Uadilifu wa Hukumu
Maelezo: Muhtasari wa kiangazio cha swali la kwa nini kuna Siku ya Hukumu, na nini mwisho wa dini zisizokuwa Uislamu.
- Na Laurence B. Brown, MD
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 2,963 (wastani wa kila siku: 3)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
“Huwezi kupata fursa ya pili ya kuwafanya watu kuwa na dhana nzuri kwako”
--methali ya zamani
Imani ya kweli ina malipo ya Akhera. Kutoamini kuna malipo pia, laaaakini ... huyataki. Huu umekuwa ujumbe wa mitume wote—wa kila mmoja wao.
Tunawezaje kuthibitisha maisha ya baada ya kifo yapo? Naam, ni wapi pengine ambapo dhuluma za maisha haya zinaweza kurekebishwa, ikiwa si katika maisha ya baada ya kifo? Kile tunachokiona kuwa ni dhuluma katika maisha ya dunia hii kitakuwa ni tafakuri mbaya juu ya uadilifu wa Mungu, ikiwa "dhuluma" hizi hazitafutiliwa mbali na malipo na adhabu mwafaka huko Akhera. Baadhi ya watu waovu sana hufurahia maisha ya anasa zaidi. Wakati huo huo, baadhi ya watu bora zaidi huteseka mno. Kwa mfano, ni mtume gani aliyekuwa na wakati mwepesi? Ni mitume gani waliishi maisha ya starehe ya kufana yanayolingana na yale ya bosi wa mafia, muuza dawa za kulevya au mtawala dhalimu, wa wakati wetu au wao? Iwapo tutategemea rehema na uadilifu wa Muumba wetu, hatuwezi kuamini kwamba Yeye ameweka thawabu za uchaji Mungu na adhabu za uvunjaji sheria ziwe katika maisha ya dunia hii tu, ilhali ukosefu wa usawa na haki hapa duniani uko wazi.
Kwa hivyo, kutakuwa na Siku ya Hukumu, ambayo sote tutakuwepo, na utakuwa wakati mbaya kuanza kufikiria kubadilisha maisha yetu kuwa bora. Kwa sababu ... sasa nisikilize kwa makini ... kwa sababu maisha yetu yataisha, kwa neno moja. Tutakuwa tumechelewa. Rekodi ya matendo yetu itakuwa imekamilika na kufungwa. Na hakuna kurudi nyuma.
Wanadamu watapangwa kulingana na imani na matendo. Waaminifu watathibitika, makafiri watalaaniwa, wakiukaji mipaka (kama hawatasamehewa) wataadhibiwa kulingana na uzito wa madhambi yao.
Mayahudi hutangaza kuwa pepo ni haki ya kuzaliwa ya “watu waliochaguliwa,” Wakristo hudai “si kuwa wakamilifu, waliosamehewa tu,” na Waislamu huamini kwamba wote wanaokufa kwa kujisalimisha kwa Muumba wanastahiki ukombozi. Wale waliofuata wahyi na Mtume wa zama zao watafaulu, ilhali wale waliokataa wahyi na Mtume wa siku zao walifanya hivyo wakiuza nafsi zao.
Kulingana na Uislamu, Mayahudi walioamini walikuwa juu ya ukweli hadi walipokataa mitume waliokuja baadaye (yaani, Yahya au Yohana Mbatizaji na Issa au Yesu Kristo), mafundisho yao na, kwa upande wa Yesu, wahyi alioufikisha. Kwa namna hii, Mayahudi waliishi wakimtii Mungu sio kwa masharti Yake, bali kwa masharti yao. Mungu alipotuma mitume au wahyi ambao hawakuupenda, walichagua kubaki katika dini ya mababu zao badala ya dini ya Mungu. Kwa namna hii, waliasi na kukufuru.
Vilevile, wafuasi wa Yesu walikuwa juu ya ukweli, hadi pale walipomkataa mtume wa mwisho (yaani, Muhammad). Isitoshe, wafuasi wa Yesu walijisalimisha kwa Mungu, lakini kwa masharti yao tu. Na hiyo haitoshi. Walipoitwa kuheshimu (kwa kukubali na kufuata) ufunuo wa mwisho (yaani, Kurani) pamoja na Mtume aliyeifikisha (yaani, Muhammad), walikataa na kutumbukia katika uasi na ukafiri ule ule kama wa binamu zao wa Kiyahudi.
Kwa mujibu wa Waislamu, dini ya ukweli daima imekuwa Uislamu (yaani, kujisalimisha kwa matakwa ya Mungu), kwani hivyo ndivyo mitume wote walivyofundisha. Lakini, uboreshaji wa ujumbe wa Uislamuunapatikana katika ufunuo wa mwisho na katika mafundisho ya mtume wa mwisho. Katika kufunua wahyi wa mwisho, Mwenyezi Mungu alifuta dini zote zilizotangulia pamoja na wahyi wa awali. Kwa hivyo, kundi pekee linalojisalimisha kwa dini ya Mwenyezi Mungu siku hizi ni la Waislamu. Wale wanaoujua Uislamu, na wakaukataa, watalaumiwa. Wale wanaoujua Uislamu na wakakwepa kimakusudi jukumu la kuisoma dini hiyo pia watashutumiwa. Hata hivyo, wale wanaokufa bila kuujua Uislamu au kwa kukusudia kuepuka kuuchunguza, watajaribiwa Siku ya Kiyama, ili kuthibitisha wangefanya nini, lau wangelijua. Na kwa msingi huo, Mungu atawahukumu.
Kwa namna hii, kama inaweza kudhaniwa kwamba kuna Mayahudi waliokufa bila ya kuwajua mitume waliokuja baadaye, na Wakristo waliokufa bila kumjua Muhammad na Kurani Tukufu, basi hao sio wa kulaumiwa. Bali, Mwenyezi Mungu atawahukumu kulingana na kujisalimisha kwao kwa kufuata wahyi uliofunuliwa kwao wakati wa maisha yao, na atajaribu imani zao na utii wao. Vivyo hivyo, itakuwa kwa wale wanaokufa bila kujua wahyi wowote. Kwa hivyo, watu wasiojua ambao hufa huku wakitafuta dini ya kweli kwa dhati wana matumaini ya wokovu, ilhali wasio wanyoofu hawana matumaini hayo, hata wakiwa wameelimika namna gani.
Hakimiliki © 2007 Laurence B. Brown; imetumika kwa ruhusa.
Dondoo hilo hapo juu limechukuliwa kutoka kitabu kijacho cha Dkt. Brown, God’ed, ambacho kinatarajiwa kuchapishwa pamoja na mwendelezo wake, MisGod’ed. Vitabu vyote viwili vinaweza kutazamwa kwenye tovuti ya Dkt. Brown, www.LevelTruth.com. Unaweza kuwasiliana na Dr. Brown kupitia baruapepe ya: BrownL38@yahoo.com
Ongeza maoni