Manufaa ya Kusilimu (sehemu ya 2 kati ya 3)
Maelezo: Sababu muhimu za kusilimu bila ya kuchelewa.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,476 (wastani wa kila siku: 4)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Watu wengi ulimwenguni huchukua muda mwingi sana kusoma na kujifunza kuhusu kanuni za Uislamu; hutafiti na kuzipitia tafsiri nyingi za Kurani na kuvutiwa na maisha na nyakati za Mtume Muhammad. Wengine huhitaji tu kujua kwa uchache kuhusu Uislamu na kusilimu mara moja. Ilhali wengine hutambua ukweli lakini hungoja, na kungoja na kuendelea kungoja, wakati mwingine kuhatarisha akhera yao. Tunaendelea na majadiliano yetu kuhusu manufaa, yasiyo wazi wakati mwingine, ya kujiunga na Uislamu.
"Na anakayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri [kupata hasara]." (Kurani 3:85)
5. Kusilimu ni hatua ya kwanza ya kuimarisha uhusiano wa kudumu na Muumba.
Kila mtu katika jamii ya wanadamu huzaliwa akijua kimaumbile kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja. Mtume Muhammad alisema kwamba kila mtoto huzaliwa katika hali ya fitra[1], huku akiwa na uelewa sahihi wa Mwenyezi Mungu.[2] Kulingana na Uislamu hii ndio hali ya asili ya mwanadamu, akiwa na silika ya kujua kwamba kuna Muumba, na kimaumbile akitaka kumuabudu na kumridhisha Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, wale wasiomjua Mungu ama wasioimarisha uhusiano na Mungu wanaweza kutatanishwa na uwepo wa mwanadamu na wakati mwingine kufadhaishwa. Kwa wale wengi, ambao humruhusu Mwenyezi Mungu kwenye maisha yao na kumuabudu Yeye kwa njia inayomridhisha, huleta maana mpya kabisa kwa maisha.
"...Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua." (Kurani 13:28)
Kupitia matendo ya ibada kama vile sala na dua, mtu huanza kuhisi ukaribu wa Mwenyezi Mungu, kupitia kwa elimu na hekima yake isiyo na kikomo. Muumini huwa salama kwa kuelewa kwamba Mwenyezi Mungu, aliye Mkuu wa Vyote, yuko juu ya mbingu, na kufarijika na uhakika kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja nao katika mambo yao yote. Muislamu kamwe hayuko peke yake.
"...Anayajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo. Naye yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote mnayoyatenda." (Kurani 57:4)
6. Kusilimu hudhihirisha rehema za Mungu na msamaha wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake.
Kama wanadamu wanyonge aghlabu tunajihisi tumepotea na tukiwa peke yetu. Kisha tunarudi kwa Mwenyezi Mungu na kuomba Huruma na Msamaha Wake. Tunaporudi kwa Mwenyezi Mungu tukijisalimisha kwake kwa dhati ya mioyo yetu, utulivu wa Mungu hutushukia. Kisha tunaweza kuhisi ubora wa huruma Yake na kuiona huruma hiyo ikidhihirika ulimwenguni. Hata hivyo, ili kumuabudu Mwenyezi Mungu, tunapaswa kumfahamu. Kwa kusilimu, milango ya kumfahamu Mungu hufunguka, ikiwemo ukweli kwamba Msamaha wa Mwenyezi Mungu hauna mipaka.
Watu wengi huchanganyikiwa ama kuaibishwa na madhambi mengi waliyotenda katika kipindi cha maisha yao. Kujiunga na Uislamu hufuta kabisa madhambi yote hayo; yakawa kana kwamba hayakuwahi kufanyika kabisa. Muislamu mgeni huwa safi kama mtoto mchanga aliyezaliwa.
"Waambie wale waliokufuru [kwamba] wakikoma, watasamehewa yaliyokwishapita. Lakini wakiyarudia, basi imekwishapita mifano ya [waasi] wa zamani." (Kurani 8:38)
Ikiwa baada ya kujiunga na Uislamu mtu atatenda madhambi zaidi, mlango wa msamaha bado huwa wazi kabisa.
"Enyi mlioamini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni madhambi [maovu] yenu, na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati [chini] yake..." (Kurani 66:8)
7. Kujiunga na Uislamu hutufunza kwamba majaribio na mitihani ni sehemu ya hali ya maisha ya mwanadamu.
Pindi mtu anapojiunga na Uislamu huanza kuelewa kwamba majaribio, masaibu, na ushindi katika maisha haya sio matukio nasibu ya ulimwengu katili usio na mpangilio. Muumini wa kweli huelewa kwamba uwepo wetu ni sehemu tu ya ulimwengu uliopangika vyema, na maisha huendelea kwa namna aliyoipanga Mwenyezi Mungu, kwa hekima Yake isiyo na kikomo.
Mwenyezi Mungu anatuambia kwamba tutafanyiwa majaribio, na Allah anatushauri kuyavumilia majaribio na masaibu hayo. Hili sio rahisi kulielewa mpaka mtu anapokubali kuwa kuna Mungu mmoja, dini ya Uislamu, ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia miongozo dhahiri kuhusu jinsi tunavyopaswa kufanya tutakapokabiliwa na majaribio na masaibu. Tukiifuata miongozo hii, iliyomo kwenye Kurani na mwenendo sahihi wa Mtume Muhammad, basi itawezekana kuyavumilia madhila kwa urahisi na hata kuwa mwenye shukurani.
"Hapana shaka Tutakujaribuni kwa chembe ya hofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri." (Kurani 2:155)
Mtume Muhammad alisema, “Mtu atapimwa kulingana na kiwango cha kujitolea kwake katika dini, na majaribio yataendelea kumuathiri muumini mpaka atakapoachwa akitembea duniani bila dhambi yoyote kabisa".[3]Muislamu anafahamu kwa hakika kwamba dunia hii, maisha haya, ni mapito ya muda mfupi tu, ni kituo katika safari ya maisha yetu ya milele ima kwenye Jehanamu ama Peponi. Kwa kukutana na Muumba bila ya mzigo wowote wa dhambi, hilo ni jambo zuri sana, bila shaka linaloambatana na ushindi wa majaribio yanayotufika.
Katika makala ifuatayo, tutakamilisha majadiliano haya kwa kutaja kwamba Uislamu ni njia ya maisha. Uislamu hufafanua wazi haki, wajibu na majukumu tuliyonayo kwa wanadamu wengine, na matunzo yetu kwa wanyama na mazingira. Uislamu una majibu ya maswali yote makubwa na madogo ya maisha yetu.
Ongeza maoni