Nataka kuwa Mwislamu lakini... Uongo Bunifu kuhusu kusilimu (sehemu ya 1 kati ya 3)
Maelezo: Mungu hufanya kitendo cha kusilimu kuwa rahisi, sio kigumu.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 14 Aug 2022
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 6,202
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Imani kuu ya msingi katika dini ya Uislamu ni kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu. Yeye, ni Peke Yake, wa Kwanza na wa Mwisho, hana washirika, watoto wa kiume, mabinti au wasta. Yuko Peke Yake katika Miliki Yake na Kudura Yake. Ni dhana rahisi sana, ni ukweli mtupu. Walakini, wakati mwingine imani halisi ya Mwenyezi Mungu inaweza kuwazidia au kuwashinda watu. Mara kwa mara tunashangaa tunapomwomba Mwenyezi Mungu na Anatujibu papo hapo.
Dini ya Uislamu inahusisha dhana hiyo rahisi - kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja na imejumuishwa kwenye neno kujisalimisha. Uislamu unamaanisha, kujisalimisha kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu. Mzizi wa neno Uislamu (sa-la-ma) ni lile lile linaloshirikisha neno la Kiarabu lenye maana ya amani na usalama. Kimsingi, amani na usalama hupatikana kwa kuishi maisha kulingana na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Daima, kama mzunguko wa maisha huanzia na kuishia mahali pamoja - hapana mungu ila Mwenyezi Mungu. Tunapojisalimisha kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu, tunakuwa ni Waislamu na ili kudhihirisha uaminifu wetu tunakiri kuwa sisi ni Waislamu kwa kutamka, peke yetu au katika makundi ya Waislamu wengine, Laa ilah illa Allah, Muhammad rasoolu Allah. Hapana mungu wa kweli isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ni mtume Wake.
Wakati wowote mwanadamu yeyote anapopata uzoefu wa na kuelewa huruma ya Mungu, Shetani hujaribu kila awezalo kumdhuru mtu huyo. Shetani hataki tufarijike wala kupata huruma; anataka tuwe na wasiwasi na huzuni. Anataka tufanye makosa na kutenda madhambi. Shetani daima hukata tamaa kupendwa na Mungu, kwa hivyo hutaka kuwapotosha wanadamu wengi kadri ya uwezo wake.
(Shetani akasema) “…Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika Njia yako Iliyonyooka. Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani.” (Kurani 7:16-17)
Wakati wowote mtu anapotambua ukweli na kutaka kuwa Mwislamu, Shetani humjulisha neno 'lakini'. Nataka kuwa Mwislamu...LAKINI! Lakini bado siko tayari. Lakini sizungumzi Kiarabu. Lakini mimi ni mweupe (nina ngozi nyeupe). Lakini sijui chochote kuhusu Uislamu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu alituonya dhidi ya Shetani na hila zake.
“Enyi wanadamu! Asije Shetani kukufitinini…” (Kurani 7:27)
“Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui…” (Kurani 35:6)
Minong'ono ya Shetani hujaribu kutuzuia kusilimu. Mawazo haya hayapaswi kuwa kizuizi baina ya mtu mwenye mafungamano na Mungu, au anayejiunga tena na Mungu Mwingi wa Rehema. Katika mfululizo huu au makala hizi tutajadili baadhi ya mambo maarufu zaidi ya uongo yaliyobuniwa (tutayaita Uongo Bunifu), tutayaweka wazi kwa kuyakagua na kuthibitisha kwamba Mungu ni Mwingi wa Rehema. Yeye husababisha tendo la kusilimu kuwa rahisi, wala sio gumu. Hakuna lakini wala hatihati!
1.Nataka kuwa Mwislamu lakini sitaki kubadilisha jina langu.
Mtu anayeingia katika Uislamu sio lazima abadilishe jina lake. Mtume Muhammad, rehema na amani za Mungu zimshukie yeye, alisema kwamba kila mtu ana haki ya kuwa na jina zuri, jina ambalo lenye maana na linaambatana na sifa. Hii sio shida kwa idadi kubwa ya watu, japo ikiwa utagundua kuwa maana ya jina lako ni baya au limehusishwa na watenda madhambi au madhalimu ni vyema kulibadilisha liwe jina linalokubalika. Ikiwa jina la mtu huyo ni jina la sanamu au linaashiria utumwa wa kitu au mtu mwingine asiyekuwa Mungu, basi lazima libadilishwe. Kumbuka kuwa Uislamu ni rahisi. Iwapo kubadilisha jina lako kirasmi kungesababisha dhiki, wasiwasi au madhara, inatosha kulibadilisha na lijulikane miongoni mwa marafiki na jamaa.
2.Nataka kuwa Muislamu lakini sijui chochote kuhusu Kiarabu.
Dini ya Uislamu iliteremshwa kwa watu wote, katika kila mahali, kwa wakati wote. Hii sio dini maalumu ya Waarabu au wasemaji wa Kiarabu. Kwa kweli, idadi kubwa ya Waislamu bilioni 1.4 ulimwenguni hawana asili ya Uarabu. Mtu anaweza kuwa Mwislamu bila kujua neno moja la Kiarabu; haiathiri uwezo wake wa kuukubali Uislamu. Hata hivyo, lugha ya Kurani ni ya Kiarabu na sala za kila siku zinatekelezwa kupitia Kiarabu, basi ingawa sio lazima kujifunza lugha nzima, baada ya kusilimu itakuwa muhimu kujifunza maneno kadhaa ya Kiarabu kwa ajili ya ibada.
Iwapo mtu hawezi kujifunza Kiarabu cha kutosha kwa lengo la kutekeleza sala zake kwa sababu ya kasoro ya kuongea au pia hawezi kutamka Kiarabu, itabidi ajaribu kadri ya uwezo wake. Na Ikiwa pia kujifunza Kiarabu kwa uchache haiwezekani, basi huondolewa jukumu hili, kwa sababu Mungu habebeshi watu dhiki zaidi ya uwezo wao. Walakini Mungu pia anasema ya kwamba amerahisisha kujifunza Kurani, kwa hivyo ni vyema mtu kujaribu awezalo.
“Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo…” (Kurani 2:286)
“Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Kurani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anayekumbuka?” (Kurani 54:17)
Mtu alienda kwa Mtume akasema: "Ee Mjumbe wa Mungu, nifundishe kitu katika Kurani ambacho kitanitosha, kwa maana siwezi kusoma." Akamwambia, "Sema: Subhaan-Allaah wa’l-hamdu Lillaah wa laa ilaaha ill-Allaah wa Allaahu akbar wa laa hawla wa laa quwwata illa Billaah (Ametakasika Mwenyezi Mungu na kila upungufu, na shukrani na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mkubwa kuliko chochote, na hakuna uwezo wala nguvu ila za Mwenyezi Mungu).”[1]
Kuingia kwenye pote la Uislamu ni rahisi. Ni njia rahisi, isiyo na shida. Katika sehemu ya 2 tutajadili upashaji tohara, ukweli kwamba Uislamu hauna pingamizi za ukabila au uasili na kuwa Mwislamu bila kujua sana juu ya Uislamu.
Nataka kuwa Muislamu lakini... Uongo Bunifu kuhusu kusilimu (sehemu ya 2 kati ya 3)
Maelezo: Mengi kuhusu uongo bunifu unaomzuia mtu kusilimu.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 19
- Imetazamwa: 6,794
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu. Ni kauli rahisi inayofanya kusilimu kuwa rahisi. Kuna Mungu Mmoja tu, na vilevile dini moja, hakuna kitu kinachoweza kuwa rahisi zaidi. Hata hivyo, kama tulivyojadili katika makala iliyopita, wakati wowote mtu anapotambua ukweli na anataka kuwa Muislamu, Shetani humjulisha neno lakini. Nataka kuwa Muislamu...LAKINI. Lakini bado siko tayari. Lakini sizungumzi Kiarabu, au lakini sitaki kubadilisha jina langu. Leo tutajadili uongo bunifu zaidi ambao unawazuia watu kusilimu.
3.Nataka kuwa Muislamu lakini sitaki kutahiriwa.
Mtume Muhammad alisema kuwa kila mtoto alizaliwa katika hali ya fitra, na ufahamu sahihi wa Mungu.[1] na hadithi za Mtume Muhammad zinatuambia kwamba hali zinazohusiana na fitra (hali ya asili ya kuwa) ni tano.
“Vitu vitano ni sehemu ya maumbile: kunyoa mavuzi, kutahiriwa, kupunguza masharubu, kung'oa au kukwanyua nywele za makwapani, na kukata kucha”.[2] Hii inaaminika kuwa ada ya kale, ni njia ya asili, iliyofanywa na Mitume wote, na wakawaamrisha waumini wao waitekeleze kulingana na sheria walizoleta.[3]
Wanazuoni wengi wa Kiislamu wanakubali ya kwamba kutahiriwa ni lazima kwa wanaume mradi wasiwe na hofu ya kwamba inaweza kuwaletea madhara. Wakati wa kukadiria kiwango cha madhara ni lazima mtu atumie mafundisho sahihi ya Kurani pamoja na mwongozo sahihi wa hadithi za Mtume Muhammad. Iwapo mwanamume hana uwezo wa kutahiriwa kwa sababu ya woga wa kupata jeraha au kwa sababu nyingine yoyote halali ambayo inaweza kufanya maisha yake yawe ya taabu basi wajibu huu umeondolewa kwake. Hairuhusiwi suala hilo kuwa kizuizi ambacho kitamzuia mtu kuukubali Uislamu[4]. Kwa maneno mengine, hii sio sharti ya kuwa Muislamu. Pia, haimzuii mtu kuongoza sala.[5]
Hakuna sharti la kupashwa tohara kwa mwanamake katika Uislamu.
4.Nataka kuwa Muislamu lakini asili yangu ni ya rangi nyeupe.
Uislamu ni dini ambayo iliteremshwa kwa watu wote, katika kila mahali, kwa wakati wote. Haikupelekwa kwa ajili ya watu wa asili fulani au kabila maalumu. Ni njia kamili ya maisha inayoambatana na mafundisho yanayopatikana katika Kurani na hadithi sahihi zenye kuelezea mwenendo wa Mtume Muhammad. Ingawa Kurani iliteremshwa kwa lugha ya Kiarabu na Mtume Muhammad alikuwa Mwarabu, itakuwa makosa kudhani kuwa Waislamu wote ni Waarabu, au vivyo hivyo, kuwa Waarabu wote ni Waislamu. Kwa kweli idadi kubwa ya Waislamu bilioni 1.4 ulimwenguni sio Waarabu.
Hakuna mahitaji ya rangi ya uasili au ukabila kwa mtu kuwa Muislamu. Katika hotuba yake ya mwisho Mtume Muhammad alisisitiza ukweli huu kwa maneno machache ya wazi.
“Wanadamu wote nasaba yao inatokana na Adamu na Hawa, Mwarabu hana ubora juu ya asiye Mwarabu na asiye Mwarabu hana ubora juu ya Mwarabu; mwenye uasili wa weupe hana ubora juu ya mwenye uasili wa weusi wala mwenye uasili wa weusi hana ubora juu ya mwenye uasili wa weupe, isipokuwa kwa uchaji Mungu na matendo mema. Jueni kuwa kila Muislamu ni ndugu wa kila Muislamu na kwamba Waislamu ni ndugu moja.”[6]
“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane…” (Kurani 49:13)
5.Nataka kuwa Muislamu lakini sijui chochote kuhusu Uislamu.
Hakuna haja ya kujua mengi kuhusu Uislamu ili kuwa Muislamu. Inatosha kujua maana ya shahada na nguzo sita za imani. Pindi tu mtu atakapoukubali Uislamu, kuna muda wa yeye kujifunza kuhusu dini yake. Hakuna haja ya kukimbilia mambo kwa pupa kisha ukazidiwa. Nenda polepole, lakini usonge mbele kwa kasi yako mwenyewe. Kuna muda wa kufahamu uzuri wa ushawishi wa Uislamu na wepesi wake, na pia kujifunza kuhusu mitume wote na wajumbe wa Uislamu akiwemo mtume wa mwisho, Muhammad. Muislamu haachi kujifunza; ni mchakato ambao utaendelea hadi kifo.
Mtume Muhammad alisema, "Muumini hatatosheka kusikiliza mambo ya kheri (kutafuta elimu) hadi atakapofikia Peponi.”[7]
6.Nataka kuwa Muislamu lakini nimefanya madhambi mengi.
Mtu anapotamka shahada, ninakiri ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu na nakiri ya kwamba Muhammad ni mjumbe Wake, anakuwa kama mtoto mchanga aliyezaliwa. Madhambi yake yote yaliyopita, hayajalishi ni makubwa au madogo, hufutwa yote. Rekodi huwa safi, haina dhambi lolote, hung'ara na nyeupe; huu ni mwanzo mpya.
“Waambie wale waliokufuru kuwa wakikoma, watasamehewa yaliyokwisha pita…” (Kurani 8:38)
Hakuna kulazimishwa kwa mtu yeyote kuukubali ukweli wa Uislamu. Hata hivyo, ikiwa moyo wako unakuambia kuna Mungu mmoja tu, usisite.
“Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uongofu umekwishapambanuka na upotofu. Basi anayemkataa Shetani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.” (Kurani 2:256)
Rejeleo la maelezo:
[1] Saheeh Muslim
[2] Saheeh Al-Bukhari, Saheeh Muslim
[3] AS-Shawkaani, Nayl al-Awtaar, Baab Sunan al-Fitrah
[4] Fataawa al-Lajnah al-Daa’imah, 5/115, Al-Ijaabaat ‘ala As’ilah al-Jaaliyaaat, 1/3,4
[6] Matini ya Hotuba ya Mwisho yanaweza kupatikana katika Saheeh Al-Bukhari na Saheeh Muslim, na kwenye vitabu vya Tirmidhi na Imam Ahmad.
[7] At Tirmidhi
Nataka kuwa Muislamu lakini... Uongo Bunifu kuhusu Kusilimu (sehemu ya 3 kati ya 3)
Maelezo: Madhambi, kuogopa watu wengine watasema nini, au kutojua Waislamu wowote hakumzuii mtu kusilimu.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,170
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Tulimaliza Sehemu ya 2 kwa kutaja ya kwamba mtu anaposilimu basi madhambi yake yote yaliyopita, hayajalishi ni makubwa au madogo, hufutwa. Rekodi huwa safi, haina dhambi lolote, hung'ara na ni nyeupe; huu ni mwanzo mpya. Hata hivyo, kuna watu wengine ambao wangesita kuukubali Uislamu kwa sababu wanaogopa kuwa hawataweza kuacha kuendelea kufanya dhambi. Tunaanza Sehemu ya 3 kwa kujadili mada hii.
7. Nataka kuwa Muislamu lakini najua kuna madhambi mengine siwezi kuacha kuyafanya.
Iwapo mtu anaamini ukweli ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, anapaswa kuukubali Uislamu bila kuchelewa, hata kama wanaamini ya kuwa wataendelea kutenda dhambi. Mtu akizoea kuishi maisha bila kubanwa na maadili yoyote, Uislamu unaweza kuonekana mwanzoni kama seti ya sheria na kanuni ambazo haziwezekani kutimizwa. Waislamu hawanywi pombe, Waislamu hawali nyama ya nguruwe, wanawake wa Kiislamu ni lazima wavae mitandio, Waislamu ni lazima wasali mara tano kila siku. Wanaume na wanawake hujikuta wakisema maneno kama, "Nisingeweza kuacha kunywa", au "Ningeona ugumu sana kusali kila siku seuze mara tano”.
Ukweli ni kuwa, mara tu mtu anapokubali ya kwamba hapana mungu anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kukuza uhusiano na Yeye, sheria na masharti hayazingatiwi kwa undani. Ni njia ya taratibu ya kutaka kumridhisha Mwenyezi Mungu. Kwa wengine, kukubali miongozo kwa ajili ya maisha ya furaha huchukua siku, hata saa, kwa wengine inaweza kuwa wiki, miezi, au hata miaka. Safari ya kila mtu kuingia katika Uislamu ni tofauti. Ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu husamehe madhambi yote. Muumini anaweza, kwa rehema ya Mungu, kuingizwa Peponi bila kuzingatia madhambi aliyotenda. Kwa upande mwingine, asiyeamini, anayeabudu kitu kingine au mtu mwingine asiyekuwa Mungu Mmoja wa Kweli, ataingizwa Moto wa milele. Kwa hivyo, ukipewa chaguo kati ya kutokubali kabisa Uislamu au kuwa Muislamu anayetenda dhambi, chaguo la pili kwa hakika ni borazaidi.
8. Nataka kuwa Muislamu lakini ninaogopa kuwajulisha wengine.
Kama tulivyosisitiza mara kwa mara kuwa hakuna kitu ulimwenguni ambacho kinamzuia mtu kuukubali Uislamu. Iwapo mtu anaogopa watu wengine watasema nini, kama vile wazazi wake, ndugu zake au marafiki zake, na anahisi kuwa hayuko tayari kuwajulisha, itabidi asilimu na kujaribu kuutekeleza Uislamu kwa siri kadri ya uwezo wake. Muda unavyosonga, na uhusiano wake na Mwenyezi Mungu umeimarika, imani ya mtu itakuwa na nguvu na atajua jinsi ya kushughulikia hali hiyo vizuri. Kwa kweli Muislamu mpya atajihisi huru na kuona haja ya kufahamisha ulimwengu wote juu ya uzuri wa Uislamu.
Wakati huo huo ni vizuri kuwatayarisha polepole na kwa ustadi marafiki zako na familia kuhusu mabadiliko ambayo yatajitokeza. Labda mtu anaweza kuanza kuzungumza waziwazi juu ya Mungu na dini kwa ujumla, kueleza kuvutiwa kwake na imani zingine au Uislamu hasa. Mtu anapoanza kuufuata Uislamu, ambao kwa kweli ni njia ya maisha, wale waliokaribu naye aghlabu hugundua tofauti fulani. Wataona heshima mpya inayopatikana kwao, familia na jamii kwa ujumla; wataona pia mabadiliko ya tabia kutoka wasiwasi na kutokuwa na furaha hadi kutulia na kutosheka.
Uislamu ni njia ya maisha na ni vigumu kuificha kwa muda mrefu. Ni muhimu kukumbuka kuwa watu watakapojua umesilimu kutatokea athari fulani. Kuna wale watafurahi na kukubali, ilhali wengine watakasirika na kusikitika. Mara nyingi wale wanaokasirika, hukubali mabadiliko baada ya muda kupita. Na wanapoona mabadiliko mengi mazuri kwako, wanaweza kuanza kuthamini uongofu wako. Mtu anahitaji kuwa imara, akiamini na kujua Mungu yuko pamoja naye. Maneno yako na tajriba yako huenda ikawaongoza wengine kufuata mfano wako. Mtegemee Mungu, jifunze yote unayoweza kujua kuhusu imani yako mpya na uwezeshe nuru ya Uislamu iangaze kupitia macho yako.
9. Nataka kuwa Muislamu lakini sijui Waislamu wowote.
Watu wengine hujifunza kuhusu Uislamu kupitia kusoma, wengine kwa kutazama tabia ya Waislamu wanaowaona katika miji yao, wengine kupitia vipindi katika runinga na wengine, kupitia sauti ya wito kwenda kusali (adhana). Mara nyingine watu hutafuta na kupata uzuri wa Uislamu bila kukutana na Muislamu yeyote. Sio lazima kujua Waislamu kabla ya kusilimu.
Kusilimu ni rahisi kama kusema maneno haya, Nakiri ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu na pia nakiri ya kwamba Muhammad ni mjumbe Wake. Kusilimu sio lazima kufanywe msikitini (au kituo cha Kiislamu) na wala mashahidi hawahitajiki. Mambo haya yote, hata hivyo, ni dhihirisho la udugu wa Waislamu na dalili ya mwanzo wa imani mpya ya mtu akisaidiwa na kushirikiana na wenzake katika imani. Ikiwa hakuna kituo cha Kiislamu karibu au Waislamu kukusaidia, mtu anaweza kufuata utaratibu ulioelezwa katika "Jinsi ya Kusilimu na kuwa Muislamu”.
Baada ya kusilimu ni muhimu kwa huyo Muislamu mpya kuwasiliana na Waislamu wengine. Wafuasi wenzako wa imani mpya wanapatikana katika misikiti unapoishi na vituo vya Kiislamu, au kujitambulisha kwa Muislamu anayeishi mtaani kwenu, anayetumia usafiri wa basi moja kama wewe, au anayefanya kazi katika kampuni hiyo hiyo na wewe. Ingawa Muislamu mpya atajihisi yuko peke yake, bado ana uhusiano na Waislamu wengine bilioni 1.5.
Kabla ya au baada ya kusilimu, tovuti hii ipo kusaidia Waislamu wapya au wale wanaofikiria kuwa Waislamu. Utapata humu mamia ya makala kuhusu Uislamu ambazo ni rahisi kueleweka. Baada ya kusilimu, tovuti hii itakusaidia kuanza kama Muislamu mpya kwa kukupa nyenzo muhimu na usaidizi wa mtandaoni kupitia Live-Chat (Gumzo ya Moja kwa Moja).
Ongeza maoni