Mazungumzo katika Pepo na Jahannam (sehemu ya 1 kati ya 3): Kuzungumza na Malaika
Maelezo: Wenzetu wa daima watakachotuambia tunapoingia katika makao yetu ya milele.
- Na Aisha Stacey (© 2012 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 11 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 25 Jul 2022
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 6,544
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Tunaanza na mfululizo mpya wa makala kuhusu mazungumzo yanayotokea Peponi na Jahannamu. Tunatazamia kuwa, kwa kukumbushana tuliyo ambiwa kuhusu Pepo na Jahannamu, tutaweza kuona na kufikiria matukio yatakayofanyika tutakapo kutana na makao yetu ya milele katika Akhera. Kwa nini Mungu anatuambia kuhusu mazungumzo haya?
Kwa nini Mungu anatuambia kuhusu mazungumzo haya? Qur'ani imejaa sio tu maelezo ya Bustani za Mbinguni na Jahannamu, lakini pia mazungumzo, majadiliano na malumbano ya kimantiki. Matukio kama hayo yanaporudiwa tena na tena ni dalili kwamba Mungu anasema, “kuweni makini!” Kwa hivyo inatupasa kufanya hivyo tu, tutafakari vizuri kwa matumaini ya kuingia makao ya neema yanayojulikana kama Pepo, au tujilinde na Moto wa Jahannamu. Habari hurudiwa tena na tena ili kutufanya tufikirie vizuri kwa muda mrefu.
Katika makala zifuatazo tutaangalia aina kadhaa za mazungumzo. Mazungumzo baina ya Malaika na watu wa Peponi, na watu wa Jahannamu, na mazungumzo baina ya watu wa Peponi na wa Jahannamu na familia zao, na mazungumzo ya Mwenyezi Mungu na watu wa Pepo na wa Jahannamu. Mbali na hayo tutaangalia pia yale wanayo sema watu wa peponi na wa Jahannamu baina yao, kati yao wenyewe na majadiliano yao ya ndani. Tuanze na mazungumzo baina ya Malaika na watu wa Akhera.
Mazungumzo na Malaika
Malaika hukaa nasi tangu mwanzo wa maisha yetu hadi mwisho. Wana wajibu wa kupumua roho kwa mtoto mchanga akiwa tumboni, wanaandika matendo yetu mema na mabaya na hutoa roho kutoka miili yetu wakati wa kufa. Tunapoingia makao yetu ya milele, maisha yetu ya baadaye, wako pamoja nasi na tutaweza kuzungumza nao.
Watu wa Mabustani Za Mbinguni
Makao ya milele ya wale ambao wameishi maisha yao kwa subira katika nyakati za dhiki, na wakajitahidi kuwa wema kwa nyakati za shida na wema, ni Bustani za Mbinguni za milele zinazojulikana kama Jannah. Na watakapo ingia na kuishi milele kwenye nyumba zao mpya katika Bustani za Mbinguni, Malaika watawasalimu. Hao ndio mabawabu wa Peponi, na watasema: 'Ingieni kwa amani kwa sababu ya kusubiri kwenu!' Bustani za Mbinguni ni pahali pa utulivu wa milele na radhi za kudumu.
Na walio mcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea Peponi kwa makundi, mpaka watakapo fikilia, nayo milango yake imekwisha funguliwa. Walinzi wake watawaambia: Salaam Alaikum, Amani iwe juu yenu! Mmet'ahirika. Basi ingieni humu mkae milele.” (Kurani 39:73)
Hisia zote za maumivu zitaondolewa kwenye nyoyo zao. Watawaitikia malaika kwa kumsifu Mwenyezi Mungu, na mazungumzo yanaendelea.
“… Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuhidi kufikia haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakutuhidi. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. Na watanadiwa kwamba: Hiyo ndiyo Pepo mliyo rithishwa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyafanya.” (Kurani 7:43)
Watu wa Motoni
Mazungumzo yatakayofanyika baina ya watu wa Jahannamu na Malaika yatakuwa tofauti kabisa. Wakaazi wa Jahannamu watakuwa na hali tofauti kabisa. Badala ya kusubiri kwa shauku kuingia katika makaazi yao ya milele, watu wa Jahannam watalazimishwa na kuvutwa na Malaika wasimamizi wa Moto. Na watakapotupwa motoni, Malaika watasema: “Je! Hakukujieni mwonyaji?“
Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji? Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa! Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni!” (Kurani 67:8-10)
Hata hivyo hii si mara ya kwanza wakazi hawa wa moto walifanya mazungumzo na malaika. Malaika wa mauti na wasaidizi wake wanapo kusanyika ili waondoe nafsi za watu hawa, watawauliza wako wapi mlio waabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Kwa sababu katika hatua hii ya maisha ya mtu sanamu zake hazitakuwepo.
…mpaka watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha, watawaambia: Wako wapi mlio kuwa mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea! Na watajishuhudia wenyewe kwamba walikuwa makafiri. (Kurani 7:37)
Baada ya muda fulani wakazi wa Jahannamu wanaanza kupoteza matumaini yote. Wamekuwa wakimwomba Mwenyezi Mungu, lakini hawapokei jibu. Hivyo wataanza kuwaomba Malaika ambao ndio mabawabu. Mwombeni Mola wenu Mlezi atupunguzie adhabu yetu. Malaika hujibu kwa maneno ambayo huwakatisha tamaa kabisa.
Na walio Motoni watawaambia walinzi wa Jahannamu: Mwombeni Mola wenu Mlezi atupunguzie walau siku moja ya adhabu. Nao watasema: Je! Hawakuwa wakikufikieni Mitume wenu kwa hoja zilio wazi? Watasema: Kwani? Watasema: Basi ombeni! Na maombi ya makafiri hayawi ila ni kupotea bure.… (Kurani 40:49-50)
Mazungumzo katika Paradiso na Jahannamu (sehemu ya 2 kati ya 3): Malumbano na Majadiliano
Maelezo: Mazungumzo zaidi yatakayo fanyika baina ya watu wa Peponi na watu wa Jahannamu.
- Na Aisha Stacey (© 2012 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 11 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,326
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Malumbano baina ya watu wa Peponi na watu wa Motoni
Malumbano yanayojiri baina ya watu wa Peponi na watu ambao makaazi yao ni Moto wa Jahannamu yanatajwa katika sehemu kadhaa katika Kurani. Tunaposoma na kutafakari juu ya aya hizi tunapaswa kufikiria na kujaribu kujifunza kitu kutokana na kukata tamaa kwa wale wanaokabiliwa na hofu za motoni. Tunapaswa kuhisi hofu yao, na tujifunze kutokana na makosa yao. Kusoma kuhusu wao kwenye Kurani kunatuwezesha kuhisi maumivu yao lakini pia kunatuwezesha kuona jinsi tunavyoweza kuepuka mwisho huo kwa urahisi.
Wataulizana wao kwa wao peponi juu ya wakosefu (washirikina na makafiri): Ni nini kilicho kuleteeni Motoni? Watasema: Sisi hatukuwa miongoni mwa wale walio kuwa wakisali, wala hatukuwalisha mafakiri. Na tulikuwa tukisema kwa maneno ya upotovu, na tulikuwa tukiikanusha Siku ya kiyama, mpaka itufikie hakika ( kifo). (Kurani 74:40 -47)
Na watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni: Sisi tumekuta aliyo tuahidi Mola wetu Mlezi kuwa ni kweli. Je, na nyinyi pia mmekuta aliyo kuahidini Mola wenu Mlezi kuwa ni kweli? Watasema: Ndiyo! Basi mtangazaji atawatangazia: Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu. (Kurani 7:44)
Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi: Tumimieni maji, au chochote alicho kuruzukuni Mwenyezi Mungu. Nao watasema: Hakika Mwenyezi Mungu ameviharimisha hivyo kwa makafiri, (Kurani 7: 50)
Inabainika kuwa mateso ya wakazi wa Jahannamu yatazidi kwa kuona na kusikia neema waliyopewa watu wa Peponi.
Mazungumzo baina ya watu wa Peponi
Maneno ya Mwenyezi Mungu katika Kurani yanatuambia kwamba watu wa Peponi wataulizana juu ya maisha yao ya zamani.
“Nao watafikiana, wakiulizana. Watasema: Tuliogopa kwa ahali zetu, lakini Mwenyezi Mungu ametuhurumia, na akatuokoa na adhabu ya Moto. (Kurani 52:25 -27)
Aya nyingi zinazoelezea mazungumzo miongoni mwa watu wa Peponi zinathibitisha kwamba wataendelea na tabia zao mema kwa kumsifu Mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa neema alizowajalia. Ingawa walikuwa wameamini ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwa ya kweli na hivyo kutenda mema ipasavyo, ufahari na ukubwa wa neema ya Pepo utawafanya wazidi kumshukuru Mola.
Na watasema: Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye tuondolea huzuni zote. Hakika Mola wetu Mlezi bila ya shaka ni Mwenye kusamehe, Mwenye shukrani. Ambaye kwa fadhila yake ametuweka makao ya kukaa daima; humu haitugusi taabu wala humu hakutugusi kuchoka. (Kurani 35:34-35)
Nao watasema: Alhamdulillah, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyetutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao (Kurani 39:74)
Mazungumzo ya Watu wa Jahannamu baina yao
Na watu waliopangiwa kuishi milele katika Moto wa Jahannamu watashtushwa kwa kuwa sanamu au watu waliowaamini na wakawafuata hawawezi kuwasaidia. Na viongozi wanaoitwa 'wenye kiburi' katika Kurani wanaambia wafuasi wao kuwa wao wenyewe walikuwa wamepotea. Basi yeyote aliyewafuata, akawafuata katika maisha yasiyo na rehema.
Watakabiliana wao kwa wao kuulizana. Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia. Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini. Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu. Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu.Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu. (Kurani 37:27-32)
Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia. (Kurani 14:21)
Na likihukumiwa jambo, yaani jambo la ni nani atakaye pelekwa Peponi, na nani atakaye elekezwa Jahannamu, mkaazi wa Jahannamu mwenye sifa mbaya kabisa, Iblisi mwenyewe, atafunua ukweli mkubwa. Ni ukweli ambao Mungu alitufunulia katika Kurani, lakini ambao watu wengi hawakuutilia maanani. Kwamba yeye, Shet'ani, alikuwa mwongo. Ahadi za Shetani hazikutimia kamwe, ahadi zake zilikuwa tupu na yeye mwenyewe alimwamini Mungu.
Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Mwenyezi Mungu alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu. (Kurani 14:22)
Mazungumzo katika Pepo na Jahannamu (sehemu ya 3 kati ya 3): Na sitawahi wakasirikia tena.
Maelezo: Mazungumzo na familia, majadiliano ya ndani na jinsi Mwenyezi Mungu anavyo itika kwa watu wa Akhera.
- Na Aisha Stacey (© 2012 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 11 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 16 Jan 2023
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 3,211
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Majadiliano ya ndani
Itakapo hukumiwa jambo, na watu wa Jahannamu wakaondoka, na watu wa Peponi wakaingia Bustani, kila kundi la watu litaongea kati yao. Maisha yao duniani hayajasahauliwa na makundi yote mawili yana wakati usioisha wa kuangalia nyuma na kuchambua kwa nini - kwa nini ninateseka, au kwa nini nina haki ya kufurahia anasa hii? Hukumu imeshaamuliwa, muda mfupi uliotumika katika maisha ya dunia umekwisha na uzima wa milele umeanza.
Atawauliza Mungu:"Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka? Watasema: "Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanao weka hisabu." Atasema Mungu: "Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua." (Kurani 23:112-114)
Tunajua ya kwamba watu wa Peponi na Jahannamu wataulizana, lakini wataambiana nini, watahisi vipi, unyonge na upweke? Mungu anatuambia kwamba watashusha pumzi, kwa hofu, kwa kuchanganyikiwa. Ni vigumu kwetu kufikiria hilo lakini tunajua kwamba wanaonekana kukata tamaa.
“ Ama wale wa mashakani hao watakuwamo Motoni wakiyayayatika na kukoroma." (Kurani 11:106)
“… Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto unao waka kwa nguvu. Watadumu humo milele na hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungeli mt'ii Mwenyezi Mungu, na tungeli mt'ii Mtume." (Kurani 33:64-66)
Na watu wa Jahannamu wanapotafakari kwa nini wale waliowafuata katika dunia hii hawawezi kuwasaidia katika mateso yao, basi ndani yake kuna somo la kujifunza. Katika Kurani na hadeeth ya Mtume Muhammad tunaweza kusoma na kuona kwa jicho la akili yetu jinsi hali yetu inaweza kuwa.
Kwa upande mwingine, furaha ilioje kwa walio ingia Peponi. Watapata radhi ya kumwona Mwenyezi Mungu. Hayo ni ya kunyimwa kwa watu wa Jahannamu. "Hakika watakuwa wamefunikwa na kumwona Mola wao siku hiyo." (Kurani 83:15)
Watu wa Peponi na watu wa Jahannamu wakizungumza na familia zao
Hakuna aya nyingi za Kurani au hadeeth kutoka kwa Mtume Muhammad, rehema na baraka za Mungu ziwe juu yake, ambazo zinatuonyesha mazungumzo yanayojiri kati ya watu na familia zao katika makao yao ya milele . Hata hivyo kuna ushahidi wa kuonyesha kwamba watakumbuka maisha yao katika ulimwengu huu na kufikiri juu ya familia zao.
“ Wataelekeana wakiulizana. Watasema: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa, basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto. Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu." (Kurani 52:25-28)
Mazungumzo baina ya Mwenyezi Mungu na watu wa Motoni
Mazungumzo tunayoyakuta baina ya Mwenyezi Mungu na watu wa Jahannamu si mengi. Tunaziona Aya za Kurani, ambapo watu wa Jahannamu wanajadiliana baina yao, au pamoja na Malaika wanaolinda milango ya Jahannamu. Hata hivyo kuna mazungumzo ambayo ni ya kushangaza na yanapaswa kuwa wazi katika akili zetu, ili tujilinde tusiwahi kuyasikia maneno haya ya kutisha. Watasema watu wa Motoni:
“ Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni. Na tufanyapo tena basi kweli sisi ni wenye kudhulumu."
Atasema Mwenyezi Mungu: "Tokomeeni humo, wala msinisemeze." (Kurani 23:107-108)
Mazungumzo baina ya Mwenyezi Mungu na watu wa Peponi
Katika hadeeth ya Mtume Muhammad tunapata mazungumzo yenye kupendeza sana kati ya Mungu na mtu wa mwisho kutoka katika adhabu ya Jahannamu kwa rehema ya Mungu. Mtu huyo anaalikwa kuingia Peponi na hivyo ataenda huko na kudhani kuwa Pepo imejaa. Anarudi kwa Mwenyezi Mungu na kusema: "Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimeona Pepo imejaa." Na Mwenyezi Mungu atasema: "Nenda ukaingie Peponi hakika unayo mle yaliyo bora mara kumi kuliko dunia na yote yaliyomo ndani yake." Akasema Mtume Muhammad: "Huyo ndiye mwenye hadhi ya chini kabisa kati ya watu wa Peponi." [1]
Na mtu mwingine ataulizwa na Mwenyezi Mungu kama ana kila anachotaka, naye atamjibu Mola wake Mlezi akisema: "Naam, lakini napenda kupanda mbegu." Hivyo atakwenda na kupanda mbegu zake, na kwa muda wa kupepesa kwa macho zitakua, kuiva, kuvunwa na kupangwa kama milima.[2]
Tutamalizia msururu wetu wa sehemu tatu kwa msemo mzuri sana kwa matumaini ya kwamba kila mmoja anayesoma au kusikia mazungumzo haya mazuri, atashiriki mazungumzo haya mwisho wa maisha yake duniani na mwanzo wa maisha yake ya Akhera.
Mwenyezi Mungu atawaambia watu wa Peponi: "Enyi Watu wa Peponi! Watajibu: "Sisi tuko hapa Mola wetu Mlezi, na kheri zote ziko mikononi mwako." Mwenyezi Mungu atasema: "Je, mumeridhika?" Watasema: "Kwa nini tusitosheke, na hali umetupa usiyowapa viumbe vyako?" Atasema: "Je! Nisiwape kilicho bora kuliko hicho? Watasema: "Ewe Mola wetu Mlezi! Nini inaweza kuwa bora kuliko hiyo? Mwenyezi Mungu atasema: "Nawapa radhi Zangu, wala sitawakasirikia tena."[3]
Ongeza maoni