Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 6 kati ya 8): Asiyeamini wakati wa Siku ya Hukumu
Maelezo: Baadhi ya mashtaka atakayokutana nayo kafiri Siku ya Kiyama.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,686 (wastani wa kila siku: 5)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Utisho mkubwa utawapata watakaofufuliwa Siku kubwa ya Kiyama.
"…Hakika Yeye anawaahirisha tu mpaka siku yatakapokodoka macho yao." (Kurani 14:42)
Kafiri atafufuliwa kutoka kwenye ‘kaburi’ lake kama ilivyoelezwa na Mungu:
"Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo. Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyokuwa wakiahidiwa." (Kurani 70:43-44)
Moyo utakuwa ukitetemeka, utachanganyikiwa kuhusu adhabu gani mbaya inawangojea:
"Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi. Giza totoro litazifunika. Hao ndio makafiri watenda maovu." (Kurani 80:40-42)
"Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayoyafanya madhalimu. Hakika Yeye anawaahirisha tu mpaka siku yatakapokodoka macho yao. Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na nyoyo zao tupu." (Kurani 14:42-43)
Watakusanywa makafiri - kama walivyozaliwa wakiwa uchi na hawajatahiriwa - kwenye uwanja mkubwa, wakikimbizwa hali ya kuwa nyuso zimeinamishwa, hawaoni, hawasikii na hawasemi:
"...Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makazi yao ni Jehanamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu." (Kurani 17:97)
"Na atakayejiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu." (Kurani 20:124)
Mara tatu "watakutana" na Mungu. Mara ya kwanza watajaribu kujitetea kwa hoja zisizo na maana dhidi ya Mwenyezi Mungu, wakisema mambo kama vile: "Mitume hawakutujia!" Ingawa Mwenyezi Mungu ameteremsha katika Kitabu Chake:
"…Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume." (Kurani 17:15)
"…msije mkasema: ‘Hakufika kwetu mbashiri wala mwonyaji….’" (Kurani 5:19)
Mara ya pili, watawasilisha visingizio vyao huku wakikiri hatia yao. Hata mashetani watajaribu kujitoa lawama kutokana na makosa yao ya kuwapoteza watu:
"Mwenzake aseme: ‘Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali.’" (Kurani 50:27)
Lakini Mungu, Aliye Juu Zaidi na Mwadilifu, hatadanganyika. Atasema:
"...Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu. Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu." (Kurani 50:28-29)
Mara ya tatu, nafsi mbaya itakutana na Muumba wake ili kupokea Kitabu chake cha Matendo[1], yenye rekodi isiyosaza chochote.
"Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyoogopa kwa yale yaliyomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyoyatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote." (Kurani 18:49)
Baada ya kupokea kumbukumbu zao, waovu watakemewa mbele ya wanadamu wote.
"Na wakahudhurishwa mbele ya Mola wako Mlezi kwa safu (wakaambiwa): Mmetujia kama tulivyokuumbeni mara ya kwanza! Bali mlidai kwamba hatutakuwekeeni miadi!" (Kurani 18:48)
Mtume Muhammad amesema: "Hawa ni wale ambao hawakumwamini Mungu!"[2] Na ni hawa ambao Mungu atawauliza kuhusiana na neema walizozipuuza. Kila mmoja ataulizwa: ‘Ulifikiri Tungekutana?’ Na kila mmoja atajibu: ‘Hapana!’ Mungu atamwambia: ‘Nitakusahau kama ulivyonisahau Mimi!’[3] Kisha kafiri atakapojaribu kudanganya, akijitoa, Mwenyezi Mungu atauziba mdomo wake, na viungo vyake vya mwili badala yake vitamshuhudilia dhidi yake.
"Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyokuwa wakiyachuma." (Kurani 36:65)
Zaidi ya madhambi yake, kafiri pia atabeba madhambi ya wale aliowapoteza.
"Na wanapoambiwa: ‘Kateremsha nini Mola wenu Mlezi?’ Husema: ‘Hadithi za kubuni za watu wa kale!’ Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu Siku ya Kiyama, na sehemu ya mizigo ya wale wanaowapoteza bila ya kujua. Angalia, ni maovu mno hayo wanayoyabeba!" (Kurani 16:24-25)
Maumivu ya kisaikolojia ya kunyimwa, upweke na kuachwa, yote yatasababisha mateso ya kimwili.
"…wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu chungu." (Kurani 3:77)
Wakati Mtume Muhammad atawaombea kwa niaba ya waumini wote kwa njia ya shufaa, kafiri hatapata mwombezi; kwani yeye aliabudu miungu ya uongo badala ya Mungu Mmoja, wa Kweli.[4]
"…Na wenye kudhulumu hawana mlinzi wala msaidizi." (Kurani 42:8)
Watakatifu wao na washauri wao wa kiroho watajitenga nao, na kafiri angetamani angerudi kwenye maisha haya ya duniani na kuwafanyia vivyo hivyo wale ambao sasa wanawakana wao.
"Na watasema wale waliofuata: ‘Laiti tungeweza kurudi tukawakataa wao kama wanavyotukataa sisi!’ Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyowaonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni." (Kurani 2:167)
Huzuni ya nafsi iliyojaa dhambi itakuwa kubwa sana hivi kwamba ataomba: ‘Ewe Mola nirehemu na uniingize Motoni.’[5] Ataulizwa ‘Je, ungependa kuwa na dhahabu iliyojaa dunia nzima ili uweze kuilipa ili ujikomboe au uwe huru?’ Ambapo atajibu: ‘Ndiyo.’ Ambapo ataambiwa: ‘Uliulizwa kitu rahisi zaidi kuliko hicho - mwabudu Mungu peke yake.’[6]
"Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu…" (Kurani 98:5)
"Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo, naye amlipe hesabu yake sawasawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu." (Kurani 24:39)
"Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyotawanyika." (Kurani 25:23)
Kisha nafsi iliyokufuru itakabidhiwa kwa mkono wake wa kushoto na kutoka nyuma ya mgongo wake, kumbukumbu yake iliyoandikwa na kutunzwa na malaika ambao walibainisha kila kitendo chake katika maisha yake ya duniani.
"Na ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: ‘Laiti nisingelipewa kitabu changu! Wala nisingelijua nini hesabu yangu.’" (Kurani 69:25-26)
"Na ama atakayepewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake, basi huyo ataomba kuteketea." (Kurani 84:10-11)
Hatimaye ataingizwa Motoni:
"Na waliokufuru wataongozwa kuendea Jehanamu kwa makundi. Mpaka watakapoifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: ‘Kwani hawakukujilieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi na kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii?’ Watasema: ‘Kwani! Lakini limekwisha thibiti neno la adhabu juu ya makafiri.’" (Kurani 39:71)
Wa kwanza kuingia Motoni watakuwa wapagani (asiyeamini Mungu wala kufuata dini yoyote), wakifuatiwa na wale Mayahudi na Wakristo walioiharibu dini ya kweli ya mitume wao.[7] Wengine watakokotwa Motoni, wengine wataanguka humo, wakinyakuliwa kwa kulabu.[8] Wakati huo, kafiri atatamani lau angeligeuzwa kuwa udongo, badala ya kuvuna matunda machungu ya matendo yake maovu.
"Hakika tumekuhadharisheni adhabu iliyo karibu kufika; Siku ambayo mtu atakapoona yaliyotangulizwa na mikono yake; na kafiri atasema: ‘Laiti ningelikuwa udongo!’" (Kurani 78:40)
Ongeza maoni