Jinsi ya Kusilimu na kuwa Muislamu
Maelezo: Kusilimu ni wepesi. Nakala hii inaelezea jinsi ya kusilimu kwa njia rahisi. Isitoshe, inatoa muhtasari wa Uislamu, imani ya watu bilioni 1.7, na inaangazia faida za kusilimu.
- Na IslamReligion.com Team
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 10
- Imetazamwa: 12,009 (wastani wa kila siku: 11)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Usaidizi wa Moja kwa Moja kupitia Maongezi
Uislamu na Waislamu
Neno la Kiarabu 'Islam' linamaanisha 'kujisalimisha', na limetokana na neno linalomaanisha 'amani'. Kwa hivyo, dini ya Uislamu inafundisha kwamba ili kupata amani halisi ya kifikra na utulivu wa moyo, ni lazima mtu ajisalimishe kwa Mwenyezi Mungu na kuishi kulingana na Sheria Yake Tukufu iliyoteremshwa kwa wanadamu kupitia mitume.
Uislamu sio dini mpya kwa sababu 'kujisalimisha ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu', yaani Uislamu, kwa kawaida umekuwa ndiyo dini pekee inayokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hii, Uislamu ni 'dini halisi' na ya kweli, na ni ujumbe ule ule wa milele uliofunuliwa kwa nyakati zote kwa mitume na wajumbe wote wa Mwenyezi Mungu. Ujumbe mkuu wa mitume wote umekuwa ni kwamba kuna Mungu Mmoja tu wa Kweli na Yeye pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa. Mitume hawa huanzia Adam pamoja na Nuhu, Ibrahim, Musa, Daudi, Sulemani, Yohana Mbatizaji, na Yesu, amani iwe juu yao wote. Mungu anasema katika Kurani Tukufu:
“Na hatukumtuma kabla yako (Ewe Muhammad) Mtume yeyote ila tulimfunulia (ya kwamba): ‘hapana mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.’” (Kurani 21:25)
Hata hivyo, ujumbe wa kweli wa mitume hawa ulipotea ama ulipotoshwa kwa muda. Hata vitabu vya hivi karibuni, Taurati na Injili vilighushiwa na kwa hivyo vilipoteza uaminifu wao wa kuwaongoza watu kwenye njia ya haki. Kwa hivyo, miaka 600 baada ya Mtume Yesu, Mwenyezi Mungu aliufufua ujumbe uliopotea wa mitume waliopita kwa kumtuma Mtume Muhammad na ufunuo wake wa mwisho, Kurani Tukufu, kwa wanadamu wote. Kwa kuwa Mtume Muhammad alikuwa mtume wa mwisho, Mwenyezi Mungu Mwenyewe aliahidi kuyahifadhi maneno Yake ya mwisho yaliyofunuliwa ili yawe chanzo cha mwongozo kwa wanadamu wote hadi Siku ya Mwisho. Sasa ni muhimu kwa kila mtu kuamini na kufuata ujumbe huu wa mwisho kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Muweza anasema katika Kurani:
“Na hatukukutuma (Ewe Muhammad) ila kwa watu wote uwe m'bashiri, na mwonyaji lakini watu wengi hawajui.” (Kurani 34:28)
“Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitakubaliwa kwake, naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri (miongoni mwa waliopata hasara).” (Kurani 3:85)
Neno "Muislamu" linamaanisha mtu anayejisalimisha kwa matakwa au mapenzi ya Mwenyezi Mungu, bila kujali asili yake, utaifa wake au kabila lake. Kwa hivyo, mtu yeyote ambaye yuko tayari kujisalimisha kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu anastahiki kuwa Muislamu.
Faida za Kusilimu
Kuna faida nyingi za kusilimu. Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:
• Mtu hujijengea uhusiano wa kibinafsi na wa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu kwa kumwabudu Yeye peke yake, bila kuhitaji wasta (mtu wa kati au kitu cha kati kufikia Mungu). Mtu huhisi kuwa na uhusiano huu wa kibinafsi na hufahamu kuwa Mungu anajua kila kitu na yupo ili kumsaidia.
• Mtu hutambua azma ya ukweli wa maisha yake, ambayo ni kumtambua Mwenyezi Mungu na kufuata amri Zake.
• Mtu hupewa nuru, ambayo humwongoza katika maisha yake. Dini ya Uislamu ina majibu ya hali zote, na mtu atajua kila mara hatua sahihi za kuchukua katika nyanja zote za maisha.
• Mtu hupata furaha ya kweli, utulivu, na amani ya ndani kwa ndani.
• Baada ya kusilimu, madhambi yake yote ya zamani husamehewa, na mtu huanza maisha mapya ya uchaji Mungu na uadilifu. Na kama Muislamu, anapokosea baadaye, anaweza kutubu kwa Mungu ambaye husamehe madhambi ya wale wanaotubu kwake kwa dhati. Hakuna wasta au viumbe wa kuwaendea kukiri makosa yao kupitia wao.
• Mtu anaokoka na Moto wa Jehanamu, ambao mitume wote wameonya juu yake.
• Faida kubwa zaidi ni kwamba Muislamu ameahidiwa na Mwenyezi Mungu thawabu ya milele ya Peponi (Mbinguni). Wale ambao wamebarikiwa kupata Pepo, wataishi milele katika neema bila aina yoyote ya maradhi, maumivu ama huzuni. Mwenyezi Mungu atawaridhia na wao watamridhia yeye. Hata walio katika daraja la chini kabisa miongoni mwa wakaazi wa Peponi watapata mara kumi ya yale yaliyo katika ulimwengu huu, na watapata kila wanalolitamani. Kwa kweli, katika Pepo kuna starehe ambazo hakuna jicho limewahi kuona, hakuna sikio limewahi kusikia, na hakuna akili limewahi kuwazia. Yatakuwa maisha ya kweli kabisa, sio ya kiroho tu, bali ya kimwili pia.
Ili kujua zaidi juu ya faida nyingine za kusilimu, unaweza kusoma makala hii “Faida za Kusilimu (sehemu 3)”.
Jinsi ya Kusilimu - Ushuhuda wa Imani (Shahada)
Mchakato wa kuwa Muislamu ni sahili na rahisi. Yote ambayo mtu anapaswa kufanya ni kupiga Shahada kwa kutamkwa hivi:
Nakiri “Laa ilaaha illa llah, Muhammadan rasuulu llah.”
Maneno haya ya Kiarabu yanamaanisha, "Hapana Mola (Mungu) wa kweli isipokuwa Allah (Mwenyezi Mungu), na Muhammad ni Mtume (Mjumbe) wa Mwenyezi Mungu." Mara tu mtu anapotamka Shahada kwa kuamini na kuelewa maana yake, basi amekuwa Muislamu.
Sehemu ya kwanza ya Shahada, "Hapana Mola wa kweli isipokuwa Mwenyezi Mungu," inamaanisha kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu hana mshirika wala hana mwana. Sehemu ya pili ya Shahada inamaanisha kuwa Muhammad alikuwa Mtume wa kweli aliyetumwa na Mungu kwa wanadamu wote.
Ili uwe Muislamu, mtu anapaswa pia:
- Kuamini ya kwamba Kurani Tukufu ni neno halisi la Mungu, lililoteremshwa na Yeye.
- Kuamini ya kwamba Siku ya Hukumu (Siku ya Ufufuo) ni kweli na inakuja.
- Kuamini mitume wa Mwenyezi Mungu waliotumwa na vitabu vilivyopelekwa kwa mitume, na malaika Wake.
- Kukubali Uislamu ni dini yake.
- Kutoabudu kitu chochote wala mtu yeyote ila Mwenyezi Mungu.
Ni rahisi sana! Kusikia Shahada, bofya bonyeza hapa ama bofya “Msaada wa Moja kwa Moja” kwa usaidizi wa papo hapo kupitia kwa gumzo.
Hatua ya kupiga shahada inaweza kufanywa na mtu peke yake, lakini ni vyema zaidi inapofanywa kupitia usaidizi wa mmoja wa washauri wetu au kupitia "Msaada wa Moja kwa Moja", kwa hivyo, tunaweza kukusaidia kuitamka shahada hiyo kwa njia iliyo sahihi na kukupa habari nyingine muhimu na ushauri ambao umeandaliwa, hasa kwa wale wageni waliosilimu, ili waweze kuanza na imani yao mpya.
Vinginevyo, tunaweza kukupigia simu ili kukusaidia na mchakato wa kusilimu. Kupitia njia hii, tafadhali tuachie nambari yako ya simu na wakati unaofaa wa kukupigia simu kwa kujaza fomu yetu ya Wasiliana Nasi.
Hauko Peke Yako
Ikiwa umefuata mwongozo wa kusilimu uliopo hapo juu na ukasilimu binafsi, basi usiwe na wasiwasi wa kuwa uko peke yako, badala yake tambua kuwa dini hii imeshirikisha watu bilioni 1.7. Tunapendekeza sana utufahamishe kupitia kwa fomu ya Wasiliana Nasi ama kupitia “Msaada wa Moja kwa Moja”, ili tuweze kukupa nyenzo muhimu na ushauri unaokufaa kama Muislamu mgeni.
Tunakupongeza kwa uamuzi wako, tunakukaribisha kwenye Uislam, na tutajitahidi kukusaidia kwa njia yoyote tutakayoweza! :)
Baadhi ya Dhana Potofu za Kawaida
Watu wengine wanaweza kuahirisha hatua yao ya kusilimu, ijapokuwa wanaamini kuwa hiyo ndiyo dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu, kutokana na dhana potofu. Wanaweza kufikiria mambo kama vile kubadilisha majina yao, kujua Kiarabu, kuwajulisha wengine kuhusu kusilimu kwao, kujuana na kutangamana na Waislamu wengine, au kutofanya madhambi mengi, kuwa ni masharti ya kujiunga na Uislamu – hata hivyo, ukweli ni kwamba hakuna hata mojawapo ni visingizio halali vinavyoweza kumchelewesha mtu kujiunga na Uislamu.
Iwapo ungependa kujifunza zaidi kuhusu hizi na dhana nyingine potofu kama hizi, tafadhali soma makala hii, "Nataka kuwa Muislamu lakini ... Uzushi kuhusu Kusilimu (sehemu 3)".
Kwa Wale Ambao Hawajashawishika
Uislamu unadai kuwa ndiyo njia ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Kinachofanya dini moja iwe halali kuliko itikadi nyingine ni ushahidi unaotoa wa ukweli wake. Kwa hivyo, mtu anahitaji kuangalia uthibitisho huu, kuupima na kuchukua uamuzi sahihi wa kielimu. Mtu anahitaji kuwa mwaminifu katika jitihada yake pamoja na kutafuta msaada wa Mwenyezi ili amwongoze katika njia ya haki.
Iwapo mtu hajashawishika kuhusu ukweli wa Uislamu, basi anaweza kuangalia zaidi ushahidi ambao Uislamu unatoa. Uislamu unatoa uthibitisho mkubwa sana wa ukweli wake na ndiyo dini pekee inayovutia maarifa ya kawaida.
Baadhi ya ushahidi ambao Uislamu unatoa ni pamoja na: uthibitisho wa kisayansi katika Kurani, miujiza iliyofanywa na Mtume Muhammad na utabiri wa kuja kwake katika maandiko yaliyotangulia, matukio yaliyotabiriwa na yaliyotajwa katika Kurani ambayo baadaye yalitokea, changamoto isiyotekelezeka ya Kurani ya kuleta hata sura moja kama hiyo, na hekima za Mungu katika sheria na mafundisho ya Uislamu ambazo zinashughulikia nyanja zote za kimaisha. Ili kujifunza zaidi kuhusu uthibitisho wa Uislamu, tafadhali angalia makala iliyo katika sehemu hii, “Ushahidi kuwa Uislamu ni Ukweli”.
Iwapo ungependa kujifunza zaidi kuhusu Uislamu na nguzo zake za imani na utekelezaji wake, basi tafadhali rejelea makala hii “Ni nini Uislamu? (sehemu 4 )”.
Maisha yetu ya milele katika Akhera hutegemea imani tunayochagua kufuata katika maisha haya yasiodumu, kwa hivyo tuyape mapambano haya kipaumbele yanayostahiki.
Ongeza maoni