Usimfuate Herakyulasi (sehemu ya 1 kati ya 2): Na Ukweli Umewekwa Wazi
Maelezo: Hadithi ya wanaume wawili waliochagua kuhatarisha maisha yao ya milele badala ya kusilimu.
- Na Aisha Stacey (© 2012 NewMuslims.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 10 Jan 2022
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,216
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Katika historia ya Uislamu kuna watu wawili maarufu sana waliokataa kusilimu hata baada ya ukweli kuwekwa wazi kwao. Wanaume hawa waliufahamu na kupendezwa na Uislamu na wao, kila mmoja kwa njia yake, walimpenda Mtume Muhammad. Watu hawa walikuwa ni pamoja na Mfalme wa Roma (Baizantina) Herakyulasi na Abu Talib, ami aliyempenda sana Mtume Muhammad. Wanaume wote wawili waliutambua vyema uzuri wa Uislamu lakini walishinikizwa na waliowazunguka na wakakataa kuukubali Uislamu kama dini yao.
Mtu anapofikiria kusilimu mara nyingi hukabiliwa na misukumo kutoka nje. Hujiuliza, wazazi wangu, mke wangu, au kaka yangu watasema nini. Huko kazini, nitawaambiaje kuwa siwezi tena kwenda baa baada ya kazi? Vitu hivi vinaweza kuonekana vidogo visiyo na maana lakini aghalabu huweza kuwa mambo makubwa ambayo humsababisha mtu kuwaza na kuwazua tena na tena. Hata baada ya mtu kusilimu na furaha ya awali kuisha wanaweza kujikuta wakikabiliwa na shinikizo nyingine zaidi kutoka nje.
Herakyulasi na Abu Talib ni mifano miwili tofauti kabisa ya jinsi mtu anavyoweza kiurahisi kuhatarisha kupata maisha ya Akhera kwa ajili ya mambo ya maisha haya ya muda mfupi.
Herakyulasi – Mfalme wa Roma
Mnamo mwaka wa 628KK Mtume Muhammad alituma barua kwa Herakyulasi akimwalika kuukubali Uislamu. Hii ilikuwa mojawapo ya barua kadhaa ambazo Mtume Muhammad alizituma kwa wakuu wa mataifa mbalimbali. Kila barua iliandikwa kwa njia maalumu kwa ajili ya mtu aliyeandikiwa na Mtume Muhammad. Hivi ndivyo sehemu ya barua aliyoandikiwa Herakyulasi ilivyokuwa;
Ninaandika mwaliko huu ili kukualika katika Uislamu. Ukijiunga na Uislamu utakuwa salama - na Mungu atakuzidishia thawabu zako maradufu, lakini ukikataa mwaliko huu wa Uislamu utabeba madhambi ya kuwapotosha wafuasi wako. Kwa hivyo nakusihi uzingatie mambo yafuatayo: “Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi waola badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakighairi basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.” Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Herakyulasi hakuiharibu barua ile kama Mfalme wa Ufursi (Khusru) alivyofanya, bali aliisoma kwa sauti kubwa kwa watu walioandamana naye na mawaziri wake. Herakyulasi pia aliihifadhi barua hiyo, aliitafakari na kuulizia kuhusu ukweli wake. Alimuuliza Abu Sufyan, adui mkubwa wa Mtume na Uislamu, ambaye alikuwa katika nchi yake kwa ajili ya biashara ya kuuza na kununua. Aliitwa kortini kuhojiwa. Abu Sufyan alisema ukweli kuhusu Mtume Muhammad na Herakyulasi aliweza kuthibitisha ukweli wa madai ya utume wa Muhammad. Herakyulasi aliwaalika watu wake waliohudhuria kortini katika Uislamu. Mwitikio wao wa mwaliko wake ulinakiliwa na Ibn al-Natur.
“Wakuu wake walipokusanyika, aliamuru milango yote ya kasri lake ifungwe. Kisha akatoka nje na kusema, "Enyi Wabaizantino! Iwapo mafanikio ni matamanio yenu na iwapo mnatafuta uongofu wa kweli na mnataka Ufalme wenu udumu, basi wekeni ahadi ya utiifu kwa Mtume aliyejitokeza! "Baada ya kusikia mwaliko huu, Wakuu wa Kanisa walikimbilia milango ya kasri kama kundi la punda wa mwituni, lakini wakapata milango imefungwa. Baada ya Herakyulasi kugundua chuki zao dhidi ya Uisilamu, alikata tamaa kuwa watu wale wangesilimu, na akaamuru warudishwe kwenye ukumbi wa mazungumzo. Waliporudi, alisema, "Kile nilichosema ni kupima tu uthabiti wa msimamo wenu, na nimeuona. "Watu walimsujudia na kumridhia, na Herakyulasi aliupuuza Uislamu.”
Kwa kweli Herakyulasi alikuwa ameshawishika na pia kuvutiwa na yale aliyosoma, na matokeo ya uchunguzi wake. Basi, kwa nini hakuukubali Uislamu? Je, ilikuwa ni hofu ya kupoteza mamlaka yake na cheo chake? Je, ilikuwa ni hofu ya kupoteza maisha yake? Ni bayana, moyo wake ulimili kuukubali Uislamu na bila shaka alijaribu kuwashawishi watu wake, huku akizingatia kwa dhati ushauri wa Mtume Muhammad wa kutowapotosha watu wake mwenyewe. Inaelekea ulimwengu huu wa kiudanganyifu ulimzonga vibaya sana Herakyulasi. Alikufa bila ya kuukubali Uislamu[1].
Hili ni tatizo ambalo wale wanafikiria kubadili dini hukumbana nalo kila siku. Uamuzi wa kubadilisha dini haupaswi kuchukuliwa kijuujuu tu hivi kwa maana ni tukio la kubadilisha maisha. Hata hivyo, zawadi ya Uislamu haipaswi kukataliwa kwani mtu hajui ikiwa atapata nafasi ya kuisoma tena.
Abu Talib
Mtume Muhammad alikuwa na umri wa miaka minane alipokuwa chini ya ulinzi na matunzo ya ami yake Abu Talib. Mtume Muhammad na Abu Talib walikuwa na usuhuba wa karibu sana na wakati Abu Talib alipopata changamoto nyakati za dhiki, Mtume Muhammad alimlelea mmoja wa watoto wake, Ali, ambaye alikuwa mkwe wa Mtume Muhammad na Khalifa wa nne wa taifa la Kiislamu. Kwa kuhubiri ujumbe wa Uislamu, Mtume Muhammad alijiweka katika hatari kubwa. Abu Talib, mtu aliyeheshimika sana Makkah, alimlinda Muhammad kwa kadiri ya uwezo wake. Hata alipohimizwa kumnyamazisha au kumdhibiti mpwa wake aliegemea upande wa Muhammad kwa kumtetea vilivyo.
Ingawa alikuwa mmoja wa waunga mkono imara wa Mtume Muhammad, Abu Talib alikataa kuukubali Uislamu. Hata wakati wa kifo chake kitandani, Mtume Muhammad alimrai aukubali Uislamu, naye akakataa huku akisema aliridhishwa na dini ya mababu zake. Abu Talib aliogopea kuharibu sifa na heshima yake miongoni mwa watu wa Makkah endapo dakika ya mwisho ya uhai wake angeamua kuacha dini ya baba yake na mababu zake. Heshima ile ile iliyomruhusu kumlinda na kumlea Mtume Muhammad kwa zaidi ya miaka arobaini, pamoja na kupitia vipindi vya ukosefu na kunyimwa kwa ajili ya mpwa wake, haingemruhusu asilimu.
Tangu mwanzo wa utume wa Muhammad, wale waliotaka kuingia katika dini mpya walikabiliwa na mateso ya kibinafsi na kufanya maamuzi magumu ya kujisalimisha kwa ajili ya mapenzi ya Mungu. Shinikizo za nje, kama vile mtu kukasirisha jamaa na marafiki zake, au kupoteza kazi kulimaanisha kuwa wengi walihatarisha ustawi wao wa duniani kwa ajili ya Akhera yao. Itakuwa kosa kubwa sana kwa mtu kuuza Pepo yake ya milele kwa faida ya muda mfupi ya ulimwengu huu.
Katika makala inayofuata tutazungumzia jinsi mtu anaweza kukabiliana na shinikizo za kisasa na kutoa baadhi ya miongozo ya hatua za kuchukua ili kuingia katika Uislamu kwa urahisi.
Rejeleo la maelezo:
[1] Kuna wale ambao wanaamini Herakyulasi aliukubali Uislamu kwa siri, hata hivyo uwezo wa kufahamu hilo anao Mwenyezi Mungu pekee.
Usimfuate Herakyulasi (sehemu ya 2 kati ya 2): Masuala ya kisasa na shinikizo za nje
Maelezo: Iwapo mtu anaamini Uislamu ni ukweli, basi anapaswa kusilimu bila kuchelewa.
- Na Aisha Stacey (© 2012 NewMuslims.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 3,770
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Ami mpendwa wa Mtume Muhammad Abu Talib, na Herakyulasi, Mfalme wa Dola ya Baizantina, wote walichagua kutokubali Uislamu. Katika visa vyote viwili tunaweza kuwa na hakika kuwa ulikuwa uamuzi ambao hawakuuchukulia kijuujuu, hata hivyo wote wawili walichagua kutii shinikizo za nje. Badala ya kumcha Mungu pekee walijikuta wakiogopa yale ambayo wengine watafikiria, watasema au watafanya. Leo, zaidi ya milenia baadaye, watu wengi hujikuta katika hali hiyo hiyo. Wanajua au wanahisi kuwa Uislamu ni dini sahihi au ya kweli lakini wanaikataa zawadi ambayo Mungu amewapa.
Kuna shinikizo nyingi katika jamii ya kisasa ambazo hufanya kusilimu kuwa jambo la kukatisha tamaa. Shinikizo za nje zinaweza kuwaweka watu wa kisasa katika nafasi ile ile kama ya kina Abu Talib and Mfalme Herakyulasi. Hata hivyo, Mungu hamwiti mtu katika Uislamu halafu akamwacha. Ikiwa mtu anajua bila shaka kuwa Uislamu ni dini sahihi anaweza pia kuwa na hakika, bila shaka, kwamba Mungu ana mamlaka na nguvu ya kuendelea kuwaongoza na kurahisisha safari yao. Wakati mwingine mlima ulio mbele unaweza kuonekana kuwa mkubwa na wa kutisha lakini mlima ni nini isipokuwa sehemu ya mahuluku vinavyonyenyekea moja kwa moja kwa mapenzi ya Mungu?
“Je, huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu…” (Kurani 22:18)
Mwenyezi Mungu hufanya kuingia katika Uislamu kuwa rahisi lakini sisi, watu, wanadamu, tuna njia isiyo ya kawaida ya kufanya maisha yetu kuwa ngumu na iliyojaa vizuizi ambavyo kwa ukweli havipo.
“…Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu…” (Kurani 5:6)
“…Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu, basi Yeye humtosha…” (Kurani 65:3)
Kauli hii ya Kurani kuhusu utegemezi ni rahisi kusema na kueleweka hata hivyo linapokuja suala la utekelezaji wa utegemezi kamili, huwa sio rahisi kila wakati. Hii ni kwa sababu mbili. Kwa kweli, mtu anapokaribia kuukubali Uislamu, Shetani humshambulia kwa hila na udanganyifu ulioundwa kumwelekeza mtu huyo mbali na njia ya Mungu iliyonyooka. Na pili, watu ambao hawaelewi kabisa asili ya Mungu huelekea kuogopa jinsi familia zao, marafiki zao au wenzao watakavyowachukulia. Abu Talib aliogopa kufikiriwa kama mtu asiyeheshimika angekataa dini ya mababu zake, na Herakyulasi alidhani atapoteza nafasi yake, nguvu zake au maisha yake. Mambo haya hayana faida yoyote yakilinganishwa na neema ya milele au laana, hata hivyo wanadamu hupigana vita kila uchao ili kujitenga na ulimwengu huu wa hadaa.
Mtu anaposilimu mabadiliko kadhaa makubwa hutokea. Mabadiliko ya kuingia katika Uislamu huibua hisia mbalimbali. Kila mtu huanza kujisikia kama mtu aliyebadilika na kwa hivyo huanza kutenda mambo kwa njia tofauti. Maswali, mawazo na matukio hujaza akili zetu, na Shetani hachoki kufanya kazi ya ziada. Pengine Abu Talib aliweza kuyashughulikia maswala hayo hayo, naye Herakyulasi aliajabia maisha yake yangekuwa hatarini ikiwa angesisitiza jambo hilo au kudhihirisha nia yake ya kufuata mafundisho ya Muhammad.
Siku hizi tunajiuliza mfululizo mwingine wa maswali lakini vivyo hivyo huvuruga utulivu wetu. Je, napaswa kuvaa tofauti? Je, niwaambie familia yangu? Je, bado naruhusiwa kwenda nje, kunywa pombe, kupanga miadi ya kukutana na msichana au mwanamke? Yapo mamia ya maswali, lakini ukweli ni kwamba maswali haya hayana uhusiano wowote na mtu kutaka kusilimu au la. Iwapo mtu anaamini Uislamu ni ukweli, basi hana budi kusilimu bila kukawia. Maelezo zaidi yatafuata mtu atakapoanzisha uhusiano na Mungu, atakapoelewa asili ya Muumba wetu.
Kila mtu ana muda wa kuishi uliokadiriwa zamani. Hatujui ni lini tutakufa na dakika inayofuata inaweza kuwa ndiyo ya mwisho wetu katika dunia hii. Kwa sababu hii peke yake mtu lazima asijifananishe na Herakyulasi au Abu Talib. Wanaume wote wawili waliyafuata mapenzi yao ya ulimwengu huu wa hadaa uongoze Akhera yao. Kusilimu kunapaswa kufanyika na kumtegemea Mungu kunapaswa kumwongoza Muislamu mpya kuwa na uhusiano wa maisha pamoja na Mungu.
Kudhihirisha kuwa wewe ni Muislamu sio sharti la kukubali Uislamu. Wakati huo huo, hata hivyo, ni lazima tuyatilie maanani mabadiliko ambayo Uislamu unahitaji kutoka kwetu na kumwomba Mungu aturahisishie njia. Tabia za zamani lazima ziachwe polepole lakini kwa yakini ya kuyamaliza, na vilevile kujifunza juu ya asili ya Mungu na sheria zake kutampa fursa kila mtu abadilike awe aina ya mtu anayependwa na Mungu. Ingawa kusilimu ni tukio la papo kwa hapo, kuwa Muislamu bora kunahitaji juhudi nzuri na endelevu kwa kila mmoja wetu.
Ongeza maoni