Raha za Peponi (sehemu ya 1 kati ya 2)
Maelezo: Makala ya kwanza kati ya sehemu mbili zinazofafanua tofauti za kimsingi kati ya Pepo na maisha ya dunia hii. Sehemu ya 1: Kutokuwepo kwa vile vitu vinavyosababisha huzuni, maumivu na mateso katika maisha haya.
- Na M. Abdulsalam (© 2006 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 29 Nov 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 15 May 2023
- Ilichapishwa: 9
- Imetazamwa: 7,047
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Ukweli wa Pepo ni kitu ambacho watu hawataweza kukielewa mpaka waingie humo, lakini Mwenyezi Mungu ametuonyesha mambo machache ndani ya Kurani. Ameelezea kuwa ni sehemu ambayo kimsingi ni tofauti na maisha ya dunia hii, katika asili na madhumuni ya maisha, pamoja na aina za starehe ambazo watu watafurahia humo. Kurani inawaambia watu kuhusu Pepo, ambayo Mwenyezi Mungu anawapa, inaelezea baraka zake kuu, na inatangaza uzuri wake kwa kila mtu. Inafahamisha watu kwamba Pepo ni mojawapo ya njia mbili za maisha zilizo tayarishwa kwa ajili yao huko akhera, na kwamba kila jambo jema litakuwa lao Peponi kwa kiwango kinachopita uwezo wetu wa sasa wa kufikiria. Inaonyesha pia kwamba Pepo ni mahali ambapo baraka zote zimeumbwa kikamilifu na ambapo watu watapewa kila kitu ambacho nafsi na mioyo yao itatamani, na kwamba watu watakuwa mbali na uhitaji na mahitaji, wasiwasi au huzuni, uchungu na majuto. Kila aina ya uzuri na baraka zipo Peponi na zitafunuliwa kwa ukamilifu ambao haujawahi kuonekana au kujulikana hapo awali. Mungu ametayarisha baraka kama hizo hapo kama zawadi, na hizi zitatolewa kwa watu ambao Yeye amependezwa nao.
Lakini ni nini asili ya furaha hizo peponi , na zitakuwaje tofauti na furaha za ulimwengu huu? Tutajaribu kuangazia baadhi ya tofauti hizi.
Furaha safi bila maumivu na mateso
Ingawa watu katika ulimwengu huu wanapata furaha fulani, kadhalika wanakabiliwa na taabu na mateso mengi. Ikiwa mtu angetathmini maisha wanayoishi, watajua kiwango cha magumu wanayokabiliana nayo yanazidi wepesi na starehe. Maisha ya Akhera hayatakuwa na dhiki wala taabu ndani yake, na watu wataishi humo kwa fahari na furaha tupu. Sababu zote za huzuni, maumivu na mateso wanayopata watu katika maisha haya yatakosekana huko Akhera. Hebu tuangalie baadhi ya sababu hizi.
Utajiri
Mtu anapofikiria mafanikio katika maisha haya, kwa kawaida, hupata taaswira ya nyumba kubwa, vito vya thamani na mavazi, na magari ya gharama kubwa; utulivu wa kifedha unaonekana kuwa ufunguo wa maisha ya furaha. Kwa watu wengi, mafanikio yanahusiana sana na utajiri, ingawa hii ipo mbali zaidi na ukweli. Ni mara ngapi tumewaona matajiri wakubwa wakiishi maisha duni kiasi kwamba wakati mwingine huwapelekea hata kujiua! Utajiri ni kitu ambacho wanadamu kwa asili yao wanatamani kwa gharama yoyote ile, na tamaa hii imeundwa kwa kusudi kubwa na la busara. Wakati tamaa hii haijatimizwa, husababisha kiasi fulani cha huzuni ndani ya mtu. Kwa ajili hiyo, Mwenyezi Mungu amewaahidi wakazi wa Peponi kwamba watapata kila walichokuwa wakikidhania kuhusu mali, kwa wale waliokuwa masikini wa kupindukia, hata walikumbwa na njaa na kiu, kwa wale walio na mali nzuri ambao walitamani hata zaidi. Mungu anatupa maono ya hili anaposema:
“... na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia …” (Kurani 43:71)
“Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita!” (Kurani 69:24)
“… Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri na at'ilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia!” (Kurani 18:31)
Ugonjwa na Kifo
Sababu nyingine ya maumivu na mateso katika maisha haya ni kifo cha mpendwa au ugonjwa, ambayo yote hayapo Peponi. Hakuna atakayehisi ugonjwa au maumivu Peponi. Amesema Mtume Muhammad kuhusu watu wa Peponi rehema na amani ziwe juu yake:
“Hawataugua kamwe, kupiga chafya au kutema mate.” (Saheeh Al-Bukhari)
Hakuna atakayekufa Peponi. Wote wataishi milele wakifurahia starehe zilizomo. Mtume Muhammad alisema kuwa muitaji ataita watu peponi watakapoingia humo:
"Hakika uwe na afya njema na usiwe mgonjwa tena, uishi na usife tena, uwe mchanga na usiwe dhaifu tena, ufurahie, na usihisi huzuni na majuto tena." (Saheeh Muslim)
Mahusiano ya Kijamii
Kuhusu majuto yanayopatikana kwa sababu ya mpasuko katika mahusiano ya binafsi, watu hawatasikia kamwe uovu wowote au maoni au maneno yenye kuumiza katika Pepo. Watasikia tu maneno mazuri na maneno ya amani. Mungu anasema:
“Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi, Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama!” (Kurani 56:25-26)
Hakutakuwa na uadui baina ya watu wala chuki:
“Na tutaondoa chuki vifuani mwao, na mbele yao iwe inapita mito.…” (Kurani 7:43)
Mtume alisema:
“Hakutakuwa na chuki wala hasira baina yao, nyoyo zao zitakuwa moja, na watamtukuza Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni.” (Saheeh Al-Bukhari)
Watu watakuwa na maswahaba bora katika Akhera, ambao pia walikuwa watu bora zaidi duniani:
“Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume – hao wa pamoja na wale alio waneemesha Mwenyezi Mungu – miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!” (Kurani 4:69)
Nyoyo za watu wa Peponi zitakuwa safi, maneno yao yatakuwa mazuri, na matendo yao ni mema. Hakutakuwa na mazungumzo ya kuumiza, kuudhi, kukera au kuchochea, kwani Pepo haina maneno na vitendo vyote visivyofaa. Kama tungejadili sababu zote za uchungu katika maisha haya, bila shaka tungeona kutokuwepo kwake au kinyume chake kuwa ni kweli Peponi.
Raha za Peponi (sehemu ya 2 kati ya 2)
Maelezo: Makala ya pili kati ya sehemu mbili zinazofafanua tofauti za kimsingi kati ya Pepo na maisha ya dunia. Sehemu ya 2: Ubora wa furaha na fahari yake ukilinganisha na maisha haya.
- Na M. Abdulsalam (© 2006 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 29 Nov 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 4
- Imetazamwa: 5,778
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Umilele wa Akhera
Starehe za dunia ni za kupita wakati furaha ya akhera ni ya kudumu na ya milele. Katika maisha haya mtu anapofurahia kitu, ni muda mfupi tu kabla ya kuchoshwa nacho na kuendelea kutafuta kitu anachohisi ni bora zaidi, au anaweza asihisi kukihitaji kabisa. Kwa starehe za Peponi, kamwe mtu hatahisi kuchoshwa na kitu chochote, bali wema wake utaongezeka kila wanapojishughulisha humo.
Pia maisha ya dunia hii ni mafupi sana. Wanadamu wanaishi hapa duniani kwa muda mfupi tu, na ni watu wachache sana wanaofikia umri wa miaka sabini.
“…Sema: Starehe ya dunia ni ndogo, na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kuchamngu...” (Kurani 4:77)
Kuhusu Peponi, watu wataishi milele. Mungu anasema:
“...matunda yake ni ya daima, na pia kivuli chake…” (Kurani 13:35)
“Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyo bakia …” (Kurani 16:96)
“Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyo malizika.” (Kurani 38:54)
Furaha ya Juu
Furaha za watu wa Peponi, kama vile mavazi, chakula, vinywaji, mapambo na majumba yao, zitakuwa bora zaidi kuliko wenzao wa dunia hii. Kwa hakika hakuna nafasi ya kulinganisha, kwani hata nafasi ndogo kabisa katika Pepo ni bora kuliko dunia hii na vyote vilivyomo ndani yake. Mtume Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, amesema:
“Nafasi ya upinde ya mmoja wenu katika Pepo ni bora kuliko zote ambazo jua uchomoza” (Mishkaat al-Masaabiyh 3/85, na. 5615).
Hakuna Uchafu wowote
Pepo haina uchafu wowote wa ulimwengu huu. Kula na kunywa katika maisha haya husababisha haja ya kutoa kinyesi na harufu zake mbaya. Ikiwa mtu anakunywa divai katika ulimwengu huu, anapoteza akili. Wanawake katika ulimwengu huu hupata hedhi na kuzaa, ambayo ni vyanzo vya maumivu na uchungu. Pepo haina usumbufu huu wote: watu wake hawatakojoa, kujisaidia, kutema mate au kuteseka na ugonjwa wa mafua. Mvinyo wa Peponi, kama ilivyoelezwa na Muumba wake, ni:
“Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao, Hakina madhara, wala hakiwaleweshi.” (Kurani 37:46-47)
Maji ya Peponi hayana chumvi, na ladha ya maziwa yake haibadiliki:
“...mito ya maji yasiyo vunda, na mito ya maziwa isiyo haribika ladha yake...” (Kurani 47:15)
Wanawake wa Peponi ni wasafi na hawana hedhi, kutokwa na damu baada ya kuzaa na uchafu mwingine wote unaowapata wanawake katika dunia hii, na wote hawatakua na kinyesi. Mungu anasema:
“...na humo watakuwa na wake walio takasika…” (Kurani 2:25)
Mtume alimjibu mtu pale walipomuuliza vipi watu wa Peponi watajisaidia:
"Wanajisaidia kwa kutokwa na jasho kwenye ngozi zao, na harufu yake itakuwa ya miski, na matumbo yote yatakua yamekonda." (ibn Hibbaan)
Hayo tuliyoyataja yamekuwa ni ulinganisho tu ili kuelewa asili ya Pepo, lakini kama Mungu alivyosema, furaha yake imefichwa kweli.
“Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda.” (Kurani 32:17)
Peponi: Hakuna Kitu Mfano Wake
Furaha za Peponi zinazidi mawazo na kupitiliza maelezo. Hakuna mfano wake kwenye vitu vinavotambulika na watu kwenye ulimwengu huu; hata tuwe na maendeleo kiasi gani, tunachopata sio kitu kwa kulinganisha na furaha ya Akhera. Kama ilivyotajwa katika ripoti kadhaa, hakuna kitu kama Pepo:
"Ni mwanga unaometa, mimea yenye kunukia, jumba la kifalme, mto unaotiririka, matunda yaliyoiva, mke mzuri na mavazi tele, katika makao ya milele yenye furaha tele, katika nyumba nzuri za juu zilizojengwa kwa sauti". (Ibn Maajah, Ibn Hibbaan)
Sahabah alimuuliza Mtume kuhusu majengo ya Peponi naye akajibu kwa maelezo ya ajabu:
“Matofali ya dhahabu na fedha, na chokaa ya miski yenye harufu nzuri, kokoto za lulu na yakuti, na udongo wa zafarani. Yeyote anayeingia humo amejawa na furaha na hatahisi huzuni kamwe; ataishi huko milele na hatakufa kamwe; nguo zao hazitachakaa na ujana wao hautanyauka.” (Ahmad, at-Tirmidhi, ad-Daarimee)
Mungu anasema:
“Na utakapo yaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa.” (Kurani 76:20)
Kile ambacho Mungu ametufichia furaha ya Peponi ni zaidi ya uwezo wetu wa kufahamu. Mtume alisema kuwa Mwenyezi Mungu alisema:
“Nimewaandalia waja Wangu yale ambayo jicho halijaona, sikio halijasikia na moyo wa mwanadamu hauwezi kufikiria.” Soma kama unataka:
“Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda.” (Kuran 32:17)
Katika ripoti nyingine:
“Usijali Mungu amekuambia nini; yale ambayo Yeye hajakuambia ni makubwa zaidi.” (Saheeh Muslim)
Katika makala nyingine, tutajaribu kutaja baadhi ya maelezo makhsusi ya Pepo na starehe zake zilizoelezwa kwetu na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wa mwisho.
Ongeza maoni