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jehanamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo! Watakapotupwa humo watausikia mngurumo wake na huku inafoka..." (Kurani 67:6-8)
Kwa kuwa watakokotwa kwenye uwanja mkubwa wa kukusanywa, wakiwa uchi na wenye njaa, watawaomba watu wa Peponi maji:
"Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi: ‘Tumimieni maji, au chochote alichokuruzukuni Mwenyezi Mungu.’ Nao watasema: ‘Hakika Mwenyezi Mungu ameviharimisha hivyo kwa makafiri.’" (Kurani 7:50)
Wakati huo huo waumini ndani ya Pepo wakipokelewa kwa heshima, kustareheshwa, na kuhudumiwa kwa karamu za ladha, naye kafiri atakula akiwa ndani ya Moto.
"Kisha nyinyi, mliopotea, mnaokanusha, kwa yakini mtakula mti wa Zakumu. Na kwa mti huo mtajaza matumbo." (Kurani 56:51-53)
Zakumu: mti ambao mizizi yake iko chini ya Jahannamu na ambayo inatawanya matawi yake sehemu nyingine; matunda yake yanafanana na vichwa vya mashetani:
"Je, kukaribishwa hivi [Peponi] si ndio bora, au mti wa Zakumu? Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa waliodhulumu. Hakika huo ni mti unaotoka katikati ya Jehanamu. Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashetani. Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo." (Kurani 37:62-66)
Waovu watakuwa na mlo mwingine wa kula, mwingine ambao hukaba koo,[1] na mwingine kama vichaka vikavu, vyenye miiba.[2]
"Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni. Chakula hicho hawakili ila wakosefu." (Kurani 69:36-37)
Na kufuatanisha vyakula vyao vya kusikitisha, ni vinywaji vya mchanganyiko baridi sana wa usaha wao wenyewe, damu, jasho na usaha wa jeraha[3] pamoja na maji yanayochemka, yanayotokota na kuteketeza, ambayo huyeyusha matumbo yao;
"…na wakinyweshwa maji yanayochemka ya kuwakata matumbo yao?" (Kurani 47:15)
Mavazi ya wakaazi wa Motoni yametengenezwa kwa moto na lami.
"...Basi waliokufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayochemka." (Kurani 22:19)
"Nguo zao zitakuwa za lami, na Moto utazigubika nyuso zao." (Kurani 14:50)
Viatu vyao,[4] kitanda, na dari vivyo hivyo vitatengenezwa kwa moto;[5] adhabu inayozunguka mwili mzima, kutoka kichwa kisichojali hadi kidole cha mguu kinachovuka mipaka:
"Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayochemka." (Kurani 44:48)
"Siku itakapowafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na itasemwa: ‘Onjeni hayo mliyokuwa mkiyatenda!’" (Kurani 29:55)
Adhabu yao katika Jehanamu itatofautiana kulingana na ukafiri wao na madhambi mengineo.
"Hasha! Atavurumishwa katika Hutwama. Na nani atakujuvya ni nini Hutwama? Moto wa Mwenyezi Mungu uliowashwa. Ambao unapanda nyoyoni. Hakika huo utafungiwa nao, kwenye nguzo zilizonyooshwa." (Kurani 104:4-9)
Kila wakati ngozi ikiungua, itabadilishwa na ngozi mpya:
"Hakika wale waliozikataa ishara Zetu tutawaingiza Motoni. Kila zitakapowiva ngozi zao tutawabadilishia ngozi nyengine ili waionje hiyo adhabu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hekima." (Kurani 4:56)
Mbaya zaidi ni kuwa, adhabu itaendelea kuongezeka:
"Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu!" (Kurani 78:30)
Athari ya kisaikolojia ya kuadhibiwa huku itakuwa kubwa sana. Itakuwa adhabu kali sana hata watakaoteseka kwa maumivu yake watapiga kelele ili iongezewe waliosababisha wao kupotea:
"Waseme: ‘Mola wetu Mlezi! Aliyetusabibisha haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni.’" (Kurani 38:61)
Wenye kuthubutu watafanya jaribio lao la kwanza kutoroka, lakini:
"Na kwa ajili yao yatakuwapo marungu ya chuma. Kila wakitaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo, na wataambiwa: ‘Onjeni adhabu ya kuungua!’" (Kurani 22:21-22)
Baada ya kushindwa mara kadhaa, watatafuta msaada kutoka kwa Ibilisi, Shetani Mkuu mwenyewe.
"Na Shetani atasema itakapokatwa hukumu: ‘Hakika Mwenyezi Mungu alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipokuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhalimu watakuwa na adhabu chungu.’" (Kurani 14:22)
Wakiwa wamevunjika moyo na Shetani, watawaelekea malaika walindao Jehanamu ili wawapunguzie adhabu, hata kama kwa siku moja tu:
"Na walio Motoni watawaambia walinzi wa Jehanamu: ‘Mwombeni Mola wenu Mlezi atupunguzie walau siku moja ya adhabu.’" (Kurani 40:49)
Wakingoja majibu kwa muda ambao Mungu apendavyo, walinzi watarudi na kuuliza:
"Nao watasema: ‘Je, hawakuwa wakikufikieni mitume wenu kwa hoja zilizo wazi?’ Watasema: ‘Kwani?’ Watasema: ‘Basi ombeni! Na maombi ya makafiri hayawi ila ni kupotea bure.’" (Kurani 40:50)
Wakiwa wamepoteza matumaini ya kupunguziwa adhabu, watatafuta njia ya kuuawa. Wakati huu watamgeukia Mlinzi Mkuu wa Jehanamu, malaika aitwaye Malik, wakimsihi kwa muda wa miaka arobaini:
"Nao watapiga kelele waseme: ‘Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi!...’" (Kurani 43:77)
Jibu la mkato la kupinga kwake baada ya miaka elfu litakuwa:
"…Naye aseme: ‘Hakika nyinyi mtakaa humo humo!" (Kurani 43:77)
Hatimaye watarejea kwa Yule Ambaye walikataa kurejea kwake wakiwa duniani, wakiomba fursa ya mwisho:
"(Watasema) ‘Mola wetu Mlezi! Tulizidiwa na uovu [upotofu] wetu na tukawa watu tuliopotea. Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni. Na tufanyapo tena [maovu], basi kweli sisi ni wenye kudhulumu.’" (Kurani 23:106-107)
Jibu la Mungu litakuwa hivi:
"...‘Tokomeeni humo, wala msinisemeze." (Kurani 23:108)
Maumivu kutoka kwa majibu haya yatakuwa mabaya zaidi kuliko mateso yao ya moto. Kwani kafiri atajua kukaa kwake Motoni ni milele, na kutokuwepo kwake Peponi ni hakika na ni uamuzi wa mwisho:
"Hakika wale waliokufuru na wakadhulumu hawi Mwenyezi Mungu kuwasamehe wala kuwaongoa njia. Isipokuwa njia ya Jehanamu. Humo watadumu milele. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi." (Kurani 4:168-169)
Kunyimwa na huzuni kubwa zaidi kwa asiyeamini itakuwa ya kiroho: atazibwa na kunyimwa kumuona Mungu:
"Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi." (Kurani 83:15)
Kama vile walivyokataa “kumwona” katika maisha haya, watatengwa na Mungu katika maisha yajayo. Waumini watawadhihaki.
"Basi leo walioamini ndio watawacheka makafiri, nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia. Je, makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda?" (Kurani 83:34-36)
Kukata tamaa na huzuni yao kamili itafikia kilele wakati kifo kitakapoletwa kama umbo la kondoo dume na kuchinjwa mbele yao, kuashiria kwamba hakuna kimbilio litakalopatikana baada ya uamuzi wa mwisho wa maangamizo.
"Na waonye, (Ewe Muhammad), siku ya majuto itakapokatwa amri; nao wamo katika ghafla, wala hawaamini!" (Kurani19:39)
Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 8 kati ya 8): Hitimisho
Maelezo: Baadhi ya sababu za kuwepo Pepo na Moto.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 1
- Imetazamwa: 4,808
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Muhammad, Mtume wa Uislamu, aliyefariki mwaka 632, alisimulia:
"Dunia hii ni gereza kwa Muumini, lakini kwa kafiri ni Pepo. Na kwa kafiri, Akhera itakuwa gereza, lakini kwa Muumini itakuwa ni Pepo yake."
Wakati mmoja, katika kipindi cha mwanzo cha Uislamu, Mkristo maskini alitokea kwa mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Uislamu, ambaye wakati huo alikuwa amepanda farasi mzuri na aliyevaa nguo nzuri. Mkristo huyo alimsomea Muislamu mwenye mali Hadithi iliyonukuliwa hapo juu, kabla ya kutoa maoni: "Lakini mimi nasimama mbele yako nikiwa sio Muislamu, maskini na fukara katika dunia hii, ilhali wewe ni Muislamu, tajiri na aliyefanikiwa.” Mwanachuoni wa Uislamu akamjibu: “Hakika ndivyo hivyo. Lakini lau ungejua hakika ya yale yanayoweza kukungojea (ya adhabu ya milele) huko Akhera, ungejiona kuwa wewe sasa uko Peponi kwa kulinganisha. Na lau ungejua hakika ya yale yanayoweza kuningojea (ya raha ya milele) huko Akhera, ungeniona kuwa mimi sasa niko gerezani kwa kulinganisha."
Kwa hivyo, ni kutokana na rehema kubwa na uadilifu wa Mwenyezi Mungu kwamba aliumba Mbingu na Jehanamu. Ujuzi wa Moto wa Jehanamu unatumika kumzuilia mwanadamu asitende maovu na wakati huo huo kuchungulia kwenye hazina za Peponi kunamchochea kutenda matendo mema na kuwa mwadilifu. Wale waliomkadhibisha Mola wao Mlezi na wakatenda maovu na hawakutubia, wataingia Jehanamu, mahali pa maumivu ya hakika na mateso. Wakati malipo ya uadilifu ni pahali pasipofikirika uzuri na ukamilifu wake, nayo ni Pepo ya Mungu.
Mara kwa mara, watu hushuhudia wema wa nafsi zao wenyewe kwa kudai kwamba wema wowote wanaoufanya ni kwa njia safi na pekee ya upendo wa kweli wa Mungu au kuishi kulingana na kanuni za maadili na wema wa ulimwengu wote, na kwa ajili hiyo, hawahitaji fimbo au karoti yoyote (ya kuwalazimisha au kuwashawishi kuyatenda mema). Lakini Mungu anapozungumza na mwanadamu ndani ya Kurani, hufanya hivyo akijua ugeugeu wa nafsi ya mwanadamu. Furaha za Peponi ni furaha halisi, za kimwili na zinazoonekana. Mwanadamu anaweza kuanza kufahamu jinsi ambavyo uchu wa kutaka vyakula, mavazi na makazi ya Peponi vilivyo kamilifu, vingi na visivyoisha, kuwa ni halisi kwa sababu anafahamu jinsi vitu hivyo vinaweza kuridhisha na kuwa vitamu katika ulimwengu halisia wa sasa.
"Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundo ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo mema." (Kurani 3:14)
Vivyo hivyo, mwanadamu anaweza kuanza kufahamu jinsi Moto wa mateso na wa kuogofya unavyoweza kuwa hasa kwa sababu anajua jinsi uchomaji wa moto unavyoweza kuwa mbaya sana katika ulimwengu huu. Kwa hivyo, safari ya roho baada ya kifo, kama ilivyoelezwa kwetu kwa kina na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu zimshukie, inapaswa, kwa vyovyote vile, kutuchochea sisi wanadamu wote kutambua lengo tukufu: nalo ni kumwabudu na kumtumikia Muumba wetu kwa upendo wa dhati usio na ubinafsi, na kunyenyekea na kushukuru. Baada ya yote,
"...nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu..." (Kurani 98:5)
Lakini, kuhusu yale makundi mengi miongoni mwa wanadamu ambayo, katika zama zote, yalipuuza wajibu wao wa kimaadili kwa Mola wao Mlezi na wanadamu wenzao, basi yasisahau kwamba:
"Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Kiyama. Na atakayeepushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu." (Kurani 3:185)
Ongeza maoni