Nafasi Yetu Ndogo Katika Uumbaji wa Mungu
Maelezo: Uumbaji wa kustaajabisha wa Mungu hutunyenyekeza na kutulazimisha Kumtambua na Kumsifu.
- Na islamtoday.net
- Iliyochapishwa mnamo 07 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 2,651 (wastani wa kila siku: 2)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Wakati fulani watu hujiona kuwa wa maana sana, wakitazama kwa dharau kutoka upande hadi upande, wakiwa wameshikilia pua zao juu hewani. Lakini iwapo watatilia tu maanani viumbe vinavyowazunguka na ambavyo ni bora na vinavyopendeza, ingewapa hisia ya unyenyekevu na wangenyenyekea mbele ya Mola wao.
Mambo ya Kuzingatia
1. Wakati wa kutungwa mimba, kati ya seli za mbegu milioni tano hadi milioni mia sita hupitia njia ya uke, kila moja ikiwa na uwezo wa kurutubisha yai na kuwa binadamu. Lakini Mungu katika hekima yake anachagua moja kati ya mamilioni hayo ili kurutubisha yai, na huyu atakua na kuwa mwanadamu aliyeumbwa kikamilifu ambaye Mungu amechagua kumuumba, kiumbe ambacho kwa neema ya Mungu kina uwezo wa kufikiri na kutoa mambo yake.
Hivi ndivyo sisi sote tulivyoumbwa, kwa hivyo tunapaswa kuhisi unyenyekevu kwa kutambua ukuu na ukubwa wa Mola wetu. Tunapaswa kukumbuka mwanzo wetu wa unyenyekevu ili tuweze kufahamu tofauti kubwa kati ya tone hilo dogo la mchanganyiko wa majimaji uliotungwa mimba na wanadamu walioumbwa kikamilifu tulionao leo. Hili lapasa kutulazimisha kumtukuza Mungu, kubaki kumjua Yeye nyakati zote, na kumshukuru.
2. Kuna seli zaidi ya trilioni mia moja katika mwili wa mwanadamu. Ndani ya kila seli hizi kuna viungo, mifumo, michakato migumu, na hifadhi kubwa ya taarifa. Kila moja na kila undani wa seli humtukuza Mola wake huku ikitekeleza jukumu lake katika seli kwa namna ya kuigwa.
Kiini cha kila seli kina takriban nyukleotidi bilioni 31 - "herufi" nne za molekyuli kwenye molekyuli ya DNA ambazo hutaja sifa za maumbile ya kiumbe hai na kudhibiti utendaji kazi wake. Ni taarifa hii ambayo kiumbe hurithi kutoka kwa baba na mama yake.
Idadi hii kubwa ya "herufi" za molekyuli zinazounda DNA yetu zimenakiliwa katika kila seli moja kati ya trilioni mia moja za miili yetu. Kila moja ya herufi hizi inathibitisha ukuu wa Mungu aliyeziumba.
3. Tunapotazama angani usiku, tunatazama mbali katika anga kubwa na mabilioni ya galaksi zilizo juu ya vichwa vyetu. Kila galaksi kwa upande wake ni msongamano wa mabilioni ya nyota, na nyota hizi zote ziko katika hatua mbalimbali katika mizunguko yao. Baadhi ziko katika harakati za kuundwa. Nyingine bado changa, nyingine zimekomaa, huku nyingine zikiwa katika lindi la kifo. Kila moja ya nyota hizi humtukuza Mungu katika anga ambayo ukubwa wake unashangaza akili. Mungu pekee ndiye anayejua ukubwa kamili wa ulimwengu. Tukiwazia meli ya angani yenye uwezo wa kusafiri kwa mwendo kasi wa mwanga, maili elfu 186 kwa sekunde, ingechukua maelfu ya miaka kwa chombo hicho kuvuka galaksi moja, achilia mbali kile kilicho mbele yake.
Mungu anasema:
"Basi naapa kwa mnavyo viona, Na msivyo viona." (Kurani 69:38-39)
Pia Mungu anasema:
"Basi naapa kwa maanguko ya nyota, Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua!." (Kurani 56:75-76)
Galaksi inaweza kuwa na nyota kuanzia milioni 100 hadi bilioni, na kila siku wanasayansi wanavumbua jambo jipya kuhusu anga za juu. Njia za uchunguzi zinazopatikana kwa sasa kwa sayansi bado ni ndogo sana. Sisi, kama viumbe vilivyoumbwa, tunapaswa kuona ukuu wa Mungu katika uumbaji wake na tujionee kwa unyenyekevu.
Ulimwengu wa asili ni kitabu kilichofunguliwa ambacho kinatukuza sifa za Mungu.
"Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake." (Kurani 17:44)
Pia Mungu anasema:
"Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.." (Kurani 22:18)
Uzuri na fahari zote za ulimwengu tunazoweza kuona ni mwonekano mdogo tu wa werevu wa Muumba..
Muumini anapotafakari uumbaji wa Mungu, inafichua jambo fulani la ukuu wa Mungu na hekimaYake kuu. Huleta amani kwa moyo unaoamini na kuimarisha imani ya muumini.
Mungu anasema:
"Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili. – Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa Mbingu na Ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto." (Kurani 3:190-191)
Ongeza maoni