Kristin, Mkatoliki wa Zamani, Marekani (sehemu ya 2 kati ya 2)
Maelezo: Baada ya kujua kuhusu Uislamu katika chumba cha mazungumzo mtandaoni, Kristin anajikuta akilia huku akisoma Qurani katika maktaba huku akitafiti dini.
- Na Kristin
- Iliyochapishwa mnamo 17 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,039 (wastani wa kila siku: 4)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Katika hatua hii nilikuwa nimechanganyikiwa kama nilivyokuwa hapo awali nilipoanza utafiti wangu. Nilihisi kutupa mikono yangu kwa Mungu na kupiga kelele, “Nifanye nini sasa?” Sikuwa Myahudi, sikuwa Mkristo; nilikuwa tu mtu aliyemwamini Mungu mmoja. Nilifikiria kuacha kabisa dini zilizopangika. Nilitaka tu ukweli, sikujali umetoka kwa kitabu kipi kitakatifu; Niliutaka ukweli tu.
Siku moja nilikuwa nikisoma kwenye mtandao na nikaamua kuchukua mapumziko na kuingia katika chumba cha mazungumzo kwenye mtandao. Niliona chumba cha “mazungumzo ya dini”, ambayo bila shaka nilikuwa nakitaka, kwa hivyo nilikifungua. Niliona chumba kinachoitwa “Mazungumzo ya Kiislamu”. Niingie? Nilikuwa natumai hakukuwa na magaidi ambao wangeweza kupata barua pepe yangu na kunituma virusi vya kompyuta - au mbaya zaidi. Picha za majitu waliokuwa wamevaa nguo nyeusi na wenye ndevu kubwa wakija mlangoni na kuniteka nyara zilinijia akilini. (Unaweza kusema nilikuwa na taarifa ya kiasi gani kuhusu Uislamu - sufuri!) Lakini nikajiambia, huu ni uchunguzi tu usio na hatia. Niliamua kuingia na kugundua kwamba watu katika chumba hiki hawakuwa wa kutisha kama nilivyofikiri wangekuwa. Kwa kweli, wengi wao waliitana “ndugu” au “dada” hata kama walikuwa wamekutana hapo tu! Niliwasalimia wote na kuwaambia wanieleze kuhusu misingi ya Uislamu - ambayo sikujua chochote kuihusu. Walichokuwa wakisema kilikuwa cha kuvutia na kiliafikiana na kile nilichoamini tayari. Baadhi ya watu walijitolea wanitumie vitabu na kwa hivyo nikasema sawa. (Aidha, sijawahi kupata virusi vyovyote na hakuna wanaume waliokuja mlangoni mwangu kunichukua, isipokuwa mume wangu lakini nilikwenda kwa hiari!)
Nilipotoka kwenye gumzo, Nilikwenda moja kwa moja kwa maktaba na kuangalia kila kitabu kilichohusu Uislamu, kama nilivyofanya na Uyahudi. Sasa nilikuwa na nia ya kusoma na kujifunza zaidi. Kabla ya hata kuweza kupeleka mzigo mkubwa wa vitabu nyumbani, nilitaka kuangalia ndani ya baadhi ya vitabu hivyo. Hii ilikuwa ni hatua muhimu sana kwangu... Vichache vya kwanza nilivyovioangalia vilielezea misingi kwa undani zaidi, vingine vilikuwa vya wasomi na baadhi vilikuwa na picha za misikiti nzuri sana na wanawake wenye mitandio. Kwa bahati nzuri nilipitia pia Qur'ani... niliifungua tu kokote na kuanza kusoma. Lugha ndio ilinivutia mwanzo, nilihisi kana kwamba ninaongeleshwa na mwenye mamlaka juu yangu, si mwanadamu anayezungumza kama nilivyopata katika maandiko mengine “matakatifu”. Kifungu nilichokisoma (na kwa bahati mbaya sijui ni kipi) kilizungumzia kile ambacho Mungu anatarajia tukifanye katika maisha haya na jinsi ya kuishi kulingana na amri zake. Kilisema kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kurehemu, Mwenye rehema, Mwenye kusamehe. Muhimu zaidi, kwake Yeye ndio kurudi kwetu. Kabla ya kujua, ningeweza kuhisi machozi yakianguka kwa kurasa ambazo nilikuwa nikisoma. Nilikuwa nikilia katikati ya maktaba, kwa sababu hatimaye, baada ya kutafuta kwangu na kuchanganyikiwa kwangu, nimepata nilichokuwa nikitafuta- Uislamu. Nilijua Qurani ilikuwa ni kitu cha kipekee kwa sababu nilikuwa nimesoma maandiko mengi ya kidini, na HAKUNA hata moja ilikuwa wazi hivi au kunipa hisia kama hiyo. Sasa ninaweza kuona hekima ya Mungu... kwa kuniruhusu nichunguze Uyahudi na Ukristo vizuri kabla sijapata Uislamu, hivyo ningeweza kulinganisha zote na kutambua kuwa HAKUNA kitu kinachofanana na Uislamu.
Kuanzia wakati huo niliendelea kutafiti Uislamu. Niliianza kwa kutafuta hitilafu kama nilivyofanya na Uyahudi na Ukristo, lakini hapakuwa na zozote. Nilipitia kwa kina Qur'ani nzima nikitafuta hitilafu yoyote; na hata leo sijaweza kupata hitilafu au utofauti hata MMOJA ndani yake! Kitu kingine kikubwa ninachokipenda kuhusu Qurani ni kuwa inatoa wito kwa msomaji kujiuliza maswali kuihusu. Inasema kujihusu kwamba kama haingetoka kwa Mungu hakika ungepata hitilafu nyingi ndani yake! Sio tu kwamba Uislamu haukuwa na hitilafu, bali pia ulikuwa na jibu kwa swali lolote ambalo ningeweza kufikiria - jibu ambalo lina maana.
Baada ya miezi mitatu, niliamua kuwa Uislamu ndio jibu na kuingia rasmi katika Uislamu kwa kusema Shahadah. Hata hivyo, ilibidi niseme Shahadah yangu kwa simu nikizungumza na imam mmoja kutoka Pennsylvania kwa sababu hapakuwa na Waislamu au misikiti karibu nami (Msikiti wa KARIBU kabisa ulikuwa na umbali wa saa 6). Sijawahi kujuta kuhusu uamuzi wangu wa kuingia katika uislamu. Kwa kuwa hapakuwa na Waislamu wanaoishi karibu nami, nilipaswa kuchukua hatua na kujifunza mengi peke yangu, lakini sijawahi kuchoka nayo kwa sababu nilikuwa nikijifunza ukweli. Kukubali Uislamu kulikuwa kama kuamka kwa roho yangu, akili yangu na hata jinsi nilivyouangalia ulimwengu.
Ninaweza kuilinganisha na mtu ambaye haoni vizuri; anajitahidi kuona na kuelewa kila kitu darasani, hawezi kuwa makini na daima anapitia changamoto kwa sababu ya ulemavu wake. Ukimpa miwani, kila kitu kinakuwa wazi . Hivi ndivyo uzoefu wangu wa Uislamu ulivyo: kama kupokea miwani, ambayo imeniwezesha, kwa mara ya kwanza, kuona ukweli.
Ongeza maoni